WAKAZI na viongozi wa jamii katika Kaunti ya Kwale wamepinga kutengwa katika mipango ya uchimbaji wa madini adimu na Niobium katika Mrima Hill, yanayokadiriwa kuwa na thamani ya Sh8 trilioni.
Jamii hiyo imelalamikia kupata taarifa kuhusu uteuzi wa muungano wa kampuni za Amerika kuendeleza mradi huo kupitia vyombo vya habari, bila kushirikishwa katika maamuzi muhimu.
Ingawa hawapingi uchimbaji, wakazi wanataka serikali iwashirikishe, ifanye tathmini ya kina ya athari za mradi kwa mazingira na jamii, na kuweka wazi namna mapato yatakavyogawanywa kati ya serikali ya kitaifa, kaunti na jamii husika.
Alhamisi iliyopita, Waziri wa Madini, Hassan Joho, alitangaza muungano wa kampuni zilizoshinda zabuni ya kuendeleza uchimbaji huo.
Kwa vizazi vingi, familia zinazoishi maeneo ya Mrima zimekuwa zikitegemea kilimo na ufugaji kujipatia riziki.
Hata hivyo, sasa zinahofia kupoteza mashamba na maeneo ya malisho, kulazimishwa kuhama, mmomonyoko wa udongo na uchafuzi wa vyanzo vya maji.
Aidha, kuna wasiwasi kuwa shughuli hizo zinaweza kuharibu maeneo ya kitamaduni na madhabahu yanayochukuliwa kuwa matakatifu na jamii.
Mzee wa Kaya, Masudi Mwarezo, alisema jamii haijashirikishwa ipasavyo licha ya Katiba kutaka wananchi washirikishwe katika maamuzi yanayowaathiri.
Alionya kuwa huenda wakazi wakanyimwa manufaa ya kiuchumi, kama walivyodai kutokea wakati wa shughuli za kampuni ya Base Titanium.
Alitaja vijiji vitano vya Bumbuni, Herani, Mwabovo, Dzuni na Mwachanongo, vinavyojulikana kama Lango la Baraka, kuwa miongoni mwa maeneo yatakayoathiriwa.
Mwarezo, ambaye ni mwenyekiti wa Mrima Hill Community Resource Trust, alisema mradi huo unaweza kuathiri madhabahu saba katika maeneo ya mlima huo na nyingine kuu iliyo katikati ya mlima.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Misitu ya Jamii cha Mrima, Ayubu Suya, alisema tathmini ya athari za mazingira inapaswa kuzingatia pia taasisi na rasilimali za jamii.
Alisema wazee wa Kaya wamebainisha rasilimali 32 za kitamaduni na kiasili, zikiwemo miti, mimea ya dawa na madhabahu.
Mwanapili Omar Suleiman, 65, alisema kampuni za kigeni zimekuwa zikifanya shughuli mbalimbali katika eneo hilo tangu miaka ya 1960 bila kuwapa wakazi maelezo ya kutosha.
Alisema familia zina wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuhama na hatima ya makazi na shughuli zao za kiuchumi.
Umiliki wa ardhi pia umeibua utata, huku baadhi ya maeneo yakidaiwa kumilikiwa kwa pamoja na jamii licha ya zoezi la upimaji lililofanyika kati ya 1992 na 1998.
Mbunge wa Lunga Lunga, Chiforomodo Munga, alisema viongozi hawajapewa taarifa za kutosha kuhusu mradi huo, licha ya Joho kuahidi kuwa ushirikishwaji wa umma ungefanyika.
Gavana wa Kwale, Fatuma Achani, pia amesisitiza kuwa serikali ya kaunti na wakazi washirikishwe ili kuhakikisha wanapata manufaa ya kiuchumi.
Akijibu malalamishi hayo, Joho alisema kampuni zilizochaguliwa zitalazimika kushauriana na jamii, wamiliki wa ardhi na uongozi wa kaunti, na kupata ridhaa zinazohitajika kabla ya kuanza shughuli za utafutaji madini.
Serikali ya Amerika imesifu uteuzi huo, ikisema mradi unaweza kuleta teknolojia mpya, nafasi za kazi na kukuza uongezaji thamani wa madini nchini.
Serikali yabanwa kuhusu uwazi wa madini ya Mrima
Taifa Leo 3 min read

This story was originally published by Taifa Leo.
Read the full story at Taifa LeoRelated stories
News2027: Tinubu’s ‘Emi lo kan’ becomes ‘Awa lo kan’, says Lagos APC
According to the party, the Tinubu political project has evolved from the “Emi lo kan” declaration that preceded the 2023 presidential election to the emerging “Awa lo kan” sentiment ahead of 2027.
Vanguard News 1 min read
News2027: Tinubu won’t be included in my national unity govt — Makinde
Makinde accused Tinubu of failing to replicate such an inclusive approach, alleging that the president's appointments were largely drawn from his political circle.
Vanguard News 1 min read
NewsVIONGOZI WATAKIWA KUTEKELEZA KWA VITENDO AGIZO LA RAIS SAMIA
Millard Ayo Video
NewsKenyan chef arrested in Nigeria over alleged drug smuggling
NDLEA arrested a Kenyan chef and South African golfer over alleged drug smuggling, exposing luggage tag swaps and tracking devices used by the syndicate.
Tuko 1 min read