IRINGA: CHUO Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kimeanza kutoa programu za masomo zinazohusiana na Akili Unde (Artificial Intelligence – AI) na Sayansi Data (Data Science), hatua inayokifanya kuwa miongoni mwa taasisi za elimu ya juu nchini zinazopanua fursa za mafunzo katika taaluma zinazohitajika zaidi katika uchumi wa kidijitali.

Hatua hiyo inaashiria mabadiliko katika mfumo wa elimu ya juu nchini, ambapo wanafunzi wanaweza kupata mafunzo katika taaluma hizo ndani ya Tanzania badala ya kutegemea kwenda nje ya nchi kama ilivyokuwa ikifanyika kwa baadhi ya vijana waliokuwa wakidhaminiwa na Serikali kusomea maeneo hayo.

Akizungumza katika Mahafali ya 18 ya chuo hicho yaliyofanyika chuoni hapo mjini Iringa, Mkuu wa MUCE, Prof. Method Semiono, alisema chuo hicho kimeanzisha programu mpya za masomo zinazolenga kukidhi mahitaji ya sasa ya soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia duniani.

Alizitaja programu hizo kuwa ni pamoja na Shahada ya Sanaa katika Tafsiri na Ukalimani (Bachelor of Arts in Translation and Interpretation), Shahada ya Sanaa katika Historia, Nyaraka na Urithi (Bachelor of Arts in History, Archives and Heritage Studies), pamoja na Stashahada ya Uzamili katika Ubunifu wa Kijamii na Ujasiriamali (Postgraduate Diploma in Social Innovation and Entrepreneurship).

Alisema kuanzishwa kwa programu hizo, pamoja na zile zinazohusiana na Akili Unde na Sayansi Data, kumeongeza uwezo wa chuo kudahili wanafunzi wapya kwa takribani 400 katika mwaka huu wa masomo.

“Kutokana na kukosekana kwa kozi zinazohusiana na maeneo haya nchini, Serikali imekuwa ikiwapeleka vijana wa Kitanzania kusoma masuala hayo nje ya nchi. Naomba kuutaarifu umma kuwa kwa sasa mafunzo haya yanapatikana Tanzania katika Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa,” alisema.

Mbali na upanuzi wa programu za masomo, MUCE imekamilisha ujenzi wa majengo matano kati ya saba yaliyokuwa yakiendelea kujengwa, kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 20, hatua inayotarajiwa kupunguza changamoto za miundombinu na kuongeza uwezo wa chuo kutoa huduma za elimu.

Majengo yaliyokamilika ni Jengo la Sayansi, Maabara ya Fizikia, Jengo la Midia Anuwai na Elimu Maalumu pamoja na mabweni mawili ya wanafunzi, yenye uwezo wa kuchukua takribani watu 2,500 kwa wakati mmoja.

Prof. Semiono alisema kukamilika kwa majengo hayo kumeongeza nafasi za ofisi kwa watumishi, uwezo wa kudahili wanafunzi na kupunguza changamoto ya malazi iliyokuwa ikiwalazimu baadhi ya wanafunzi kupanga nyumba mitaani katika mazingira yasiyofaa kwa masomo ya elimu ya juu.

Majengo hayo yalizinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius John Ndejembi, Oktoba 18, 2026, katika ziara iliyokuwa ya kihistoria kwa kuwa ilikuwa mara ya kwanza kwa Makamu wa Rais kutembelea chuo hicho.

Katika kuimarisha uwezo wa kufundisha na kujifunza, chuo hicho pia kimetumia Sh milioni 196.1 kuboresha miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ikiwemo kuweka mfumo wa kisasa wa intaneti unaotumia mkongo wa mawasiliano (fibre optic) na mifumo mipya ya ulinzi wa mtandao.

Maboresho hayo yamewezesha kurejeshwa kwa huduma za simu za mezani zipatazo 50 baada ya kukosekana kwa zaidi ya miaka 15, huku mifumo ya maktaba na huduma nyingine za kidijitali ikiimarishwa.

Aidha, MUCE imeanzisha mfumo wa ufundishaji kwa njia ya mtandao na masafa unaojulikana kama MUCE Virtual Learning Environment (MUCE VLE), utakaowawezesha wanafunzi kupata elimu bila kulazimika kuhudhuria chuoni ana kwa ana.

Mfumo huo unatarajiwa kuongeza nafasi za upatikanaji wa elimu kwa watu walio katika ajira na wenye majukumu mengine, huku chuo kikitarajia kuongeza idadi ya wanafunzi kinaoweza kuwahudumia.

Chuo pia kimeweka studiojanja (Smart Studio) ya kwanza katika historia yake, itakayowezesha ufundishaji kwa njia ya video, mikutano na makongamano ya mtandaoni, pamoja na kufundisha madarasa zaidi ya moja kwa wakati mmoja.

Katika hatua nyingine, uwezo wa intaneti umeongezwa kutoka megabaiti 305 hadi 400 kwa sekunde (Mbps), kutoka 105 Mbps mwaka 2025, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukifanya chuo kuwa kampasi janja (Smart Campus).

Akizungumzia nafasi ya wahitimu katika maendeleo ya nchi, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Balozi Mwanaidi Sinare, aliwataka kutumia maarifa waliyopata kubuni fursa za kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine badala ya kutegemea kuajiriwa pekee.

Alisema wahitimu wanapaswa kuimarisha stadi za karne ya 21, zikiwemo ubunifu, fikra tunduizi, mawasiliano, ushirikiano, utatuzi wa changamoto na ujuzi wa kidijitali ili kukabiliana na ushindani katika soko la ajira la kitaifa na kimataifa.

Aliwataka pia kuzingatia maadili, uzalendo na matumizi sahihi ya teknolojia, akisisitiza kuwa elimu wanayoipata inapaswa kuonekana katika mwenendo wao na mchango wao kwa jamii.

Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 1,785 wa shahada za awali walitunukiwa shahada zao na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Jakaya Kikwete ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne. Kati yao, wanaume walikuwa 956, sawa na asilimia 53.6 ya wahitimu wote, huku wanawake wakiwa 829, sawa na asilimia 46.4.

Wahitimu hao walitoka katika fani tano, ambazo ni Elimu Jamii na Ualimu (563), Elimu katika Elimu Jamii (336), Elimu katika Sayansi (368), Sayansi katika Kemia (24), pamoja na Sayansi na Ualimu (494).

Kwa upande wa Digirii za Umahiri, wanafunzi 14 wamefuzu na kutunukiwa digirii hizo ambao kati yao wanafunzi nane ni wa kiume.