PENDEKEZO la Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kuanza kutoa vyeti maalumu kuruhusu walimu kuendelea kufundisha limezua mjadala mkali, huku wadau wa elimu wakitofautiana kuhusu mamlaka ya tume hiyo kusimamia ajira na pia kudhibiti taaluma ya ualimu.


Pendekezo hilo limo katika Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya TSC wa 2026, unaolenga kufanya mafunzo ya mara kwa mara ya kuwaongezea walimu ujuzi kuwa ya lazima. Walimu watakaokosa kushiriki mafunzo hayo wanaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu.


Hata hivyo, wadau wanatofautiana kuhusu mpango huo. Baadhi wanataka kuundwa kwa chombo huru kitakachosimamia mafunzo na utoaji wa vyeti vya kitaaluma, huku wengine wakitaka serikali ihakikishe walimu hawalazimishwi kulipia mafunzo hayo.


Kifungu cha 28 cha mswada huo kinapendekeza kubadilishwa kwa Kifungu cha 35 cha Sheria ya TSC ili kuipa tume jukumu la kuhakikisha walimu wote wanazingatia viwango vya taaluma ya ualimu.Mswada huo unapendekeza tume iwalazimishe walimu wote waliosajiliwa kushiriki mafunzo ya kuendeleza ujuzi wao na kisha kuwapa vyeti vya kuwaruhusu kuendelea kufundisha.


Mwalimu atakayekosa kutimiza masharti hayo atakabiliwa na hatua za kiutawala zitakazofafanuliwa katika kanuni.Pendekezo hilo lina maana kwamba hata walimu ambao wamesajiliwa na TSC na wamehudumu kwa miaka mingi watalazimika kutimiza masharti mapya ili kupata vyeti hivyo.Ingawa usajili wa TSC unatambua mwalimu kuwa amekidhi masharti ya kujiunga na taaluma, cheti kipya kitategemea ushiriki wake katika mafunzo ya mara kwa mara.


Hata hivyo, mswada haujaeleza vyeti hivyo vitakuwa halali kwa muda gani, vitafanywa upya baada ya kipindi gani, au kama walimu watalazimika kuvilipia. Pia haujaweka wazi muda wa mafunzo hayo wala atakayeyagharamia.


Chama cha Wadau wa Elimu nchini kimepinga pendekezo hilo, kikisema TSC haipaswi kuwa mwajiri na wakati huo huo kuwa msimamizi wa leseni za taaluma.Katibu Mkuu wa kitaifa wa chama hicho, Ndung’u Wangenye, alisema Bunge linapaswa kupitisha sheria ya kuunda chombo huru kitakachosimamia mafunzo na kutoa vyeti vya kitaaluma kwa walimu.


Alisema jukumu la TSC linapaswa kubaki kuwa kuajiri walimu, kama vile serikali za kaunti, shule za kibinafsi na bodi za usimamizi wa shule zinavyoajiri.Kwa upande mwingine, Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kati (Kuppet), kimeunga mkono pendekezo hilo, kikisema mafunzo ya mara kwa mara yatawasaidia walimu kutambua udhaifu wao na kuboresha maarifa na ujuzi.


Naibu Katibu Mkuu wa Kuppet, Moses Nthurima, alisema mafunzo yatakayofanyika mtandaoni yatawapa walimu nafasi ya kuchagua maeneo wanayohitaji kuimarisha na kujifunza kwa wakati unaowafaa.A


lisema mfumo huo unatumika katika taaluma nyingine duniani, akitaja mawakili, wahandisi na masoroveya ambao hulazimika kuhudhuria mafunzo ili kudumisha leseni zao za kazi.Aliongeza kuwa vyeti hivyo vinaweza kuwasaidia walimu wa Kenya kupata nafasi za ajira nje ya nchi kwa kuwa vitatoa ushahidi wa ziada kuhusu uwezo wao wa kitaaluma.


Hata hivyo, Kuppet inakiri kuwa kuna changamoto ya TSC kuwa mwajiri na mdhibiti wa taaluma kwa wakati mmoja. Bw Nthurima alisema hali hiyo imetokana na mfumo uliowekwa na Katiba na kwamba walimu wanapaswa kukubali mfumo uliopo hadi mabadiliko yatakapofanywa.


Naye Bw Boaz Waruku wa kundi la Elimu Bora Working Group, alisema anaunga mkono mafunzo ya mara kwa mara kwa sababu yanaweza kuinua viwango vya ufundishaji.Hata hivyo, alionya kuwa walimu hawapaswi kubebeshwa gharama za mafunzo hayo.


Alisema kama TSC inawataka walimu kujiendeleza kitaaluma, basi kama mwajiri ina wajibu wa kugharamia mafunzo yao. “Utekelezaji wa mpango huu haupaswi kuwa kwa gharama ya mwalimu,” alisema.


Bw Waruku pia aliunga mkono wazo la kutenganisha majukumu ya TSC kama mwajiri na mdhibiti wa taaluma, akisema chombo maalumu kinaweza kuundwa ndani ya mfumo wa sasa wa kikatiba kusimamia udhibiti wa taaluma.


Alisema utaratibu huo utasaidia kuimarisha uwajibikaji na kuondoa mgongano wa maslahi unaoweza kujitokeza pale taasisi moja inapokuwa mwajiri na mdhibiti wa wafanyakazi wake


.“Kuendeleza ujuzi ni jambo la kawaida katika taaluma ya sheria, udaktari na uhandisi. Kinachopaswa kujadiliwa ni nani atakayelipia mafunzo hayo,” alisema.Aliongeza kuwa mwajiri ana wajibu wa kuendelea kuwapa wafanyakazi wake mafunzo, hivyo TSC inapaswa kugharimia mpango huo badala ya kuwatwika walimu mzigo wa ziada.