DAR ES SALAAM: MAMA na baba lishe wa Kata ya Vijibweni, Wilaya ya Temeke, wamepatiwa elimu kuhusu matumizi ya mkaa mbadala katika juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Elimu hiyo imetolewa na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), kwa kushirikiana na kampuni ya EcoPower, ikiwa na lengo la kuwajengea washiriki uelewa kuhusu matumizi ya nishati mbadala katika shughuli zao za kila siku za upishi.

Katika mafunzo hayo, washiriki wameelekezwa namna ya kutumia mkaa huo, ambao unaweza kudumu hadi saa sita wakati wa kupika vyakula mbalimbali.

Mafunzo hayo yamewalenga wafanyabiashara wadogo wa chakula wanaotumia nishati katika shughuli zao za kila siku za upishi.

Akizungumza leo, Novemba 24, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Petroli wa PBPA, Mhandisi Bruno Tarimo, amesema mkaa huo hauna madhara kwa afya na kwamba matumizi yake yanasaidia kulinda mazingira.

“Mkaa mwingi unasafirishwa kutoka mikoani, tayari hapo kunakuwa na athari za kimazingira,” amesema Tarimo.

Amesisitiza kuwa kuna pia majiko ya umeme ambayo yamepimwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kubainika kuwa na matumizi madogo ya umeme, hivyo kuwataka mama na baba lishe kuyatumia.

Aidha, tani 1,500 za mkaa mbadala zimegawiwa bure katika mafunzo hayo kwa lengo la kuwahamasisha mama na baba lishe kuachana na matumizi ya kuni na vyanzo vingine vya nishati isiyo safi, ikiwemo mkaa wa kawaida.

Tarimo amewataka mama na baba lishe kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika jamii.

Akizungumzia mafanikio ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, Rais wa Mama na Baba Lishe amesema kampeni mbalimbali za uhamasishaji zimechangia kwa kiwango kikubwa kuongeza mwitikio wa kundi hilo katika matumizi ya nishati safi.

Ameiambia HabariLEO kuwa awali baadhi ya wanufaika waliokuwa wamegawiwa mitungi ya gesi walikabiliwa na changamoto ya kushindwa kuendelea kuitumia baada ya gesi kuisha kutokana na gharama za kujaza mitungi hiyo.

Nilifuatilia nibadili mfumo, nilikuwa napita maeneo ya mama lishe, natafuta kiongozi mmoja ambaye kila siku atakuwa anakusanya Sh 1,000 kwa ajili ya kuwezesha kujaza mitungi,” amesema.

Ameongeza kuwa mfumo huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa, ambapo kwa sasa hakuna mama lishe anayehifadhi mtungi baada ya gesi kuisha kwa sababu ya kukosa fedha za kujaza.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaeleza kuwa Tanzania inalenga kufikia asilimia 100 ya matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2050, huku ikilenga kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.

Kwa upande wake, mama lishe Mwashamba Mkwawa amesema amefurahishwa na matumizi ya mkaa mbadala, akieleza kuwa awali alikuwa akitumia hadi Sh 80,000 kwa ajili ya mkaa, lakini sasa ananufaika na mkaa mbadala unaouzwa kwa Sh 13,000 kwa kiloba kinachoweza kutumika kwa wiki mbili.