ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Mike Sonko, ataendelea kuhudumu kama kiongozi wa chama cha National Economic Development Party (NEDP) baada ya Mahakama Kuu kukataa kwa mara ya pili ombi la kumzuia kushikilia wadhifa huo.
Jaji Roselyne Aburili alikataa ombi jipya lililowasilishwa na wakili Nick Sanare, aliyetaka Sonko azuiwe kutumia mamlaka ya kiongozi wa chama hicho hadi kesi inayopinga ufaafu wake iamuliwe.
Wakili huyo pia anataka Msajili wa Vyama vya Kisiasa azuiwe kumtambua au kumchapisha Sonko kwenye Gazeti Rasmi la Serikali kama kiongozi au afisa wa NEDP.
Mzozo huo unatokana na swali kuhusu iwapo kuondolewa kwa Sonko katika wadhifa wa ugavana kupitia mchakato wa kumng'oa madarakani kunamnyima kikatiba nafasi ya kuongoza chama cha kisiasa.
Bw Sanare anasema kuondolewa kwa Sonko kunamzuia kushikilia wadhifa wowote katika uongozi wa chama chini ya Sura ya Sita ya Katiba na Sheria ya Vyama vya Kisiasa.
Anategemea Kifungu cha 75(3) cha Katiba, kinachoweka masharti kuhusu mtu aliyeondolewa madarakani kwa kukiuka maadili ya uongozi kushikilia wadhifa mwingine wa serikali.
Pia anataka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) izuiwe kupokea vyeti vya uteuzi, orodha za wagombeaji au stakabadhi nyingine zitakazotiwa saini na Sonko akiwa kiongozi wa NEDP.
Katika kesi hiyo, anadai Sonko alianzisha chama hicho kilichosajiliwa Desemba 9, 2025, na ameendelea kutekeleza majukumu ya uongozi, yakiwemo kuwasilisha wagombeaji katika chaguzi ndogo.
Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imeomba mahakama iondoe jina lake kwenye kesi hiyo, ikisema hakuna ushahidi wa kuonyesha ilikiuka wajibu wake.
Msajili wa Vyama vya Kisiasa pia anapinga ombi la Bw Sanare.
Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi Februari 3, 2027, ambapo itatoa maelekezo kuhusu kuwasilishwa kwa hoja za mwisho na kupanga tarehe ya uamuzi.




