Kitandula ahimiza ukamilishaji miundombinu Mikumi

Habari Leo
Published: Jan 11, 2025 09:40:31 EAT   |  Travel

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula amehimiza kukamilishwa kwa miradi mbalimbali ya miundombinu chini ya Mradi…

The post Kitandula ahimiza ukamilishaji miundombinu Mikumi appeared first on HabariLeo.

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula amehimiza kukamilishwa kwa miradi mbalimbali ya miundombinu chini ya Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Kitandula amesema  hayo alipofanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini ya Mradi wa REGROW kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Naibu Waziri alikagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya miundombinu, ikiwemo ujenzi wa Kiwanja cha Kisasa cha Ndege, majengo ya kupokelea wageni, mageti mawili ya kisasa, na nyumba za kisasa za kupumzikia wageni.

Hivyo aliwataka wasimamizi wa mradi huo kutunza miundombinu ya kisasa inayojengwa, kwani kukamilika kwa miradi hiyo kutakuwa na manufaa makubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Amesema miradi hiyo itachochea ukuaji wa sekta ya utalii, kuboresha huduma kwa wageni, na kuongeza idadi ya watalii katika hifadhi ya Taifa Mikumi ambalo pia litakaloongeza mapato ya utalii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo ya jirani.

“Miundombinu hii ya kisasa ni muhimu katika kufungua fursa za kiuchumi na kijamii, hususan kwa jamii zinazozunguka Hifadhi ya Taifa Mikumi,” amesema Naibu Waziri .

“Tunahitaji kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na fursa zinazotokana na mradi huu,” amesisitiza  Kitandula.

Naibu Waziri Kitandula amesisitiza umuhimu wa miradi hiyo katika kuimarisha sekta ya utalii, na aliwataka wasimamizi kuunga mkono jitihada za  Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuisimamia vyema na kuitunza miundombinu hiyo.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Kanda ya Mashariki ,John Nyamhanga,amesema  mradi wa REGROW umeweza kubadilisha  muonekano wa Hifadhi ya Taifa Mikumi.

Nyamhanga ameeleza kuwa namna ambavyo uboreshaji wa miundombinu hiyo unavyofanyika utaongeza mazao ya utalii, na hivyo kuhamasisha ongezeko la idadi ya watalii na kukuza pato la Taifa.

“Mradi wa REGROW katika hifadhi ya Taifa Mikumi ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Tanzania katika kutunza na kuendeleza rasilimali za asili za nchi kwa ajili ya manufaa ya wananchi na ustawi wa taifa” amesema Nyamhanga.

Mradi wa REGROW, unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania, unalenga kuboresha miundombinu ya utalii, kuimarisha usimamizi wa maliasili, na kuvutia uwekezaji katika sekta ya utalii.

Kupitia mradi huo, maeneo muhimu ya Hifadhi ya Mikumi yameboreshwa, yakiwemo miundombinu ya barabara, vituo vya taarifa, na huduma bora za wageni.

The post Kitandula ahimiza ukamilishaji miundombinu Mikumi appeared first on HabariLeo.