MBEYA; Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju, amewataka viongozi wa dini nchini kuendelea kuhimiza maadili mema katika jamii, akieleza kuwa wamekuwa na mchango mkubwa katika kujenga tabia njema, kubadilisha mienendo ya watu na kuimarisha mshikamano wa taifa.
Amesema viongozi wa dini wana nafasi muhimu katika kudumisha amani, haki na usalama wa taifa kupitia maombi, mafundisho na malezi ya kiroho wanayoyatoa kwa jamii, kwa kuwa ni wawakilishi wa Mwenyezi Mungu wanaosaidia watu kuwa na mahusiano mema na Mungu pamoja na wenzao.
Jaji Masaju amesema hayo leo jijini Mbeya wakati akizungumza na viongozi wa dini pamoja na maelfu ya waumini mbalimbali wa mkoa huo waliohudhuria kongamano la kuliombea taifa.
“Hata viongozi wanapoapishwa kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi,humtaja Mungu katika viapo vyao,kwa hiyo Serikali pia inatambua uwepo wa Mungu na ndio maana hata katiba yetu inatambua uwepo wa madhahebu ya dini,” amesema Jaji Masaju.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Jumanne Sagini, amesema Serikali inaendelea kushirikiana na viongozi wa dini katika kuimarisha amani na maendeleo ya jamii.
Amesema mkoa huo unatarajia kuandaa kongamano kubwa la kimataifa la biashara na uwekezaji mwakani, kwa lengo la kutangaza fursa zilizopo mkoani humo na kukuza maendeleo ya kiuchumi.
Ameeleza kuwa maandalizi ya kuboresha na kupanga jiji yanaendelea ili kuweka mazingira mazuri yatakayowezesha kufanyika kwa kongamano hilo na kuvutia washiriki kutoka ndani na nje ya nchi.




