DAR ES SALAAM: Wakati akiwa kazini amevaa sare ya Jeshi la Polisi akitekeleza majukumu ya kulinda jamii, nje ya kazi Inspekta Salim Hussein Ng’anzi anatumia kalamu kuelimisha jamii, safari iliyomfikisha katika ushindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi Afrika.
Ng’anzi, ambaye ni mkufunzi wa Shule ya Polisi Tanzania iliyopo Moshi, Kilimanjaro, ametwaa nafasi ya kwanza katika kipengele cha Riwaya kupitia muswada wake wa Mwanamkasi Ndio Basi, katika tuzo zilizotangazwa hivi karibuni, jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo ni sehemu ya safari yake ya muda mrefu katika uandishi wa fasihi, ambayo alianza kuijenga baada ya kuhitimu kidato cha sita mwaka 2010, akivutiwa na kazi za waandishi mbalimbali wakiwamo Shaaban Robert, Shafi Adam Shafi, Ben Rashidi Mtobwa na Hussein Issa Tuwa.
Akielezea safari yake, Ng’anzi anasema kipaji cha uandishi kilianza kujitokeza akiwa mwanafunzi wa kidato cha sita jijini Mbeya, ambako alianza kuvutiwa na kazi za waandishi mbalimbali na hatimaye kuamua kushika kalamu.
Tangu wakati huo, ameendelea kujenga jina lake katika uandishi wa riwaya na mashairi, akiwa tayari ameandika na kuchapisha vitabu vitano, vikiwamo Mbio za Sakafuni (2019), Mafasa (2021), Wahitimu Vivuli (2022), Ghubari la Kiza (2023) na Mafasa Toleo Jipya (2025).
Hata hivyo, safari yake ya ushindi wa Safal imepitia muswada wa riwaya Mwanamkasi Ndio Basi, ambao uliingia katika kinyang’anyiro kilichohusisha zaidi ya miswada 200 iliyowasilishwa na waandishi mbalimbali.
Katika riwaya hiyo, Ng’anzi anaangazia maisha ya Mwanamkasi, msichana aliyekulia katika maadili mema na kufanikiwa kujiunga na chuo kikuu, lakini baadaye anajikuta akiingia katika ushawishi wa makundi rika na kufanya maamuzi yanayobadilisha maisha yake.
Mwanamkasi anajikuta akiacha masomo, kuingia katika maisha ya anasa na hatimaye kutumiwa bila kujua katika biashara ya dawa za kulevya, hali inayomfikisha gerezani akitumikia kifungo cha miaka 20.
Kupitia simulizi hiyo, mwandishi anatoa ujumbe kuwa makosa ya vijana yanayosababishwa na ushawishi na maamuzi yasiyo sahihi yanaweza kuharibu maisha yao, lakini mtu hapaswi kukata tamaa kuhusu uwezekano wa kubadilika na kujenga upya maisha yake.
Ujumbe huo una uhusiano na majukumu yake ya kila siku ndani ya Jeshi la Polisi, ambako anafundisha masomo ya haki za binadamu pamoja na namna ya kutambua na kukabiliana na itikadi kali na ugaidi.
Mbali na majukumu hayo, Ng’anzi pia ni mkufunzi wa kwata za uwanjani na msimamizi wa maktaba ya Shule ya Polisi Tanzania, majukumu ambayo hayajamzuia kuendelea kukuza kipaji chake cha uandishi.
Anasema hutumia muda wake wa ziada kuandika, huku akieleza kuwa kazi ya uandishi inahitaji uvumilivu na inaweza kuchukua miezi kadhaa kukamilisha kazi moja.
Mafanikio hayo yanamfungulia ukurasa mpya katika safari yake ya kifasihi, huku muswada uliompa ushindi ukitarajiwa kuchapishwa na kampuni ya Mkuki na Nyota Publishers ya Dar es Salaam ili kuwafikia wasomaji wengi zaidi.
Kwa Ng’anzi, ushindi huo si mafanikio ya mtu mmoja pekee, bali pia ni fursa ya kuonesha kuwa watumishi wa umma wanaweza kutumia vipaji vyao nje ya majukumu ya kawaida na kuchangia maendeleo ya jamii kupitia sanaa na fasihi.




