Chuo Kikuu cha Rongo kilipokuwa kikifanya mahafali yake ya 11 mjini Migori Ijumaa, aliyekuwa gavana wa kwanza wa kaunti hiyo, Okoth Obado, alikuwa akihukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani kwa mauaji ya mwanafunzi wa zamani wa chuo hicho, Sharon Otieno.
Baada ya kuhudumu kwa miaka tisa akiwa na mamlaka makubwa kisiasa, Obado sasa anaanza maisha ya gerezani pamoja na aliyekuwa msaidizi wake Michael Oyamo na aliyekuwa karani wa serikali ya kaunti ya Migori, Caspal Obiero.
Obado na Oyamo walihukumiwa kifungo cha miaka 25 kila mmoja, huku Obiero akipewa miaka 18 kwa kuhusika katika njama ya kumuua Sharon, aliyekuwa na umri wa miaka 26.
Hukumu hiyo ilifunga rasmi kesi iliyokuwa ikifuatiliwa kwa karibu nchini kwa miaka minane.Usiku wa Septemba 3, 2018, Sharon, ambaye alikuwa na watoto watatu na ujauzito wa miezi saba, alitekwa nyara pamoja na mwandishi wa habari wa Nation Media Group, Barack Odour.
Odour aliweza kutoroka kwa kuruka kutoka kwenye gari lililokuwa likienda kasi. Sharon hakubahatika. Baadaye mwili wake ulipatikana ukiwa na majeraha saba ya visu tumboni. Alifariki pamoja na mtoto aliyekuwa tumboni mwake.
Mauaji hayo yalizua hasira kubwa nchini huku wananchi wakitaka haki itendeke.
Katika uamuzi wake wa Julai 23, Jaji Cecilia Githua alisema kuwa ingawa hakukuwa na mtu aliyeshuhudia washtakiwa wakimuua Sharon, ushahidi uliowasilishwa mahakamani uliunganisha matukio yote na kuonyesha jinsi mauaji yalivyopangwa.
“Ushahidi uliowasilishwa ulipounganishwa uliunda msururu kamili kiasi kwamba hapakuwa na njia nyingine ya kufikia hitimisho isipokuwa kwamba washtakiwa, kwa pamoja na wengine ambao hawakuwa mahakamani, walitenda kosa hilo,” alisema jaji.
Kiini cha kesi ya upande wa mashtaka kilikuwa mzozo kuhusu ujauzito wa Sharon. Obado alitajwa kuwa baba wa mtoto huyo, lakini inadaiwa alitaka Sharon aiavye mimba huku yeye akisisitiza kuutunza ujauzito.
Mama yake Sharon, Melinda Auma, aliambia mahakama kuwa binti yake alimweleza kuhusu mabadiliko ya ghafla katika tabia ya Obado.
Alisema gavana huyo alianza kuepuka simu za Sharon, akasitisha msaada wa kifedha na kumpa Sh30,000 ili atoe mimba, lakini Sharon alikataa.
Ushahidi wa mawasiliano kati ya wawili hao pia uliwasilishwa. Katika baadhi ya jumbe, Sharon alikuwa akimuuliza Obado kuhusu nyumba ya vyumba vitatu aliyokuwa ameahidi kununua Kisumu.
Mahakama pia iliona picha za uchunguzi wa mtoto aliyekuwa tumboni mwa Sharon. Obado alipoonyeshwa picha hizo, alijibu, “Sawa sawa. Nakutakia kila la heri.”Mwanahabari Odour aliambia mahakama kuwa Sharon alikuwa amemchezea rekodi za mazungumzo yake na Obado kwa lugha ya mama. Katika mazungumzo hayo, gavana huyo alidaiwa kumshinikiza atoe mimba na kuahidi kumpa pesa.Odour pia alieleza jinsi alivyovutwa katika mtego wa kukutana na Sharon na Oyamo katika Hoteli ya Graca mjini Rongo. Baadaye waliambiwa waingie kwenye gari aina ya Toyota Fielder.
Gari lilipoanza kuondoka, Oyamo alishuka na wanaume wawili wakaingia nyuma, wakimzingira Sharon na Odour.
Watekaji waliwaamuru watoe simu zao.Odour alitoroka kwa kuruka kutoka kwenye gari hilo, lakini Sharon akabaki mikononi mwa watekaji.Ushahidi wa simu na mawasiliano ya WhatsApp uliwasaidia wachunguzi kuunganisha watatu hao.
Rekodi zilionyesha mawasiliano kati ya Obado, Oyamo na Obiero katika kipindi cha kabla na baada ya mauaji.Wachunguzi pia walifuatilia gari lililotumiwa katika utekaji nyara. Kampuni iliyokuwa imeweka kifaa cha kufuatilia gari hilo iliambia mahakama kuwa kifaa hicho kilizimwa siku ya tukio na kuwashwa tena siku iliyofuata.
Gari hilo lilikuwa likitumika kama teksi na lilimilikiwa na Olivia Oloo, mke wa Obiero.
Dereva wake, Jackson Otieno Gombe, alitoa ushahidi mahakamani.
Oyamo alijisalimisha katika Kituo cha Polisi cha Uriri siku iliyofuata, akidai kuwa alikuwa ametekwa na kuibiwa Sh270,000 za gavana.
Hata hivyo, Odour alikuwa tayari ameripoti kutekwa kwake katika vituo vya polisi.Polisi walipopokea taarifa kuhusu Oyamo, alikamatwa akiandika taarifa yake na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Homa Bay.
Baadaye mwili wa Sharon ulipatikana kichakani karibu na Mto Owade na Moses Onditi Oguta. Ugunduzi huo uliimarisha uchunguzi uliofanywa na kitengo cha mauaji cha DCI.
Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 42 na vielelezo 81. Ushahidi huo ulijumuisha rekodi za simu, jumbe, taarifa za mashahidi na maelezo kuhusu gari lililotumiwa katika utekaji nyara.
Obado alijitetea akisema alikuwa Nairobi wakati Sharon alipouawa. Hata hivyo, jaji alikataa maelezo hayo baada ya kuchunguza ushahidi uliounganisha washtakiwa na mpango huo.
Katika kesi hiyo, aliyekuwa MCA wa Kanyadoto, Lawrence Obonyo Owour almaarufu Mulla, pia alitoa ushahidi. Alifariki Mei 2024 baada ya kuanguka mjini Homa Bay na kufikishwa hospitalini akiwa tayari amefariki.
Familia yake ilisema alikuwa ameonekana mzima kabla ya kifo chake cha ghafla, na polisi wakaanzisha uchunguzi kuhusu kilichosababisha kifo chake.
Huu ndio ushahidi uliomfanya Obado kusukumwa jela miaka 25
Taifa Leo 4 min read

This story was originally published by Taifa Leo.
Read the full story at Taifa LeoRelated stories
NewsUduere Killings in Delta: Six trucks of policemen, yet bullets still found targets
“Policemen told me APC supporters were not shooting guns, but knockouts (fireworks). I said but you can see them brandishing pump actions openly"
Vanguard News 1 min read
NewsHow Tinubu fought Obasanjo to reclaim Lagos coastline – Fashola
“Funsho Williams was a man of peace, a fine gentleman, an outstanding public servant. No one deserved to be treated the way he was cruelly murdered"
Vanguard News 1 min read
NewsTAARIFA YA HABARI YA ASUBUHI: NOV 28, 2026
Usisahau kutufuatilia katika mitandao yetu ; Subscribe to our Youtube Channel : http://bit.ly/itvtanzania
ITV Tanzania Video
News2027 Presidential poll: What will influence our vote — Nigerians
“My decision on who to vote for in the 2027 presidential election will be guided by how convinced I am about how the various candidates address sustainable development concerns"
Vanguard News 1 min read