FAMILIA za wanaume wawili waliotekwa nyara katika visa tofauti Mombasa na Lamu zimeendelea kukosa majibu kuhusu waliko wapendwa wao baada ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kusema haijawazuilia.


Hata hivyo, Mahakama Kuu ya Mombasa imeagiza maafisa wa usalama kukamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti kamili ndani ya siku tatu kuhusu kutoweka kwa Ismail Yusuf Mohamed na Ali Kassim.


Mohamed alitekwa eneo la Bondeni karibu na Camels Joint usiku wa Oktoba 30 mwaka huu akitafuta chakula.


Kwa mujibu wa DCI, kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Central mnamo Oktoba 31 na Fatuma Saidi.


Polisi walisema uchunguzi ulianza katika kituo hicho kabla ya kuhamishiwa kwa DCI Urban Police Station, huku taarifa za kutafuta Mohamed zikitumwa katika vituo vya polisi kote nchini.


Hata hivyo, DCI ilisema baadhi ya mashahidi wanaohusishwa na tukio hilo hawajapatikana na uchunguzi wa kamera za CCTV bado unaendelea.


Shirika la Vocal Africa, ambalo limewasilisha kesi kwa niaba ya Mohamed, linadai kuwa kamera zilirekodi watu waliokuwa wakimfuatilia kwa gari aina ya pickup kabla ya kumteka na kumuingiza katika Toyota Land Cruiser nyeupe.


Shirika hilo linataka Inspekta Jenerali wa Polisi amfikishe Mohamed mahakamani akiwa hai au amekufa na kueleza aliko.


Mohamed aliwahi kushtakiwa kwa kosa la kuajiri watu kwa ajili ya kundi la kigaidi, lakini aliachiliwa huru na mahakama ya Malindi Agosti 11, 2023 baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kesi.


Katika kisa cha pili, Kassim alitekwa nyumbani kwake katika kijiji cha Tchundwa, Lamu Mashariki, usiku wa Septemba 26, 2026.


DCI ilisema takriban watu 10 waliovalia mavazi ya kijeshi na kufunika nyuso zao waliingia nyumbani kwake saa 4.40 usiku na kumchukua.


Mkewe, Sauda Mumin, aliripoti tukio hilo katika kituo cha polisi cha Tchundwa siku iliyofuata.


Vocal Africa inadai waliomchukua Kassim walijitambulisha kuwa maafisa wa polisi na kumwahidi mkewe kwamba wangemwachilia baada ya kumhoji.


Familia zote mbili zinataka maafisa wa usalama kueleza waliko wanaume hao na sababu za kutoweka kwao.


Kesi hizo zinatarajiwa kusikilizwa Novemba 23.