TUME ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC) imewaonya magavana, madiwani na maafisa wakuu wa serikali za kaunti dhidi ya kuingilia shughuli za kuajiri na kuwapandisha vyeo wafanyakazi.

EACC inasema tabia hiyo inawanyima Wakenya waliohitimu nafasi za ajira wanazostahili.

Tume hiyo inadai kuwa kuna ongezeko la visa vya wanasiasa kuingilia uhuru wa kikatiba wa Bodi za Utumishi wa Umma za Kaunti, huku baadhi yao wakidaiwa kushinikiza kuajiriwa, kuteuliwa na kupandishwa vyeo kwa watu wanaowapendelea.

Kwa mujibu wa EACC, baadhi ya madiwani wanadaiwa kutaka nafasi fulani za kazi zinazotangazwa zihifadhiwe kwa jamaa zao, marafiki na wafuasi wao wa kisiasa.

Wanapewa hisani hizo ili wapunguze shinikizo kwa serikali za kaunti na kulegeza majukumu yao ya kutathmini utendakazi wa magatuzi yao.

Afisa Mkuu wa EACC, Abdi Mohamud alisema uchunguzi wa tume hiyo umebaini kuwa baadhi ya wafanyakazi hupandishwa vyeo kutokana na uhusiano binafsi, mapendeleo ya kisiasa au kutoa hongo badala ya uwezo na utendakazi wao.

“Kuna visa ambapo nafasi za kazi hazitangazwi kupitia ushindani wa haki, au taratibu za kuajiri hupangwa kimakusudi ili kuwafaa jamaa, marafiki, wafuasi wa kisiasa na washirika wa watu wenye ushawishi,” akasema Bw Mohamud.

Katika hotuba yake iliyosomwa na Meneja wa EACC katika eneo la Magharibi Eric Ngumbi wakati wa uzinduzi rasmi wa ukaguzi wa mifumo ya usimamizi wa rasilimali katika serikali ya Kaunti ya Kakamega, tume hiyo ilisema tabia hiyo haikomei kwa magavana na madiwani pekee.

Baadhi ya wabunge wa Bunge la Kitaifa pia wanadaiwa kuingilia uajiri wa wafanyakazi katika kaunti zao.

EACC sasa inazitaka Bodi za Utumishi wa Umma za Kaunti kulinda uhuru wao na kukataa shinikizo za kisiasa, ikisisitiza kuwa ajira za umma zinapaswa kutegemea sifa, elimu, uwezo na ushindani wa haki ulio wazi.

“Kinachotia wasiwasi zaidi ni baadhi ya Bodi za Utumishi wa Umma za Kaunti kusalimu amri na kuachana na uhuru waliopewa na Katiba, na kuanza kufanya kazi kana kwamba ni idara zilizo chini ya afisi za magavana. Hali hii inadhoofisha uhuru wao na kufungua mlango wa kuingiliwa kwa maamuzi ya kuajiri na kusimamia wafanyakazi,” akasema Bw Mohamud.

Alionya kuwa ufisadi katika utoaji ajira una madhara makubwa kuliko kuongeza gharama za mishahara ya wafanyakazi wa umma.

Alisema kila nafasi inayotwaliwa isivyo halali inamnyima Mkenya aliyehitimu fursa ya kupata ajira.

“Kila mfanyakazi hewa kwenye orodha ya mishahara anawakilisha fedha za umma ambazo zingetumika kuboresha huduma za afya, elimu, miundombinu na huduma nyingine muhimu.

“Vilevile, kila cheo kinachopatikana kupitia hongo, upendeleo wa kifamilia au ushawishi wa kisiasa hudhoofisha mfumo wa kutambua uwezo, hushusha ari ya wafanyakazi na kudhoofisha utendakazi wa taasisi,” akaongeza.

EACC pia imeangazia visa vya wafanyakazi wa muda kuingizwa katika ajira za kudumu na zenye pensheni bila kupitia ushindani wa haki.

Tabia hiyo inadaiwa kushamiri hasa wakati wa mabadiliko ya uongozi katika kaunti.

Hatari nyingine zilizotambuliwa ni pamoja na kuchezea orodha za mishahara, kuwa na wafanyakazi hewa, kuendelea kuwalipa watu ambao tayari wameacha kazi na kutumia vibaya makato ya kisheria au kushindwa kuyawasilisha kwa taasisi husika.

Akizungumza katika hafla hiyo, Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa alizitaka Bodi za Utumishi wa Umma, maafisa katika idara ya utoaji ajira na wafanyakazi wengine wa serikali kuzingatia sheria na kuwajibikia maamuzi yao.

Alisema usimamizi wa wafanyakazi ni muhimu katika kujenga uadilifu, uwazi na imani ya wananchi kwa taasisi za umma.

“Kwa kuwa usimamizi wa rasilimali unaunganisha sera zinazohusu wafanyakazi na uhalali wa taasisi, uadilifu na utendakazi, ni sehemu muhimu ya mfumo wa utawala. Kila kitu mnachofanya kama maafisa kinapaswa kuonyesha dhamira ya kuimarisha uwazi na kujenga imani ya wananchi,” alisema Bw Barasa.

Gavana huyo pia alizitaka kaunti nyingine kuunga mkono mipango ya EACC na kushirikiana na tume hiyo kuzuia ufisadi badala ya kuikwepa na kuanza kulalamika zinapoitwa kuelezea matumizi mabaya ya fedha za umma.

Ukaguzi huo wa wiki tatu unaofanywa na EACC Kakamega unalenga kuchunguza mifumo ya usimamizi wa wafanyakazi, kubaini mianya ya ufisadi na kupendekeza mageuzi yatakayoongeza uwazi, uwajibikaji na uadilifu katika utumishi wa umma wa kaunti hiyo.