TAKRIBAN thuluthi moja ya wanafunzi wanaojiunga na Sekondari Pevu kutoka Sekondari Msingi hawana ujuzi muhimu wa kusoma, kuandika na kuhesabu, ripoti mpya imefichua.
Ripoti hiyo iliyotolewa na Usawa Agenda, shirika linalofanya utafiti kuhusu elimu ya msingi, pia imeonyesha kuwa wanafunzi katika shule za umma za maeneo ya mashambani ndio walioathirika zaidi.
Utafiti huo uliofanywa katika kaunti zote 47 ulihusisha familia 41,156, shule 1,527 na wanafunzi 49,835. Pia ulihusisha jamii za wakimbizi katika kambi za Dadaab, Kakuma na Kalobeyei.
Ripoti hiyo inasema asilimia 29 ya wanafunzi wa Gredi 9 hawana ujuzi wa msingi wa kusoma na kuhesabu.
Mwanafunzi mmoja kati ya watano wa Gredi 9 hawezi kusoma hadithi ya Kiingereza ya kiwango cha Gredi 3.
Hali hiyo pia inawakumba wanafunzi watatu kati ya 10 wa Gredi 7.
Hata hivyo, pengo hilo huanza mapema zaidi. Asilimia 41 ya wanafunzi wa Gredi 7 hawana ujuzi wa msingi wa kusoma na kuhesabu.
Ripoti hiyo ilisema shule za umma hufanya vibaya kuliko shule za kibinafsi katika kusoma na kuhesabu.
“Ushahidi unaonyesha kuwa sera za serikali zimefanikiwa kuwadumisha wanafunzi madarasani, lakini bado hazijafanikiwa kuhakikisha wanajifunza au shule wanazojiunga nazo zina vifaa sawa vya kusoma,” ripoti hiyo ilisema.
Ripoti hiyo ilibaini pia upungufu mkubwa wa vifaa shuleni.
Ni asilimia 27.5 pekee ya shule za Sekondari Msingi zilizo na maabara za sayansi zinazofanya kazi, huku asilimia 27 zikiwa na maktaba.
Ni asilimia 34.3 pekee zilizo na vifaa vya kutosha vya kusoma na asilimia 46.3 zilikuwa na kompyuta za wanafunzi.
Tofauti za kikanda ni kubwa. Nairobi ina maabara zinazofanya kazi katika asilimia 98.7 ya shule za Sekondari Msingi, ikilinganishwa na asilimia 15.4 Kaskazini Mashariki na asilimia 13.8 Magharibi.
Mkurugenzi wa Idara ya Sekondari Msingi katika Wizara ya Elimu Hellen Avisa, alisema changamoto ya ujuzi wa msingi inapaswa kushughulikiwa mapema.
Alisema ushahidi uliowasilishwa unapaswa kuchochea hatua katika ngazi ya kitaifa, kaunti na shule.
Ripoti hiyo inapendekeza wanafunzi wa Gredi 7 hadi 9 wapewe masomo maalum ya kurekebisha mapengo ya kusoma na kuhesabu.
Pia inataka serikali kuongeza uwekezaji katika maabara, maktaba, vifaa vya kusoma na kuhakikisha fedha za shule zinatolewa kwa wakati.
Ripoti hiyo ilisema ni asilimia 52.3 pekee ya shule za Sekondari Msingi zinazopokea fedha kwa wakati.
Wanafunzi wengi wa Gredi 9 hawawezi kusoma ipasavyo -Ripoti

This story was originally published by Taifa Leo.
Read the full story at Taifa LeoRelated stories
EducationalChama cha CHAWAKAMA-KENYA kinavyopeleka Kiswahili jukwaa la kimataifa
CHAMA cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA-KENYA) kimezidisha juhudi za kukiendeleza Kiswahili na kukipa nafasi katika ulimwengu wa utandawazi kupitia makongamano yanayowaleta pamoja wanazuo, watafiti na wadau wa lugha hii adhimu. Mbali na kukuza Kiswahili, chama hiki kimekuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wanafunzi wa vyuo vikuu, kuibua vipaji, kujenga mitandao ya kitaaluma na kuhamasisha ubunifu. Pia, kimechangia kuzalisha viongozi, waandishi, wahariri, watafiti na wakalimani watakaokipeperusha Kiswahili katika majukwaa ya kimataifa. Mwelekeo huo ulidhihirika Novemba 6–7 mwaka huu, wakati CHAWAKAMA-Kenya kilipoandaa kongamano la kikanda katika Chuo Kikuu cha Laikipia, lililoongozwa na kaulimbiu ya ‘Kiswahili na Utandawazi’. Kongamano hilo liliwakutanisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali, vikiwemo Rongo, Laikipia, Masinde Muliro, Kisii, Daystar, Kabianga, Murang’a, Turkana na Kaimosi. Washiriki walijadili nafasi ya Kiswahili katika kuzalisha maarifa, kuwasilisha uvumbuzi na kutatua changamoto za jamii. Kongamano lilifunguliwa rasmi na Prof Guyo Sarr Huka, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Laikipia anayesimamia masuala ya kitaaluma. Katika tukio hilo, kamati andalizi ikiongozwa na Mwenyekiti Clinton Ageta na mlezi wa chama Prof Sheila Wandera, ilizindua bidhaa zenye nembo ya CHAWAKAMA-Kenya, zikiwemo mashati-tao, chepeo, kalamu, bango na vitabu vilivyoandikwa na wanachama. Ubunifu wa wanachama ulijitokeza pia kupitia Kishazi TV, runinga ya mtandaoni iliyorusha matukio ya kongamano mubashara na kusambaza maudhui yake kupitia mitandao ya kijamii. Kongamano lilipambwa na michango ya wataalamu mashuhuri wa Kiswahili, akiwemo Dkt Moses Wasike (Mgeni Rasmi), Dkt Riro Matinde, Prof James Ontieri, Dkt Nixon Sangili na Dkt Sussy Nandama, miongoni mwa wengine. Mafanikio hayo yalitokana na ushirikiano wa CHAWAKAMA-Kenya, Idara ya Masomo ya Kibinadamu na Maendeleo, uongozi wa Chuo Kikuu cha Laikipia na Chama cha Kiswahili cha Laikipia (CHAKILA). Chama hicho kinaongozwa na Clinton Ageta (Mwenyekiti), Granton Mdogo (Naibu Mwenyekiti), Doreen Mukami (Katibu Mkuu), Griffin Amakala (Naibu Katibu Mkuu), Diana Mirriam (Mhazini), Velma Natang’a (Afisa wa Uhusiano Mwema), Micah Sikolia (Katibu Mtendaji) na Okimba Lester (Afisa Mwenezi). Wahariri ni Luke Shikoli, Kweyu Remjo, Augustine Wekesa, Winjoy Gacheri na Zdame Zuhura, huku Samson Nyamosi na Denis Chumo wakihudumu kama Maafisa wa Nidhamu. Kwa hakika, CHAWAKAMA-Kenya kinaendelea kuthibitisha kuwa mustakabali wa Kiswahili unategemea ubunifu, ushirikiano na juhudi za kizazi kipya.
Educational‘Shule zisizo na vifaa zisipokee wanafunzi wa amali’
MOROGORO: WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amewaagiza maofisa uthibiti ubora wa shule kufuatilia shule zote zinazotoa elimu ya amali na kuhakikisha zina miundombinu, vifaa na vitendea kazi vinavyokidhi mahitaji ya mafunzo ya ufundi. Amesema shule zilizosajiliwa kutoa elimu ya amali lakini hazina vifaa vya kufundishia na kujifunzia hazipaswi kuendelea kupokea wanafunzi…
EducationalWazazi wapinga mfumo wa uchaguzi wa shule za sekondari
WAZAZI wawili wamewasilisha kesi mahakamani kutaka Wizara ya Elimu izuiwe kukamilisha uteuzi wa wanafunzi wa Gredi 10 katika shule za sekondari, wakidai mfumo wa kusimamia habari za elimu Kenya ( KEMIS) una hitilafu zinazowanyima wanafunzi nafasi ya kuchagua shule wanazotaka. Mabw Omwenga Ongegu na John Ominde wanasema mfumo huo unaonyesha shule 1,000 pekee kwa kila mseto wa masomo, hata pale ambapo shule nyingi zaidi zinatoa mseto huo nchini. Pia wanadai kuwa baadhi ya miseto ya masomo haina shule zilizoorodheshwa. Katika ombi lao, Ongegu alisema miseto 26 ya masomo imeathiriwa na idadi ya shule hizo 1,000, hali inayoficha taasisi nyingine zinazotoa masomo hayo. Kwa mfano, mseto wa ST1048 unaojumuisha Baiolojia, Kemia na Fizikia katika mkondo wa Sayansi, Tekonolojia na Hisbati (STEM) una shule 10,515 zinazodaiwa kuutoa nchini, lakini mfumo unaonyesha shule 1,000 pekee. Hii ina maana kuwa wanafunzi wanaona takriban asilimia 9.51 pekee ya shule zinazopatikana kwa mseto huo. Walalamishi pia wanasema kuwa kati ya mIseto 418 iliyoorodheshwa kwenye mfumo, 28 haina shule yoyote iliyoonyeshwa, huku 303 ikiwa na shule 94 au chini ya hapo. Wanasema kasoro hizo zinazuia wanafunzi na wazazi kupata taarifa sahihi kabla ya kufanya maamuzi yatakayoathiri masomo yao ya baadaye. “Hii haiwezi kuachwa bila kurekebishwa hadi wanafunzi watakapofika wakati wa kuomba nafasi za shahada na diploma kupitia KUCCPS,” sehemu ya kesi inasema. Pia walalamishi wameibua wasiwasi kuhusu jinsi masomo ya Gredi 10 yatakavyoathiri nafasi za kujiunga na vyuo vikuu. Wanasema hakuna ufafanuzi wa kutosha kuhusu jinsi somo la Community Service Learning litakavyoathiri wanafunzi kujiunga na kozi mbalimbali. Wanataka mahakama itangaze kuwa kuonyesha orodha zisizokamilika bila kutoa tahadhari kunakiuka haki za wanafunzi. Pia wanataka wizara iamriwe kufungua tena mfumo huo ili wanafunzi warekebishe uchaguzi wao baada ya kupewa taarifa kamili kuhusu shule na mseto wa masomo. Wamependekeza mfumo ufunguliwe tena baada ya mitihani ya tathmini ya Gredi 9 kuanza Oktoba 26, ili kuepusha kuwaongezea watahiniwa shinikizo. Mfumo wa KEMIS ulifunguliwa Agosti 24, 2026, na muda wa kuchagua shule uliongezwa hadi Septemba 15.
EducationalKiruswa akabidhi vifaa shule ya Lesing’ita
LONGIDO: NAIBU Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Longido mkoani Arusha, Dk. Stephen Kiruswa, amekabidhi mashine ya kunakili na kuchapisha nyaraka pamoja na kompyuta kwa Shule ya Msingi Lesing’ita, vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni tatu, ili kupunguza gharama za shule katika uchapishaji wa karatasi za mazoezi, mitihani na shughuli nyingine za…