MGONJWA anapoingia hospitalini hupokea matibabu akiamini dawa alizopewa ni salama na zenye ubora unaostahili. Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kuwa baadhi ya dawa zenye kasoro huingia katika mfumo wa afya na kuwafikia wagonjwa kabla ya dosari zake kugunduliwa.
Mwaka huu pekee, Bodi ya Dawa na Sumu Kenya (PPB) imetoa maagizo 16 ya kuondoa sokoni dawa na bidhaa za matibabu zinazoshukiwa kuwa na matatizo ya ubora. Dawa hizo zimehusisha za kugadisha, vifaa vya pumu, dawa za tumbo na bidhaa nyingine muhimu zinazotumiwa hospitalini kila siku.
Mkurugenzi Mkuu wa PPB, Dkt Ahmed Mohamed, amesema ongezeko la visa vya kuondolewa kwa dawa sokoni linaonyesha kuwa mifumo ya ufuatiliaji imeimarika na sasa inafanikiwa kugundua matatizo ambayo hapo awali yangeweza kupita bila kugunduliwa.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, changamoto inaanzia katika hatua mbalimbali za mfumo wa ugavi wa dawa. Baadhi ya dosari hutokana na utengenezaji katika viwanda vya nje ya nchi, huku nyingine zikisababishwa na hali mbaya ya uhifadhi au usafirishaji wa dawa kabla hazijamfikia mgonjwa.
Dawa nyingi zilizoondolewa sokoni mwaka huu zilitengenezwa katika nchi za kigeni, hasa India. Kampuni kadhaa zilihusishwa na matatizo kama kubadilika kwa rangi ya dawa, kushindwa kufikia viwango vya kemikali vinavyohitajika au kuwepo kwa hitilafu zinazoweza kuhatarisha afya ya watumiaji.
Mfamasia wa viwandani katika Hospitali ya Mafunzo, Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTTRH), Dkt Lonary Ngetich, anasema dawa zinazotengenezwa Kenya mara nyingi huondolewa sokoni kutokana na hitilafu zinazoonekana kwa macho kama uchafu. Kinyume chake, dawa nyingi za nje huonyesha matatizo ya kemikali yanayoweza kugunduliwa tu kupitia maabara.
Anasema hata dawa inayotoka kiwandani ikiwa katika hali nzuri inaweza kuharibika kutokana na joto kali, unyevunyevu au uhifadhi usiofaa wakati wa usafirishaji na usambazaji.
Madhara ya dawa hizo kwa wagonjwa yanaweza kuwa makubwa. Dawa zisizo na kiwango sahihi cha kemikali zinaweza kusababisha ugonjwa kuendelea kuenea, viungo vya mwili kutofanya kazi au hata kifo. Aidha, matumizi ya dawa hafifu yanaweza kuongeza tatizo la dawa, ambapo bakteria na vimelea hujenga uwezo dhidi ya dawa.
Ingawa PPB ina mifumo ya kupokea ripoti kutoka kwa wahudumu wa afya na wananchi, wataalamu wanaonya kuwa mara nyingi dosari hugunduliwa baada ya wagonjwa tayari kutumia dawa hizo.
Ili kudhibiti hali hiyo, serikali inatekeleza Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Dawa Hafifu na Bandia. Mpango huo unalenga kuimarisha usimamizi wa mfumo wa ugavi, kuboresha ufuatiliaji wa soko na kuhakikisha ni dawa salama pekee zinawafikia Wakenya.
Kulingana na takwimu za PPB, visa vya dawa zenye kasoro vilivyoripotiwa viliongezeka kutoka 42 mwaka 2021 hadi 85 mwaka 2023 kabla ya kupungua katika miaka iliyofuata. Aidha, bidhaa bandia zilianza kugunduliwa mwaka 2023. Hata hivyo, kiwango halisi cha wagonjwa walioathiriwa na dawa hizo bado hakijabainishwa rasmi.
Wagonjwa hatarini: Jinsi dawa zenye dosari hupenya Kenya

This story was originally published by Taifa Leo.
Read the full story at Taifa LeoRelated stories
EducationalChama cha CHAWAKAMA-KENYA kinavyopeleka Kiswahili jukwaa la kimataifa
CHAMA cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA-KENYA) kimezidisha juhudi za kukiendeleza Kiswahili na kukipa nafasi katika ulimwengu wa utandawazi kupitia makongamano yanayowaleta pamoja wanazuo, watafiti na wadau wa lugha hii adhimu. Mbali na kukuza Kiswahili, chama hiki kimekuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wanafunzi wa vyuo vikuu, kuibua vipaji, kujenga mitandao ya kitaaluma na kuhamasisha ubunifu. Pia, kimechangia kuzalisha viongozi, waandishi, wahariri, watafiti na wakalimani watakaokipeperusha Kiswahili katika majukwaa ya kimataifa. Mwelekeo huo ulidhihirika Novemba 6–7 mwaka huu, wakati CHAWAKAMA-Kenya kilipoandaa kongamano la kikanda katika Chuo Kikuu cha Laikipia, lililoongozwa na kaulimbiu ya ‘Kiswahili na Utandawazi’. Kongamano hilo liliwakutanisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali, vikiwemo Rongo, Laikipia, Masinde Muliro, Kisii, Daystar, Kabianga, Murang’a, Turkana na Kaimosi. Washiriki walijadili nafasi ya Kiswahili katika kuzalisha maarifa, kuwasilisha uvumbuzi na kutatua changamoto za jamii. Kongamano lilifunguliwa rasmi na Prof Guyo Sarr Huka, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Laikipia anayesimamia masuala ya kitaaluma. Katika tukio hilo, kamati andalizi ikiongozwa na Mwenyekiti Clinton Ageta na mlezi wa chama Prof Sheila Wandera, ilizindua bidhaa zenye nembo ya CHAWAKAMA-Kenya, zikiwemo mashati-tao, chepeo, kalamu, bango na vitabu vilivyoandikwa na wanachama. Ubunifu wa wanachama ulijitokeza pia kupitia Kishazi TV, runinga ya mtandaoni iliyorusha matukio ya kongamano mubashara na kusambaza maudhui yake kupitia mitandao ya kijamii. Kongamano lilipambwa na michango ya wataalamu mashuhuri wa Kiswahili, akiwemo Dkt Moses Wasike (Mgeni Rasmi), Dkt Riro Matinde, Prof James Ontieri, Dkt Nixon Sangili na Dkt Sussy Nandama, miongoni mwa wengine. Mafanikio hayo yalitokana na ushirikiano wa CHAWAKAMA-Kenya, Idara ya Masomo ya Kibinadamu na Maendeleo, uongozi wa Chuo Kikuu cha Laikipia na Chama cha Kiswahili cha Laikipia (CHAKILA). Chama hicho kinaongozwa na Clinton Ageta (Mwenyekiti), Granton Mdogo (Naibu Mwenyekiti), Doreen Mukami (Katibu Mkuu), Griffin Amakala (Naibu Katibu Mkuu), Diana Mirriam (Mhazini), Velma Natang’a (Afisa wa Uhusiano Mwema), Micah Sikolia (Katibu Mtendaji) na Okimba Lester (Afisa Mwenezi). Wahariri ni Luke Shikoli, Kweyu Remjo, Augustine Wekesa, Winjoy Gacheri na Zdame Zuhura, huku Samson Nyamosi na Denis Chumo wakihudumu kama Maafisa wa Nidhamu. Kwa hakika, CHAWAKAMA-Kenya kinaendelea kuthibitisha kuwa mustakabali wa Kiswahili unategemea ubunifu, ushirikiano na juhudi za kizazi kipya.
Educational‘Shule zisizo na vifaa zisipokee wanafunzi wa amali’
MOROGORO: WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amewaagiza maofisa uthibiti ubora wa shule kufuatilia shule zote zinazotoa elimu ya amali na kuhakikisha zina miundombinu, vifaa na vitendea kazi vinavyokidhi mahitaji ya mafunzo ya ufundi. Amesema shule zilizosajiliwa kutoa elimu ya amali lakini hazina vifaa vya kufundishia na kujifunzia hazipaswi kuendelea kupokea wanafunzi…
EducationalWazazi wapinga mfumo wa uchaguzi wa shule za sekondari
WAZAZI wawili wamewasilisha kesi mahakamani kutaka Wizara ya Elimu izuiwe kukamilisha uteuzi wa wanafunzi wa Gredi 10 katika shule za sekondari, wakidai mfumo wa kusimamia habari za elimu Kenya ( KEMIS) una hitilafu zinazowanyima wanafunzi nafasi ya kuchagua shule wanazotaka. Mabw Omwenga Ongegu na John Ominde wanasema mfumo huo unaonyesha shule 1,000 pekee kwa kila mseto wa masomo, hata pale ambapo shule nyingi zaidi zinatoa mseto huo nchini. Pia wanadai kuwa baadhi ya miseto ya masomo haina shule zilizoorodheshwa. Katika ombi lao, Ongegu alisema miseto 26 ya masomo imeathiriwa na idadi ya shule hizo 1,000, hali inayoficha taasisi nyingine zinazotoa masomo hayo. Kwa mfano, mseto wa ST1048 unaojumuisha Baiolojia, Kemia na Fizikia katika mkondo wa Sayansi, Tekonolojia na Hisbati (STEM) una shule 10,515 zinazodaiwa kuutoa nchini, lakini mfumo unaonyesha shule 1,000 pekee. Hii ina maana kuwa wanafunzi wanaona takriban asilimia 9.51 pekee ya shule zinazopatikana kwa mseto huo. Walalamishi pia wanasema kuwa kati ya mIseto 418 iliyoorodheshwa kwenye mfumo, 28 haina shule yoyote iliyoonyeshwa, huku 303 ikiwa na shule 94 au chini ya hapo. Wanasema kasoro hizo zinazuia wanafunzi na wazazi kupata taarifa sahihi kabla ya kufanya maamuzi yatakayoathiri masomo yao ya baadaye. “Hii haiwezi kuachwa bila kurekebishwa hadi wanafunzi watakapofika wakati wa kuomba nafasi za shahada na diploma kupitia KUCCPS,” sehemu ya kesi inasema. Pia walalamishi wameibua wasiwasi kuhusu jinsi masomo ya Gredi 10 yatakavyoathiri nafasi za kujiunga na vyuo vikuu. Wanasema hakuna ufafanuzi wa kutosha kuhusu jinsi somo la Community Service Learning litakavyoathiri wanafunzi kujiunga na kozi mbalimbali. Wanataka mahakama itangaze kuwa kuonyesha orodha zisizokamilika bila kutoa tahadhari kunakiuka haki za wanafunzi. Pia wanataka wizara iamriwe kufungua tena mfumo huo ili wanafunzi warekebishe uchaguzi wao baada ya kupewa taarifa kamili kuhusu shule na mseto wa masomo. Wamependekeza mfumo ufunguliwe tena baada ya mitihani ya tathmini ya Gredi 9 kuanza Oktoba 26, ili kuepusha kuwaongezea watahiniwa shinikizo. Mfumo wa KEMIS ulifunguliwa Agosti 24, 2026, na muda wa kuchagua shule uliongezwa hadi Septemba 15.
EducationalKiruswa akabidhi vifaa shule ya Lesing’ita
LONGIDO: NAIBU Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Longido mkoani Arusha, Dk. Stephen Kiruswa, amekabidhi mashine ya kunakili na kuchapisha nyaraka pamoja na kompyuta kwa Shule ya Msingi Lesing’ita, vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni tatu, ili kupunguza gharama za shule katika uchapishaji wa karatasi za mazoezi, mitihani na shughuli nyingine za…