TUME ya kuajiri walimu (TSC) imetangaza upya nyadhifa 1,631 za kuwapandisha cheo wasimamizi wa shule, na kuwapa fursa nyingine walimu wanaomezea mate nyadhifa za uongozi huku kukiwa na uhaba wa wasimamizi waliothibitishwa katika shule za umma.
Nyadhifa hizo zinajumuisha nafasi 1,470 za Naibu Mwalimu mkuu, 132 Naibu Mwalimu Mkuu III na 29 za Mwalimu Mkuu II katika shule za msingi na sekondari.
Tume imealika maombi kutoka kwa walimu wanaohudumu waliofuzu kujaza nafasi hizi za kupandishwa cheo kuambatana na Mwongozo wa Maendeleo Kitaaluma kwa Walimu.
Maombi ni sharti yapokewe kufikia usiku wa manane Jumatatu Septemba 14, 2026, ilisema TSC katika notisi.
Tangazo hilo jipya limejiri wiki chache tu baada ya Tume kuzindua mchakato wa kupandisha cheo uliojumuisha walimu 34,016 katika daraja zote, katika kile kilichotajwa kuwa moja kati ya shughuli kubwa zaidi za maendeleo kitaaluma katika miaka ya majuzi.
Shughuli hiyo iliyotangazwa Julai, iliangazia nyadhifa kuanzia Mwalimu wa Ngazi ya Juu II hadi Mwalimu Mkuu na ilijumuisha nyadhifa za kufundisha, usimamizi wa shule, kuboresha mtaala na vyuo vya mafunzo ya walimu.
Nyadhifa mpya zilizotangazwa ni muhimu, kwa sababu zinalenga nafasi za usimamizi wa shule wakati ambapo maelfu ya shule za umma zinaendeshwa bila wasimamizi waliothibitishwa.
Mchakato huo wa kupandisha vyeo umejiri kukiwa na malalamishi kuhusu kukwama kitaaluma katika huduma ya kufundisha.
TSC ilieleza Bunge kwamba walimu 178,871 wa shule za msingi na sekondari wamesalia katika daraja lile lile la kazi kutokana na upungufu kwenye bajeti, huku tume ikisema inahitaji mabilioni kushughulikia suala hilo.
Tume ilisema sehemu kubwa ya walimu waliokwama kitaaluma ni kutoka gredi C3 kwa walimu wa sekondari na gredi C1 kwa walimu wa shule ya msingi ambapo waelimishaji wengi wamesalia kwa miaka mingi licha ya kutimiza viwango vya kufuzu kupandishwa cheo.
“Tunaitaka TSC kutangaza mara moja nyadhifa za kuwapandisha vyeo walimu 135,000 ambao wamekwama katika daraja zao za kazi,” alisema Katibu Mkuu wa Kuppet, Bw Akello Misori.
TSC yatangaza nafasi 1,631 kwa walimu wanaotaka kupanda ngazi

This story was originally published by Taifa Leo.
Read the full story at Taifa LeoRelated stories
EducationalChama cha CHAWAKAMA-KENYA kinavyopeleka Kiswahili jukwaa la kimataifa
CHAMA cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA-KENYA) kimezidisha juhudi za kukiendeleza Kiswahili na kukipa nafasi katika ulimwengu wa utandawazi kupitia makongamano yanayowaleta pamoja wanazuo, watafiti na wadau wa lugha hii adhimu. Mbali na kukuza Kiswahili, chama hiki kimekuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wanafunzi wa vyuo vikuu, kuibua vipaji, kujenga mitandao ya kitaaluma na kuhamasisha ubunifu. Pia, kimechangia kuzalisha viongozi, waandishi, wahariri, watafiti na wakalimani watakaokipeperusha Kiswahili katika majukwaa ya kimataifa. Mwelekeo huo ulidhihirika Novemba 6–7 mwaka huu, wakati CHAWAKAMA-Kenya kilipoandaa kongamano la kikanda katika Chuo Kikuu cha Laikipia, lililoongozwa na kaulimbiu ya ‘Kiswahili na Utandawazi’. Kongamano hilo liliwakutanisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali, vikiwemo Rongo, Laikipia, Masinde Muliro, Kisii, Daystar, Kabianga, Murang’a, Turkana na Kaimosi. Washiriki walijadili nafasi ya Kiswahili katika kuzalisha maarifa, kuwasilisha uvumbuzi na kutatua changamoto za jamii. Kongamano lilifunguliwa rasmi na Prof Guyo Sarr Huka, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Laikipia anayesimamia masuala ya kitaaluma. Katika tukio hilo, kamati andalizi ikiongozwa na Mwenyekiti Clinton Ageta na mlezi wa chama Prof Sheila Wandera, ilizindua bidhaa zenye nembo ya CHAWAKAMA-Kenya, zikiwemo mashati-tao, chepeo, kalamu, bango na vitabu vilivyoandikwa na wanachama. Ubunifu wa wanachama ulijitokeza pia kupitia Kishazi TV, runinga ya mtandaoni iliyorusha matukio ya kongamano mubashara na kusambaza maudhui yake kupitia mitandao ya kijamii. Kongamano lilipambwa na michango ya wataalamu mashuhuri wa Kiswahili, akiwemo Dkt Moses Wasike (Mgeni Rasmi), Dkt Riro Matinde, Prof James Ontieri, Dkt Nixon Sangili na Dkt Sussy Nandama, miongoni mwa wengine. Mafanikio hayo yalitokana na ushirikiano wa CHAWAKAMA-Kenya, Idara ya Masomo ya Kibinadamu na Maendeleo, uongozi wa Chuo Kikuu cha Laikipia na Chama cha Kiswahili cha Laikipia (CHAKILA). Chama hicho kinaongozwa na Clinton Ageta (Mwenyekiti), Granton Mdogo (Naibu Mwenyekiti), Doreen Mukami (Katibu Mkuu), Griffin Amakala (Naibu Katibu Mkuu), Diana Mirriam (Mhazini), Velma Natang’a (Afisa wa Uhusiano Mwema), Micah Sikolia (Katibu Mtendaji) na Okimba Lester (Afisa Mwenezi). Wahariri ni Luke Shikoli, Kweyu Remjo, Augustine Wekesa, Winjoy Gacheri na Zdame Zuhura, huku Samson Nyamosi na Denis Chumo wakihudumu kama Maafisa wa Nidhamu. Kwa hakika, CHAWAKAMA-Kenya kinaendelea kuthibitisha kuwa mustakabali wa Kiswahili unategemea ubunifu, ushirikiano na juhudi za kizazi kipya.
Educational‘Shule zisizo na vifaa zisipokee wanafunzi wa amali’
MOROGORO: WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amewaagiza maofisa uthibiti ubora wa shule kufuatilia shule zote zinazotoa elimu ya amali na kuhakikisha zina miundombinu, vifaa na vitendea kazi vinavyokidhi mahitaji ya mafunzo ya ufundi. Amesema shule zilizosajiliwa kutoa elimu ya amali lakini hazina vifaa vya kufundishia na kujifunzia hazipaswi kuendelea kupokea wanafunzi…
EducationalWazazi wapinga mfumo wa uchaguzi wa shule za sekondari
WAZAZI wawili wamewasilisha kesi mahakamani kutaka Wizara ya Elimu izuiwe kukamilisha uteuzi wa wanafunzi wa Gredi 10 katika shule za sekondari, wakidai mfumo wa kusimamia habari za elimu Kenya ( KEMIS) una hitilafu zinazowanyima wanafunzi nafasi ya kuchagua shule wanazotaka. Mabw Omwenga Ongegu na John Ominde wanasema mfumo huo unaonyesha shule 1,000 pekee kwa kila mseto wa masomo, hata pale ambapo shule nyingi zaidi zinatoa mseto huo nchini. Pia wanadai kuwa baadhi ya miseto ya masomo haina shule zilizoorodheshwa. Katika ombi lao, Ongegu alisema miseto 26 ya masomo imeathiriwa na idadi ya shule hizo 1,000, hali inayoficha taasisi nyingine zinazotoa masomo hayo. Kwa mfano, mseto wa ST1048 unaojumuisha Baiolojia, Kemia na Fizikia katika mkondo wa Sayansi, Tekonolojia na Hisbati (STEM) una shule 10,515 zinazodaiwa kuutoa nchini, lakini mfumo unaonyesha shule 1,000 pekee. Hii ina maana kuwa wanafunzi wanaona takriban asilimia 9.51 pekee ya shule zinazopatikana kwa mseto huo. Walalamishi pia wanasema kuwa kati ya mIseto 418 iliyoorodheshwa kwenye mfumo, 28 haina shule yoyote iliyoonyeshwa, huku 303 ikiwa na shule 94 au chini ya hapo. Wanasema kasoro hizo zinazuia wanafunzi na wazazi kupata taarifa sahihi kabla ya kufanya maamuzi yatakayoathiri masomo yao ya baadaye. “Hii haiwezi kuachwa bila kurekebishwa hadi wanafunzi watakapofika wakati wa kuomba nafasi za shahada na diploma kupitia KUCCPS,” sehemu ya kesi inasema. Pia walalamishi wameibua wasiwasi kuhusu jinsi masomo ya Gredi 10 yatakavyoathiri nafasi za kujiunga na vyuo vikuu. Wanasema hakuna ufafanuzi wa kutosha kuhusu jinsi somo la Community Service Learning litakavyoathiri wanafunzi kujiunga na kozi mbalimbali. Wanataka mahakama itangaze kuwa kuonyesha orodha zisizokamilika bila kutoa tahadhari kunakiuka haki za wanafunzi. Pia wanataka wizara iamriwe kufungua tena mfumo huo ili wanafunzi warekebishe uchaguzi wao baada ya kupewa taarifa kamili kuhusu shule na mseto wa masomo. Wamependekeza mfumo ufunguliwe tena baada ya mitihani ya tathmini ya Gredi 9 kuanza Oktoba 26, ili kuepusha kuwaongezea watahiniwa shinikizo. Mfumo wa KEMIS ulifunguliwa Agosti 24, 2026, na muda wa kuchagua shule uliongezwa hadi Septemba 15.
EducationalKiruswa akabidhi vifaa shule ya Lesing’ita
LONGIDO: NAIBU Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Longido mkoani Arusha, Dk. Stephen Kiruswa, amekabidhi mashine ya kunakili na kuchapisha nyaraka pamoja na kompyuta kwa Shule ya Msingi Lesing’ita, vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni tatu, ili kupunguza gharama za shule katika uchapishaji wa karatasi za mazoezi, mitihani na shughuli nyingine za…