Na Ramadhan Hassan, Dodoma
benki ya Maendeleo ya TIB imewekeza zaidi ya Sh bilioni 630 katika miradi ya maendeleo, ambayo imesaidia kuzalisha zaidi ya ajira 12,547 kwa Watanzania.
Hayo yameelezwa leo, Machi 20, Jijini Dodoma, na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB, Lilian Mbassy, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya benki hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Mbassy alisema kuwa kupitia uwekezaji huu mkubwa, benki hiyo imeweza kuzalisha ajira mpya 12,547, kutokana na kufadhili miradi ya muda wa kati na mrefu. Alifafanua kuwa fedha hizo za mikopo zimetumika katika sekta mbalimbali, ikiwemo miradi ya maji, nishati, utalii, viwanda, usafirishaji, na usalama wa chakula.
Alisema kuwa shilingi bilioni 11.5 zimewekezwa katika sekta ya nishati safi kupitia mradi wa upanuzi wa umeme vijijini, huku shilingi bilioni 250 zikielekezwa katika ukuaji wa uchumi na ajira.
Kaimu Mkurugenzi huyo pia alitaja vipaumbele vya benki hiyo kuwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali katika kutekeleza sera na mikakati ya kitaifa ili kuongeza kasi ya maendeleo.

