MTWARA: WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameuagiza Wakala wa Barabara (TANROAD) na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kusimamamia wakandarasi ili kutoa ajira kwa wananchi wazawa wanapotekeleza miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja.
Ulega ametoa agizo hilo leo Mei 27, 2025 alipotembelea na kukagua mradi wa ukarabati wa barabara ya Mtwara – Mingoyo (Mnazi Mmoja) yenye urefu wa km 82 kwa thamani ya Sh bilioni 152 na ile ya Mingoyo-Masasi yenye urefu wa Km 118 kwa thamani ya Sh bilioni 249.
“Ofisa rasilimali watu uhakikishe vijana wa hapa wanapata ajira, wakati wa kutoa ajira mshirikishe ofisi ya Mkuu wa Wilaya na serikali kwa ujumla, maafisa kazi waje hapa ili mwisho tuweze kujua mradi umeleta ajira ngapi kwa wananchi wetu,” amesema.
SOMA ZAIDI:
Ulega ataka kasi ujenzi miundombinu Dodoma
Akizungumza na wafanyakazi wa mradi huo Ulega amesema: “Barabara hii si ya mchina, ni yetu watanzania, msifanye udokozi, fanyeni kazi kwa kujituma ili mradi unapoisha muwe mmepata maarifa ambayo yatakusaidia kuwa fundi mzuri”.
Waziri Ulega ameeleza kuwa serikali imeanza mchakato wa kuwarasimisha mafundi wasio rasmi ambao hawajapita kwenye vyuo vya mafunzo ya ufundi ila wana uzoefu wa ujenzi ili wapewe ajira hivyo kuzitaka mamlaka pamoja na wakandarasi kutoa vyeti kwa wafundi pindi mradi unapokamilika vitakavyowawezesha kutambuliwa.
Aidha, Waziri Ulega amemtaka mkandarasi huyo kufanya kazi kwa wakati na kwa ubora kwani tayari Serikali imeshamlipa malipo ya awali.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amemshukuru Waziri Ulega pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuifungua Mtwara kwa miradi mbalimbali ya maendeleo.


