BAADHI ya maudhui katika mitandao ya kijamii hasa watoto wanapokaribia kufunga shule kwa likizo, huwa ni watu wakiulizana kuhusu bajeti zao za chakula.
Mbali na kiwango cha chakula, kuna wale wanaozungumzia saa ambapo wana wao hutaka kula, wengine hata wakisaka chakula usiku wa manane.
Hata hivyo, wataalamu wa lishe wanasema kuwa watoto hawa ambao pia wako katika umri ambao muda wao mwingi wanatumia katika masomo, asilimia ishirini ya kiwango cha chakula wanachokula kila mara hutumika na ubongo.
Kulingana na Tom Wanjala, baba wa watoto watatu ambaye kifungua mimba wake ana umri wa miaka 16 na mchezaji wa mchezo wa raga, anasimulia jinsi alivyoshuhudia mabadiliko hayo kwa mwanawe.
“Punde tu kifungua mimba wangu alipofikisha umri wa miaka 13, alianza kula chakula kingi zaidi. Hivi majuzi alipokuwa nyumbani kwenye likizo nilipokuwa nikimuangalia anavyokula sima maanake nilikuwa naye mezani, ndipo nilithibitisha kuwa katika umri wake na pia akiwa mtoto wa kiume anakula zaidi ya watu wengine katika familia,” anasema mzazi huyo.
Baba huyo pia anasema kuwa mwanawe alipokuwa wa umri mdogo, hamu yake ya kula ilikuwa chini sana. Kulingana naye, kumuona mwanawe kuwa na hamu ya juu ya kula kunamdhihirishia jinsi anavyozidi kukua.
Hamu ya kula imezidi
“Hata mwanangu ambaye ana umri wa miaka 10 pia nimegundua kuwa hamu yake ya kula imezidi kuongezeka kinyume na alivyokuwa akila hapo awali. Miaka ya hapo awali haswa walipokuwa chini ya umri wa miaka saba, nilikuwa nikiwalazimisha wote wawili kula lakini kwa sasa wanataka chakula wenyewe tena kwa wingi,” anaongeza Tom.
Mzazi huyo ambaye anaelewa sayansi ya matumizi ya lishe mwilini miongoni mwa watoto wanaobalehe, anasema kuwa kwa sasa jukumu lake ni kuhakikisha kuwa wanawe hawakosi chakula ilikuwasaidia kukua.
“Huwa namruhusu mwanangu ale kwa sababu najua atafika katika umri ambapo hamu yake ya chakula itapunguka jinsi tu yangu ilivyopunguka. Nilipokuwa kwenye umri wa kubalehe nilikuwa nikila jinsi tu mwanangu anavyokula kwa sasa. Nafahamu kuwa anahitaji nguvu nyingi za kutembea, kucheza na pia kwenye shughuli tofauti maanake ni vigumu sana kumpata akiwa ameketi tu na kutulia sehemu moja akiwa nyumbani,” anasimulia.
Alfrique Otieno Mwana, pia anashuhudia hali sawia kwake.
“Kifungua mimba wangu yuko katika Gredi 10. Wakati alipokuwa nyumbani kwenye likizo na kuketi kwenye meza alikuwa akipakua chakula kingi ambacho alikuwa akila chote. Mwenzake mdogo ambaye pia ni mvulana wa umri wa miaka 10 pia hula kiwango cha juu cha chakula kinyume na hapo awali,” anasema mzazi huyo.
Wakati uo huo, Alfrique anasema kuwa kifungua mimba wake ambaye yuko katika shule ya bweni huwa na hamu ya juu ya chakula kutokana na tamaa ya kukosa chakula cha nyumbani kwa muda.
“Anapokuja nyumbani wakati wa likizo anataka sana kula chapati na akipewa moja au mbili hashibi. Unapata anakula tatu au nne ndiposa anashiba. Huwa namhimiza ale hadi ashibe kwa sababu hivyo ndivyo babangu alivyonifunza kula ilmradi siharibu chakula. Ninapomuona mwanangu anapokuwa na hamu ya juu ya kula chakula najua ni umri wake ambao ataupita siku za usoni,” anasema.
Ishara ya kukua
Kama tu Tom, mzazi Alfrique pia anakumbuka jinsi wanawe walipokuwa wachanga hawakuwa na hamu ya kula chakula. Kuwaona hamu yao ikiongezeka ni ishara kwake kuwa wanakua.
“Wakati wakiwa kwenye likizo wanakula mara tatu kwa siku na pia wanakula vitafunio katikati. Kitinda mimba wangu wa umri wa miaka miwili angali hana hamu ya kula hivyo mara nyingi anakula kiamsha kinywa kuchelewa kisha anakula chajio mapema kwa sababu huwa anaamka kuchelewa na pia analala mapema,” anasema Alfrique.
Kiwango cha lishe katika umri wa watoto wanaobalehe hutegemea na viwango vyao vya ukuaji.
Haya ni kwa mujibu wa mtaalamu wa lishe ya kitabibu katika hospitali ya, Aga Khan University Hospital, Valentine Young Kwadha.
Wakati uo huo, anaeleza kuwa mabadiliko yanayoendelea katika mwili wa mtoto kuanzia umri wa miaka 10 huhitaji ale chakula kingi zaidi ya alivyokuwa akila hapo awali.
Hali hii anasema huchangia mtoto anayebalehe kula angalau asilimia 25 ya chakula zaidi ya kiwango ambacho mtu mzima katika familia hula.
“Haistahili kuwa jambo la kushtua kuona mtoto anayebalehe akila chakula kingi kwa sababu hicho ndicho kiwango wanachohitaji kulingana na shughuli za kimwili..Mahitaji ya nguvu mwilini mwa watoto hawa kwa ujumla huanzia 2,000 hadi 3,000 kilokalori kila siku. Hii ni sawa na kusema kuwa mtoto anakula mara sita kwa siku kwa sababu wanakula mara nyingi na kiwango cha chakula wanachokula pia kinaongezeka,” anaeleza mtaalamu huyo.
Kiwango cha mazoezi ya mwili
Pia anasema kuwa kiwango cha chakula watoto hawa hula hutofautiana kulingana na urefu, jinsia na kiwango cha mazoezi miongoni mwao.
Kwa mfano, mtoto wa umri wa miaka 13 aliye na urefu wa sentimita 120 atakula chakula zaidi ya mwenzake wa umri sawa lakini urefu wake ni sentimita 100.
“Jinsi mwili unavyotumia nguvu na virutubisho kuanzia umri wa miaka 10 hadi 13 huwa juu miongoni mwa watoto wavulana ukilinganishwa na wasichana. Katika umri huu, miili ya wasichana huunda seli za mafuta zaidi huku miili ya wavulana ikiunda misuli. Misuli inahitaji nguvu na virutubisho zaidi,” anasema Valentine.
Anawashauri wazazi wa watoto walio katika umri wa kubalehe kuwa watoto hao wanastahili kula kila baada ya saa 3-4.
Kiamsha kinywa, chakula cha mchana na chajio anasema zinastahili kuwa sehemu kuu ya mlo wao.
Katikati ya milo hiyo, anasema kuwa watoto hao wanastahili kula vitafunio kama vile matunda, njugu na sehemu ya kile walichobakisha wakati wa kiamsha kinywa kwa kuzingatia lishe bora.
“Sahani ya mtoto anayebalehe inastahili kuwa na wanga, vitamini na protini. Katika umri huu, watoto wanahitaji protini zaidi. Kwa mfano, ikiwa aina ya chakula cha protini unaowalisha ni mayai, basi watahitaji mayai mawili wakati wa kiamsha kinywa, mayai mawili wakati wa chakula cha mchana na mayai mawili kwa chajio. Mayai hayo yatawapa kiwango cha protini wanayohitaji siku hiyo,” anaeleza Valentine.
Vilevile, anawashauri wazazi kutowalisha watoto zaidi au kiwango cha chini cha chakula ili kuzuia watoto hao kukabiliwa na athari za utapiamlo.
Hali hiyo huweza kubainishwa kupitia ushauri wa mtaalamu wa lishe kwa sababu kila mtoto huhitaji ushauri binafsi kulingana na kiwango cha lishe miili yao inahitaji.
Kadhalika, anahimiza wazazi kuhakikisha kuwa watoto hawa wanapata usingizi wa kutosha wa kati ya saa nane hadi 10 mfululizo kila usiku, muda ambao pia hawastahili kuwa wanakula.
Kinachochangia matineja kuwa na hamu kubwa ya kula bila kunenepa

This story was originally published by Taifa Leo.
Read the full story at Taifa LeoRelated stories
EducationalChama cha CHAWAKAMA-KENYA kinavyopeleka Kiswahili jukwaa la kimataifa
CHAMA cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA-KENYA) kimezidisha juhudi za kukiendeleza Kiswahili na kukipa nafasi katika ulimwengu wa utandawazi kupitia makongamano yanayowaleta pamoja wanazuo, watafiti na wadau wa lugha hii adhimu. Mbali na kukuza Kiswahili, chama hiki kimekuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wanafunzi wa vyuo vikuu, kuibua vipaji, kujenga mitandao ya kitaaluma na kuhamasisha ubunifu. Pia, kimechangia kuzalisha viongozi, waandishi, wahariri, watafiti na wakalimani watakaokipeperusha Kiswahili katika majukwaa ya kimataifa. Mwelekeo huo ulidhihirika Novemba 6–7 mwaka huu, wakati CHAWAKAMA-Kenya kilipoandaa kongamano la kikanda katika Chuo Kikuu cha Laikipia, lililoongozwa na kaulimbiu ya ‘Kiswahili na Utandawazi’. Kongamano hilo liliwakutanisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali, vikiwemo Rongo, Laikipia, Masinde Muliro, Kisii, Daystar, Kabianga, Murang’a, Turkana na Kaimosi. Washiriki walijadili nafasi ya Kiswahili katika kuzalisha maarifa, kuwasilisha uvumbuzi na kutatua changamoto za jamii. Kongamano lilifunguliwa rasmi na Prof Guyo Sarr Huka, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Laikipia anayesimamia masuala ya kitaaluma. Katika tukio hilo, kamati andalizi ikiongozwa na Mwenyekiti Clinton Ageta na mlezi wa chama Prof Sheila Wandera, ilizindua bidhaa zenye nembo ya CHAWAKAMA-Kenya, zikiwemo mashati-tao, chepeo, kalamu, bango na vitabu vilivyoandikwa na wanachama. Ubunifu wa wanachama ulijitokeza pia kupitia Kishazi TV, runinga ya mtandaoni iliyorusha matukio ya kongamano mubashara na kusambaza maudhui yake kupitia mitandao ya kijamii. Kongamano lilipambwa na michango ya wataalamu mashuhuri wa Kiswahili, akiwemo Dkt Moses Wasike (Mgeni Rasmi), Dkt Riro Matinde, Prof James Ontieri, Dkt Nixon Sangili na Dkt Sussy Nandama, miongoni mwa wengine. Mafanikio hayo yalitokana na ushirikiano wa CHAWAKAMA-Kenya, Idara ya Masomo ya Kibinadamu na Maendeleo, uongozi wa Chuo Kikuu cha Laikipia na Chama cha Kiswahili cha Laikipia (CHAKILA). Chama hicho kinaongozwa na Clinton Ageta (Mwenyekiti), Granton Mdogo (Naibu Mwenyekiti), Doreen Mukami (Katibu Mkuu), Griffin Amakala (Naibu Katibu Mkuu), Diana Mirriam (Mhazini), Velma Natang’a (Afisa wa Uhusiano Mwema), Micah Sikolia (Katibu Mtendaji) na Okimba Lester (Afisa Mwenezi). Wahariri ni Luke Shikoli, Kweyu Remjo, Augustine Wekesa, Winjoy Gacheri na Zdame Zuhura, huku Samson Nyamosi na Denis Chumo wakihudumu kama Maafisa wa Nidhamu. Kwa hakika, CHAWAKAMA-Kenya kinaendelea kuthibitisha kuwa mustakabali wa Kiswahili unategemea ubunifu, ushirikiano na juhudi za kizazi kipya.
Educational‘Shule zisizo na vifaa zisipokee wanafunzi wa amali’
MOROGORO: WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amewaagiza maofisa uthibiti ubora wa shule kufuatilia shule zote zinazotoa elimu ya amali na kuhakikisha zina miundombinu, vifaa na vitendea kazi vinavyokidhi mahitaji ya mafunzo ya ufundi. Amesema shule zilizosajiliwa kutoa elimu ya amali lakini hazina vifaa vya kufundishia na kujifunzia hazipaswi kuendelea kupokea wanafunzi…
EducationalWazazi wapinga mfumo wa uchaguzi wa shule za sekondari
WAZAZI wawili wamewasilisha kesi mahakamani kutaka Wizara ya Elimu izuiwe kukamilisha uteuzi wa wanafunzi wa Gredi 10 katika shule za sekondari, wakidai mfumo wa kusimamia habari za elimu Kenya ( KEMIS) una hitilafu zinazowanyima wanafunzi nafasi ya kuchagua shule wanazotaka. Mabw Omwenga Ongegu na John Ominde wanasema mfumo huo unaonyesha shule 1,000 pekee kwa kila mseto wa masomo, hata pale ambapo shule nyingi zaidi zinatoa mseto huo nchini. Pia wanadai kuwa baadhi ya miseto ya masomo haina shule zilizoorodheshwa. Katika ombi lao, Ongegu alisema miseto 26 ya masomo imeathiriwa na idadi ya shule hizo 1,000, hali inayoficha taasisi nyingine zinazotoa masomo hayo. Kwa mfano, mseto wa ST1048 unaojumuisha Baiolojia, Kemia na Fizikia katika mkondo wa Sayansi, Tekonolojia na Hisbati (STEM) una shule 10,515 zinazodaiwa kuutoa nchini, lakini mfumo unaonyesha shule 1,000 pekee. Hii ina maana kuwa wanafunzi wanaona takriban asilimia 9.51 pekee ya shule zinazopatikana kwa mseto huo. Walalamishi pia wanasema kuwa kati ya mIseto 418 iliyoorodheshwa kwenye mfumo, 28 haina shule yoyote iliyoonyeshwa, huku 303 ikiwa na shule 94 au chini ya hapo. Wanasema kasoro hizo zinazuia wanafunzi na wazazi kupata taarifa sahihi kabla ya kufanya maamuzi yatakayoathiri masomo yao ya baadaye. “Hii haiwezi kuachwa bila kurekebishwa hadi wanafunzi watakapofika wakati wa kuomba nafasi za shahada na diploma kupitia KUCCPS,” sehemu ya kesi inasema. Pia walalamishi wameibua wasiwasi kuhusu jinsi masomo ya Gredi 10 yatakavyoathiri nafasi za kujiunga na vyuo vikuu. Wanasema hakuna ufafanuzi wa kutosha kuhusu jinsi somo la Community Service Learning litakavyoathiri wanafunzi kujiunga na kozi mbalimbali. Wanataka mahakama itangaze kuwa kuonyesha orodha zisizokamilika bila kutoa tahadhari kunakiuka haki za wanafunzi. Pia wanataka wizara iamriwe kufungua tena mfumo huo ili wanafunzi warekebishe uchaguzi wao baada ya kupewa taarifa kamili kuhusu shule na mseto wa masomo. Wamependekeza mfumo ufunguliwe tena baada ya mitihani ya tathmini ya Gredi 9 kuanza Oktoba 26, ili kuepusha kuwaongezea watahiniwa shinikizo. Mfumo wa KEMIS ulifunguliwa Agosti 24, 2026, na muda wa kuchagua shule uliongezwa hadi Septemba 15.
EducationalKiruswa akabidhi vifaa shule ya Lesing’ita
LONGIDO: NAIBU Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Longido mkoani Arusha, Dk. Stephen Kiruswa, amekabidhi mashine ya kunakili na kuchapisha nyaraka pamoja na kompyuta kwa Shule ya Msingi Lesing’ita, vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni tatu, ili kupunguza gharama za shule katika uchapishaji wa karatasi za mazoezi, mitihani na shughuli nyingine za…