HOMA Bay imekumbwa na ukosefu wa usalama huku wakazi wakitumia majina ya utani kama vile Yemen na Haiti kurejelea hali katika kaunti hiyo.
Wakazi wanalalamikia ongezeko la kundi la magenge linalowahangaisha wafanyabiashara na wanafunzi.
Majina hayo yalianza kusambaa mitandaoni baada ya mkutano wa Linda Mwananchi uliofanyika Agosti 16, 2026, huku picha za maeneo kame ya Suba zikilinganishwa na nchi za Mashariki ya Kati.
Hata hivyo, jina la Haiti lilipata umaarufu zaidi kutokana na vitisho vilivyotokana na magenge yanayodaiwa kutumia mapanga kuwashambulia na kuwaibia wananchi.
Magenge hayo yanadaiwa kuwatisha wafanyabiashara, kuwatoza madereva wa magari ya uchukuzi fedha na kuchukua chakula na vinywaji katika vibanda na mikahawa bila kulipa.
Mwenyekiti wa Muungano wa Wafanyabiashara Homa Bay Jack Nyambega alisema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifunga maduka yao mapema kwa kuhofia kushambuliwa wanaporejea nyumbani wakiwa na mapato ya siku.
Alisema maandamano yaliyotokea baada ya kukamatwa kwa Kassim Abdi, anayezuiliwa kuhusiana na kuongoza magenge hayo, yalisababisha uporaji wa bidhaa na uharibifu wa maduka.
Bw Nyambega alisema biashara nyingi zilisitishwa, huku wafanyabiashara wadogo wakikabiliwa na changamoto za kulipa mikopo ya biashara kutokana na kukosa mapato.
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tom Mboya pia wameathiriwa na hali hiyo. Mwenyekiti wa chama cha wanafunzi Collins Ouma alisema baadhi yao wameibiwa simu na pesa, huku wengine wakishambuliwa wanapotembea usiku kutafuta chakula au kushughulikia mahitaji yao.
Alitaka polisi kuongeza doria na kuwakamata wahalifu.
Katika kukabiliana na hali hiyo, polisi walianzisha operesheni kali Oktoba 10 baada ya siku mbili za maandamano yenye vurugu. Zaidi ya washukiwa 40 walikuwa wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kufikia wiki iliyopita.
Polisi pia wamebomoa vibanda vinavyodaiwa kutumiwa kama maficho ya magenge hayo katika mzunguko wa Kodoyo na kituo cha mabasi. Maafisa wenye silaha wameendelea kufanya doria mjini humo.
Katibu Mkuu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Raymond Omollo alisema operesheni hiyo itaendelea hadi amani irejee kikamilifu.
Alionya wahalifu dhidi ya kuwatisha wafanyabiashara na kuvuruga shughuli zao, akisema serikali pia itashirikiana na vijana kuwapa fursa za elimu na kujikimu kimaisha.
Kamishina wa Kaunti ya Homa Bay Ronald Mwiwawi alisema maafisa wa usalama wataendelea kulinda biashara na kuhakikisha wakazi wanaendesha shughuli zao bila hofu.
Hofu ‘Panga Boys’ wakihangaisha wakazi

This story was originally published by Taifa Leo.
Read the full story at Taifa LeoRelated stories
BusinessWafanyabiashara Moro wahamasishwa malipo kidigitali
MOROGORO:BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewahimiza wafanyabiashara nchini kutumia mifumo ya malipo ya kidijitali katika manunuzi na mauzo ya bidhaa zao, ikieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza kasi ya mzunguko wa fedha katika uchumi na kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na kubeba fedha taslimu. Rai hiyo imetolewa na Ofisa wa BOT kutoka Kurugenzi ya Mifumo…
BusinessWhy Ajaokuta remains moribund after 40 years — NES president
By Emma Ujah, Abuja Bureau Chief The President of the Nigerian Economic Society (NES), Dr. Baba Musa, has attributed the continued failure of the multi-billion-dollar Ajaokuta Steel Company to the absence of sustained long-term development plans. Musa said this at the 2026 National Growth and Development Forum (NGDF), with the theme, “The Nigeria We Want: […]
BusinessBoT yaimarisha ujumuishi wa kifedha kwa walemavu
IRINGA: Walemavu mkoani Iringa wameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kutoa elimu ya fedha inayowasaidia kuelewa utunzaji sahihi wa fedha, matumizi ya mikopo na namna ya kutambua alama za usalama zilizopo kwenye noti, huku wakiiomba benki hiyo kupanua wigo wa mafunzo hayo ili yawafikie walemavu wengi zaidi, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini. Pongezi hizo…
BusinessMuseveni, Samia push railway link to DRC
This could reshape trade routes into the Great Lakes region.