DAR ES SALAAM: MENEJA Mkazi wa Kampuni ya Moil Industries Dk Sajad Habib Rai ametunukiwa tuzo ya Mchango wa muda mrefu (Lifetime Achievement Award) na taasisi ya Mikono Tanzania, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake katika sekta ya nishati ya mafuta nchini Tanzania.
Tuzo hiyo na nyinginezo zilizotolewa Novemba 27,2026 Jijini Dar es Salaam kwa watendaji na viongozi wengine wa taasisi mbalimbali, zimelenga kutambua juhudi zao katika maeneo mbalimbali ya kazi wanapozitumikia nafasi zao.
Akizungumza muda mfupi mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Dk Sajad amesema kwake hiyo ni hatua nyingine kubwa ikizingatiwa kuwa siku moja kabla ya kupokea tuzo hiyo alipokea tuzo nyingine iliyotambua mchango wake katika sekta hiyo ya nishati ya mafuta.
“Namshukuru Mungu kwa hatua hii kubwa lakini pia nitumie nafasi hii kwa kuwashukuru waandaji wa tuzo hizi kwa kuona mchango wangu ninaoutoa kwa Kampuni yangu lakini pia kwa Taifa langu katika eneo hili la Nishati ya mafuta, naahidi kuendelea kutumia weledi wangu ili kuleta mabadiriko chany,” amesema Dk Sajad.
Mbunifu huyo wa mfumo wa udhibiti wa mafuta (BIL), unaolenga kupunguza mianya ya udanganyifu katika uagizaji na ununuzi wa mafuta na hivyo kuchangia mapato kwa Serikali pamoja na mambo mengine amewataka watendaji wengine kutoka taasisi mbalimbali kutumia nafasi walizonazo kuleta tija katika maeneo yao ya kazi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mratibu na Mwanzilishi wa tuzo hizo Deogratius Kihwele pamoja na pongezi zake kwa washindi wa tuzo hizo pia amewahimiza viongozi na watendaji wakuu wa kampuni na taasisi nchini kuendelea kufanya kazi kwa ubunifu, weledi, uadilifu na kuleta matokeo chanya katika taasisi wanazoziongoza.
Takribani Wakurugenzi, Mameneja na Wakuu wa Taasisi mbalimbali za umma na binafasi kutoka ndani na nje ya nchi walipokea tuzo hizo ikiwa ni utaratibu wa kila Mwaka unaofanywa na taasisi ya mikono huku wakitajia kuandaa tuzo zingine mwakani kwa viongozi wa kidunia zinazotarajiwa kufanyika nchini Dubai.




