ZAIDI ya watahiniwa milioni 3.6 wanaojiandaa kufanya mitihani na tathmini za kitaifa wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha shuleni na tishio la mgomo wa walimu wanaosimamia na kusahihisha mitihani.
Watahiniwa 1,048,355 wa Mtihani wa Kitaifa cha Kidato cha Nne (KCSE) walifanya maandalizi ya mwisho mnamo Alhamisi, huku mitihani ya utendaji ikipangwa kuanza Jumatatu, Oktoba 19, 2026. Mitihani mikuu itafanyika kuanzia Novemba 2 hadi 20.
Wakati huo huo, watahiniwa wa Tathmini ya Elimu ya Msingi (KPSEA) na Tathmini ya Elimu ya Sekondari ya Chini (KJSEA) wanatarajiwa kufanya mitihani yao baadaye mwezi huu.
Hata hivyo, maandalizi yamekumbwa na mgogoro wa malipo baada ya Muungano wa Walimu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai (Kuppet) kuwataka wanachama wake kususia usimamizi, uangalizi na usahihishaji wa mitihani hadi malalamishi yao yatakaposhughulikiwa.
Katibu Mkuu wa Kuppet, Akello Misori, anataka wasimamizi walipwe angalau Sh4,000 kwa siku na walimu wanaosahihisha karatasi za mitihani walipwe angalau Sh100 kwa kila karatasi.
Kwa sasa, wasimamizi hulipwa kati ya Sh630 na Sh680 kwa siku, huku malipo ya kusahihisha karatasi yakianzia Sh35 hadi Sh75.
Hali hiyo imewafanya walimu wakuu kutaka mkutano wa dharura kati ya Muungano wa Kitaifa wa Walimu Wakuu wa Shule za Upili (KESSHA), Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) na Kuppet ili kutafuta suluhu kabla ya mitihani kuanza.
Mwenyekiti wa KESSHA, Willy Kuria, alisema malalamishi ya walimu yana msingi, lakini kususia mitihani kutawaathiri zaidi ya watahiniwa milioni moja wa KCSE.
“Tunahitaji mkutano kutatua masuala haya. Badala ya mgomo, tunaweza kukubaliana jinsi ya kuendesha mitihani,” akasema.
Afisa Mkuu Mtendaji wa KNEC, David Njengere, alisema viwango vya malipo ya wasimamizi wa vituo, wasimamizi na walimu wanaosahihisha mitihani hupitiwa kila baada ya miaka minne na vinatarajiwa kufanyiwa marekebisho mwaka ujao.
Mbali na mgogoro huo, shule zinakabiliwa na uhaba wa fedha za kununua vifaa vya maabara na mahitaji mengine ya mitihani ya vitendo.
KESSHA inasema shule za sekondari za umma zimekosa Sh5,787 kwa kila mwanafunzi katika mgao wa mwaka huu, hali inayozilazimisha baadhi kukopa kutoka kwa wasambazaji.
Serikali inapaswa kutoa Sh22,244 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka, lakini mgao uliopokelewa umekuwa chini ya kiwango hicho.
Katika hatua nyingine, maafisa wa elimu na usalama wamesema mipango imewekwa kuhakikisha watahiniwa wanalindwa na mitihani inafanyika bila udanganyifu. Katika Kaunti ya Nakuru, watahiniwa 48,038 wanatarajiwa kufanya mitihani katika vituo 485.
KESSHA imesisitiza kuwa mazungumzo ya haraka ni muhimu ili kulinda uadilifu wa mitihani na kuhakikisha wanafunzi hawaadhibiwi kutokana na mizozo kati ya walimu na serikali.
Changamoto tele katika sekta ya elimu mitihani ya Kitaifa ikikaribia

This story was originally published by Taifa Leo.
Read the full story at Taifa LeoRelated stories
EducationalChama cha CHAWAKAMA-KENYA kinavyopeleka Kiswahili jukwaa la kimataifa
CHAMA cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA-KENYA) kimezidisha juhudi za kukiendeleza Kiswahili na kukipa nafasi katika ulimwengu wa utandawazi kupitia makongamano yanayowaleta pamoja wanazuo, watafiti na wadau wa lugha hii adhimu. Mbali na kukuza Kiswahili, chama hiki kimekuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wanafunzi wa vyuo vikuu, kuibua vipaji, kujenga mitandao ya kitaaluma na kuhamasisha ubunifu. Pia, kimechangia kuzalisha viongozi, waandishi, wahariri, watafiti na wakalimani watakaokipeperusha Kiswahili katika majukwaa ya kimataifa. Mwelekeo huo ulidhihirika Novemba 6–7 mwaka huu, wakati CHAWAKAMA-Kenya kilipoandaa kongamano la kikanda katika Chuo Kikuu cha Laikipia, lililoongozwa na kaulimbiu ya ‘Kiswahili na Utandawazi’. Kongamano hilo liliwakutanisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali, vikiwemo Rongo, Laikipia, Masinde Muliro, Kisii, Daystar, Kabianga, Murang’a, Turkana na Kaimosi. Washiriki walijadili nafasi ya Kiswahili katika kuzalisha maarifa, kuwasilisha uvumbuzi na kutatua changamoto za jamii. Kongamano lilifunguliwa rasmi na Prof Guyo Sarr Huka, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Laikipia anayesimamia masuala ya kitaaluma. Katika tukio hilo, kamati andalizi ikiongozwa na Mwenyekiti Clinton Ageta na mlezi wa chama Prof Sheila Wandera, ilizindua bidhaa zenye nembo ya CHAWAKAMA-Kenya, zikiwemo mashati-tao, chepeo, kalamu, bango na vitabu vilivyoandikwa na wanachama. Ubunifu wa wanachama ulijitokeza pia kupitia Kishazi TV, runinga ya mtandaoni iliyorusha matukio ya kongamano mubashara na kusambaza maudhui yake kupitia mitandao ya kijamii. Kongamano lilipambwa na michango ya wataalamu mashuhuri wa Kiswahili, akiwemo Dkt Moses Wasike (Mgeni Rasmi), Dkt Riro Matinde, Prof James Ontieri, Dkt Nixon Sangili na Dkt Sussy Nandama, miongoni mwa wengine. Mafanikio hayo yalitokana na ushirikiano wa CHAWAKAMA-Kenya, Idara ya Masomo ya Kibinadamu na Maendeleo, uongozi wa Chuo Kikuu cha Laikipia na Chama cha Kiswahili cha Laikipia (CHAKILA). Chama hicho kinaongozwa na Clinton Ageta (Mwenyekiti), Granton Mdogo (Naibu Mwenyekiti), Doreen Mukami (Katibu Mkuu), Griffin Amakala (Naibu Katibu Mkuu), Diana Mirriam (Mhazini), Velma Natang’a (Afisa wa Uhusiano Mwema), Micah Sikolia (Katibu Mtendaji) na Okimba Lester (Afisa Mwenezi). Wahariri ni Luke Shikoli, Kweyu Remjo, Augustine Wekesa, Winjoy Gacheri na Zdame Zuhura, huku Samson Nyamosi na Denis Chumo wakihudumu kama Maafisa wa Nidhamu. Kwa hakika, CHAWAKAMA-Kenya kinaendelea kuthibitisha kuwa mustakabali wa Kiswahili unategemea ubunifu, ushirikiano na juhudi za kizazi kipya.
Educational‘Shule zisizo na vifaa zisipokee wanafunzi wa amali’
MOROGORO: WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amewaagiza maofisa uthibiti ubora wa shule kufuatilia shule zote zinazotoa elimu ya amali na kuhakikisha zina miundombinu, vifaa na vitendea kazi vinavyokidhi mahitaji ya mafunzo ya ufundi. Amesema shule zilizosajiliwa kutoa elimu ya amali lakini hazina vifaa vya kufundishia na kujifunzia hazipaswi kuendelea kupokea wanafunzi…
EducationalWazazi wapinga mfumo wa uchaguzi wa shule za sekondari
WAZAZI wawili wamewasilisha kesi mahakamani kutaka Wizara ya Elimu izuiwe kukamilisha uteuzi wa wanafunzi wa Gredi 10 katika shule za sekondari, wakidai mfumo wa kusimamia habari za elimu Kenya ( KEMIS) una hitilafu zinazowanyima wanafunzi nafasi ya kuchagua shule wanazotaka. Mabw Omwenga Ongegu na John Ominde wanasema mfumo huo unaonyesha shule 1,000 pekee kwa kila mseto wa masomo, hata pale ambapo shule nyingi zaidi zinatoa mseto huo nchini. Pia wanadai kuwa baadhi ya miseto ya masomo haina shule zilizoorodheshwa. Katika ombi lao, Ongegu alisema miseto 26 ya masomo imeathiriwa na idadi ya shule hizo 1,000, hali inayoficha taasisi nyingine zinazotoa masomo hayo. Kwa mfano, mseto wa ST1048 unaojumuisha Baiolojia, Kemia na Fizikia katika mkondo wa Sayansi, Tekonolojia na Hisbati (STEM) una shule 10,515 zinazodaiwa kuutoa nchini, lakini mfumo unaonyesha shule 1,000 pekee. Hii ina maana kuwa wanafunzi wanaona takriban asilimia 9.51 pekee ya shule zinazopatikana kwa mseto huo. Walalamishi pia wanasema kuwa kati ya mIseto 418 iliyoorodheshwa kwenye mfumo, 28 haina shule yoyote iliyoonyeshwa, huku 303 ikiwa na shule 94 au chini ya hapo. Wanasema kasoro hizo zinazuia wanafunzi na wazazi kupata taarifa sahihi kabla ya kufanya maamuzi yatakayoathiri masomo yao ya baadaye. “Hii haiwezi kuachwa bila kurekebishwa hadi wanafunzi watakapofika wakati wa kuomba nafasi za shahada na diploma kupitia KUCCPS,” sehemu ya kesi inasema. Pia walalamishi wameibua wasiwasi kuhusu jinsi masomo ya Gredi 10 yatakavyoathiri nafasi za kujiunga na vyuo vikuu. Wanasema hakuna ufafanuzi wa kutosha kuhusu jinsi somo la Community Service Learning litakavyoathiri wanafunzi kujiunga na kozi mbalimbali. Wanataka mahakama itangaze kuwa kuonyesha orodha zisizokamilika bila kutoa tahadhari kunakiuka haki za wanafunzi. Pia wanataka wizara iamriwe kufungua tena mfumo huo ili wanafunzi warekebishe uchaguzi wao baada ya kupewa taarifa kamili kuhusu shule na mseto wa masomo. Wamependekeza mfumo ufunguliwe tena baada ya mitihani ya tathmini ya Gredi 9 kuanza Oktoba 26, ili kuepusha kuwaongezea watahiniwa shinikizo. Mfumo wa KEMIS ulifunguliwa Agosti 24, 2026, na muda wa kuchagua shule uliongezwa hadi Septemba 15.
EducationalKiruswa akabidhi vifaa shule ya Lesing’ita
LONGIDO: NAIBU Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Longido mkoani Arusha, Dk. Stephen Kiruswa, amekabidhi mashine ya kunakili na kuchapisha nyaraka pamoja na kompyuta kwa Shule ya Msingi Lesing’ita, vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni tatu, ili kupunguza gharama za shule katika uchapishaji wa karatasi za mazoezi, mitihani na shughuli nyingine za…