EP ya Omari K yaiva Marekani

Mtanzania
Published: Jan 20, 2025 12:43:39 EAT   |  Entertainment

Kentucky, MAREKANI MSANII wa kizazi kipya anayefanya vyema nchini Marekani, Omari K, ameweka wazi ujio wa albamu yake fupi (EP) aliyoipa jina la I AM BANTU MUSIC, itakayotoka hivi karibu kwenye majukwaa (platforms) yote ya kupakua na kununua muziki duniani. Omari K ni miongoni mwa wasanii wa wachache sana wa Kitanzania wanaoishi Marekani wenye mafanikio […]

Kentucky, MAREKANI

MSANII wa kizazi kipya anayefanya vyema nchini Marekani, Omari K, ameweka wazi ujio wa albamu yake fupi (EP) aliyoipa jina la I AM BANTU MUSIC, itakayotoka hivi karibu kwenye majukwaa (platforms) yote ya kupakua na kununua muziki duniani.

Omari K ni miongoni mwa wasanii wa wachache sana wa Kitanzania wanaoishi Marekani wenye mafanikio makubwa kwenye tasnia ya muziki kama kushinda tuzo nne, kufanya kazi na mastaa wakubwa hapa Bongo kama Alikiba, Chino Wanaman na kolabo na Malkia wa mipasho, Khadija Omari Kopa.

Rapa huyo ambaye ni mmiliki wa leo ya Upendo Records na chombo cha habari, Upendo Records Media, ameweza kujizolea maelfu ya mashabiki ndani na nje ya Marekani akitumia lugha tofauti tofauti kama Kizigua,Kiswahili, Mai Mai na Kingereza.

Akizungumza na mtanzania.co.tz, Omari K amesema ndani ya EP hiyo mpya kutakuwa na nyimbo kali tano zitakazoendelea kumpa heshima yeye na tasnia ya muziki ya Tanzania hivyo mashabiki wakae mkao wa kuburudika.

“I AM BANTU MUSIC ni EP iliyoshiba, inayoendelea kunipa heshima, nimeshafanya mambo makubwa kwenye huu muziki na mwaka huu nitaendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania hapa Marekani kwenye tasnia ya muziki na hata filamu pia.

“Sababu tayari nimetoa kionjo (trailer) ya filamu yangu mpya inayoitwa Qeen of The Ring itakayoanza kuonyeshwa kwenye majumba ya sinema hapa Marekani Oktoba mwaka huu, hivyo naomba sapoti kwa mashabiki zangu wa Tanzania, Kenya na Afrika Mashariki yote kwani nawawakilisha vizuri hapa Marekani,” amesema Omari K ambaye mashabiki wamempachika jina jipya la K Boss.