Bingwa wa bendi ya Them Mushrooms Ted Kalanda afariki
MWANAMUZIKI mashuhuri na mwanzilishi wa bendi maarufu ya Them Mushrooms Ted Kalanda Harrison amefariki dunia.
Kalanda, 72, alikufa Jumanne, Septemba 17, 2024 nyumbani kwake Kaloleni, kaunti ya Kilifi baada ya kuugua kansa kwa miaka mingi.
Kakake mdogo, John Katana, ambaye ndiye kiongozi wa sasa wa bendi hiyo mnamo Jumanne alithibitisha habari hiyo ya tanzia.
Akasema: “Imekuwa safari ndefu yenye machungu kwa kaka yetu mkubwa, ambaye amekuwa mlezi wetu sote katika tasnia hii ya muziki.”
John alisema kakake alikata roho nyumbani kwake katika kijiji cha Mushrooms, Kaloleni.
Ted amekuwa akiugua kansa tangu mwaka wa 2018. Ugonjwa huo ulimwathiri hadi akapoteza uwezo wa kuona.
Katika miaka ya hivi karibuni, marehemu anayekumbukwa kwa kibao chake maarufu, “Jambo Bwana”, alikuwa amestaafu kutoka muziki.
Wimbo huo ulipata umaarufu mkubwa katika anga za kimataifa na imeigwa na wanamuziki wengi wa humu nchini na wale wa ng’ambo.
Ted ambaye alikuwa mchezaji maarufu wa chombo cha saxophoni na mwimbaji, aliasisi bendi ya Them Mushrooms mnamo 1972.
Ilikuwa ni bendi ya familia japo ilishirikisha marafiki kadhaa wa Ted kutoka Mombasa.
Inashikilia rekodi kama bendi ambaye imedumu kwa miaka mingi zaidi miongoni mwa bendi za Kenya
Wanachama asilia wa bendi hiyo walikuwa kaka wawili Teddy Kalanda na George Zirro (sasa marehemu), Billy Sarro, Denis Kalume (marehemu) na Joh Katana (kakake Ted).
Wakati huu, bendi ya Them Mushrooms inaongozwa na Kataba akisaidiana na Billy.
Katika miaka ya 1980s bendi hiyo ilihama kutoka Mombasa hadi Nairobi na ikachomoa albamu moto moto kwa jina “At the Carnivore”.
Mnamo mwaka wa 2002 bendi hiyo ilibadilisha jina hadi kuitwa Uyoga Band kabla ya kurejelea jina lake asilia.
Nyimbo zingine ambazo bendi hiyo imechomoa ni pamoja na “Unkula huu” Wazee Wakatike”, “Nyambura”, “Ndogo Ndogo” , na “Hapo Kale” .
Kifungua mimba wa Ted, Henry Harrison pia ni mwanamuziki na anaishi Uswidi pamoja na mkewe.
Mipango ya mazishi itatangazwa baadaye.
Wakati huo huo, mashabiki wa Ted Kalanda walituma rambirambi zao kupitia mitandao ya kijamii baada ya wao kupata habari za kifo chake.
Patrick Mkando Farah na David Munga ambao ni wanachama wa kundi la Rabai Crew Welfare group walimtaja marehemu kama mwanamuzi wa kupigiwa mfano katika eneo zima la Pwani.