Timu 64 kuchuana Bonnah Segerea Cup, mshindi kunyakua Sh milioni 5

Mtanzania
Published: Apr 02, 2024 17:51:51 EAT   |  Sports

Na Nora Damian, Mtanzania Digital Timu 64 za soka kutoka katika mitaa na makundi mbalimbali ya Jimbo la Segerea zinatarajia kuchuana kuwania Bonnah Segerea Cup ambapo mshindi atazawadiwa Sh milioni 5. Mashindano hayo yatakayoanza kutimua vumbi Aprili 5 hadi Juni 2,2024 yanashirikisha timu 61 za mitaa yote ya jimbo hilo na timu tatu za makundi […]

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Timu 64 za soka kutoka katika mitaa na makundi mbalimbali ya Jimbo la Segerea zinatarajia kuchuana kuwania Bonnah Segerea Cup ambapo mshindi atazawadiwa Sh milioni 5.

Mashindano hayo yatakayoanza kutimua vumbi Aprili 5 hadi Juni 2,2024 yanashirikisha timu 61 za mitaa yote ya jimbo hilo na timu tatu za makundi ya waendesha bajaji, bodaboda na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Zawadi za washindi zimetangazwa leo Aprili 2,2024 wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo ambapo mshindi wa pili atazawadiwa Sh milioni 3 na wa tatu Sh milioni 2.

Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano ya soka aliyoyaandaa.

Katika mchezo wa rede utakaoratibiwa na UWT Ilala bingwa atazawadiwa Sh milioni 2, mshindi wa pili atazawadiwa Sh milioni 1 na wa tatu Sh 500,000.

Akizungumza katika hafla hiyo Bonnah amesema mashindano hayo yanalenga kuibua na kukuza vipaji vya vijana sambamba na kuwapatia fursa mbalimbali.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano ya soka yaliyoandaliwa na Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli.

“Nimekuwa nikiandaa mashindano haya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM hasa ikizingatiwa kwamba michezo ni ajira na afya. Kupitia michezo tutaweza pia kuimarisha ulinzi na usalama kwenye maeneo yetu,” amesema Bonnah.

Naye Katibu wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika jimbo hilo, Thomas Temsa, amesema mashindano hayo yameongeza hamasa kwa vijana kushiriki michezo na kukuza vipaji vyao.

“Mheshimiwa mbunge amefanya kazi kubwa, kwanza anaimarisha mahusiano kati yetu wenyeviti na kutujengea uelewa mpana. Mashindano haya yatakuwa sehemu ya hamasa kwa vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki kujiandikisha kupiga kura, tuwashawishi na tuwashirikishe,” amesema Temsa.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, amesema Bonnah anatekeleza Ilani ya Uchaguzi kwani ibara ya 242 na 243 zinasisitiza juu ya michezo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amempongeza Bonnah kwa kuandaa mashindano hayo ambayo yataleta chachu ya maendeleo na kuimarisha umoja na mshikamano kuanzia ngazi ya mtaa, kata hadi wilaya.

“Vijana watapata nafasi ya kujua afya zao zikoje, tumetoa maelekezo kwamba kutengwe muda wa dakika 20 vijana wawe wanapewa elimu kuhusu masuala ya afya na maadili. Polisi kata nao watoe elimu ya namna ya kuimarisha ulinzi na usalama kwenye maeneo yao,” amesema Mpogolo.

Amesema kupitia mashindano hayo vijana wataelimishwa juu ya umuhimu wa kujiandikisha kwa ajili ya maandalizi ya kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.

Aidha amewaasa vijana kutumia mashindano hayo kuzungumzia masuala yao ya kiuchumi ili waweze kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na halmashauri ambapo wametenga Sh bilioni 11 kwa mwaka 2024/25.

Mkuu huyo wa wilaya amesema pia kupitia mashindano hayo na mengine yanayoandaliwa katika majimbo ya wilaya hiyo inawezekana kuunda timu ya wilaya itakayoshiriki ligi mbalimbali hadi ligi kuu.

Katika uzinduzi huo mbunge huyo pia aligawa jezi kwa timu zote shiriki.