Tangazeni mazuri yanayofanywa na Serikali – Sidde

Mtanzania
Published: Nov 27, 2022 18:22:12 EAT   |  News

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, amewataka wanachama wa chama hicho kuwaeleza wananchi mambo ambayo yamefanyika kwenye maeneo yao ikiwamo miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa. Sidde ameyasema hayo Novemba 26,2022 wakati wa hafla ya kumpongeza iliyoandaliwa na wanachama wa CCM tawi la Shaurimoyo. Amesema mwaka 2024/25 kutakuwa na […]

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, amewataka wanachama wa chama hicho kuwaeleza wananchi mambo ambayo yamefanyika kwenye maeneo yao ikiwamo miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa.

Katibu wa CCM Tawi la Shaurimoyo, Mwajuma Mnekea, akimvisha taji Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, wakati wa hafla ya kumpongeza iliyoandaliwa na wanachama wa tawi hilo.

Sidde ameyasema hayo Novemba 26,2022 wakati wa hafla ya kumpongeza iliyoandaliwa na wanachama wa CCM tawi la Shaurimoyo.

Amesema mwaka 2024/25 kutakuwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofuatiwa na Uchaguzi Mkuu hivyo wananchi wana wajibu wa kufahamu miradi iliyotekelezwa katika sekta mbalimbali kwenye maeneo yao.

“Lengo kubwa la CCM ni kushinda uchaguzi na kushika dola hivyo, niwaombe wanachama wenzangu na viongozi, yapo mambo mengi ambayo Serikali imeyafanya, tufanye kazi kubwa ya kuwaeleza wananchi mambo makubwa ambayo yamefanyika katika maeneo yetu,” amesema Sidde.

Aidha amewaomba wanachama kuwapa ushirikiano viongozi wapya ili waweze kutimiza majukumu yao kwa kufuata haki na katiba kwani bila kufanya hivyo heshima ya Ilala inaweza kupotea.

Naye Katibu wa UVCCM Tawi la Shaurimoyo, Batuli Kibaja, ambaye alisoma risala iliyoandaliwa na uongozi wa tawi hilo amesema lina wanachama 900 lakini wanachama wapya walioingizwa Agosti mwaka huu hawajapata kadi za kielektroniki.

“Kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa kadi za kielektroniki, wanachama wengi kadi hazipatikani tunapata shida kuzifuatilia, tunaomba mtusaidie tuweze kuongeza wanachama.

“Changamoto nyingine ni ya miundombinu ya barabara, kipindi cha mvua wananchi wanapata taabu n ahata miundombinu ya majitaka si salama,” amesema Batuli.