Serikali yakabidhi eneo la ujenzi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu

Mtanzania
Published: Jun 02, 2023 15:37:14 EAT   |  News

Na Mwandishi Wetu, Arusha Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imekabidhi eneo la ujezi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kwa Mkandarasi ambaye ni CRJE (East Africa) Ltd na Mshauri Elekezi Aru Built Environment Consulting Company Ltd (ABECC) katika eneo la Lakilaki, jijini Arusha. Hafla […]

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imekabidhi eneo la ujezi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kwa Mkandarasi ambaye ni CRJE (East Africa) Ltd na Mshauri Elekezi Aru Built Environment Consulting Company Ltd (ABECC) katika eneo la Lakilaki, jijini Arusha.

Hafla ya makabidhiano ya eneo hilo la ujenzi imeongozwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Samwel Shelukindo ambaye amekabidhi eneo hilo kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baada ya makabidhiano hayo Dk. Shelukindo amesema kuwa Serikali imetoa eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 26 hivyo Wizara itaendelea kutoa usaidizi wa karibu katika usimamizi wa ujenzi wa mradi huu ambao katika hatua ya awali unatarajiwa kugharimu kiasi cha Sh billioni nane (8) na utakamilika baada ya miaka miwili kulingana na mkataba wa mradi huo.

“Ujenzi wa majengo ya mahakama hiyo utakuwa wa kisasa kwa kuwa umezingatia taratibu na vigezo vya ujenzi wa majengo ya ofisi za kimataifa ambapo pamoja na jengo kuu, kutakuwa pia na jengo la mahakama, hospitali, shule na mengine yanayoendana na huduma za mahakama hiyo,” alisema Dk. Shelukindo

Naye Rais wa Mahakama wa Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Imani Aboud alieleza kuwa amefurahishwa na hatua hiyo iliyofikiwa na Serikali ya kukabidhi eneo la ujenzi wa mradi huo lililosubiriwa kwa muda mrefu.

“Tunaishukuru na kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa hatua hii itaiwezesha Mahakama kuwa na majengo ya kisasa na ofisi za kudumu kwa ajili ya kutoa huduma zake na tunatarajia ujenzi wa maradi huu utakamilika kwa wakati na salama,” alisema Jaji Aboud.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella ameishukuru pia Serikali kwa kuitimza ndoto yake ya miaka mingi ya kujenga mahakama hiyo nchini ambayo italiletea fursa nyingi Jiji la Arusha ikiwemo ajira za mafundi, walinzi pamoja na kuongeza taswira nzuri ya jiji hilo la kitalii.

“Jiji la Arusha limebahatika kuwa mwenyeji wa taasisi za kimataifa zinazojengwa katika eneo hili la Lakilaki hivyo Mkoa utatoa usaidizi wakati wa ujenzi wa mradi huu ili ukamilike kwa ubora na wakati na kuyafikia malengo yaliyowekwa na Serikali,” alisema Mongella.

Hafla hiyo ya makabidhiano ilihudhuriwa pia na Meneja wa Mradi kutoka CRJE (East Africa) Ltd, Zhang Cuishan, Mshauri elekezi kutoka chuo cha Ardhi, QS. Dk. Godwin Maro, viongozi na Maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja watumishi kutoka Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.

Mwaka 2005 Umoja wa Afrika uliridhia kuwepo na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ambapo Tanzania ilijitolea kuwa mwenyeji wa Mahakama hiyo na kuanzia wakati huo Serikali imekuwa ikikamilisha taratibu mbalimbali za nyaraka za eneo la mradi ambao utajengwa katika eneo la Lakilaki nje kidogo ya jiji la Arusha.