Kwa nini tubadili mfumo wa usajili magazeti

Mtanzania
Published: Nov 28, 2022 06:10:00 EAT   |  News

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital SERIKALI imeshauriwa kubadili utaratibu wa toaji leseni za magazeti kutoka mfumo wa sasa wa kila mwaka badala yake yapewe usajili wa kudumu uliokuwa ukitumia awali. Aidha, imeshauriwa kuwepo kwa sheria ya adhabu ya miezi sita jela kwa kampuni zitakazoshindwa kulipa fedha za matangazo kwa vyombo vya habari ndani ya siku […]

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

SERIKALI imeshauriwa kubadili utaratibu wa toaji leseni za magazeti kutoka mfumo wa sasa wa kila mwaka badala yake yapewe usajili wa kudumu uliokuwa ukitumia awali.

Aidha, imeshauriwa kuwepo kwa sheria ya adhabu ya miezi sita jela kwa kampuni zitakazoshindwa kulipa fedha za matangazo kwa vyombo vya habari ndani ya siku 30.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Jukuwaa la Wahariri Tanzania(TEF), Deodatus Balile katika mkutano maalumu uliofanyika kwa njia ya mtandao ulioandaliwa na jukwaa kwa ajili ya kujadili mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria ya Habari nchini.

“Ili vyombo vya habari vifanye kazi kwa uhuru lazima baadhi ya vifungu viondolewe katika sheria ya sasa, miongoni mwa hivyo ni pamoja na utaratibu wa kutoa leseni kwa magazeti unaotumika hivi sasa.

“Wote ni mashahidi kwamba tumeshuhudia ukitumika vibaya kufifisha uhuru wa vyombo vya habari nchini. Mfano tumeshuhudia kusitisha leseni za magazeti ya Mawio, Mwanahalisi, Mseto, na kufuta Tanzania Daima, je utaratibu huu una faida yoyote zaidi ya kuua Uhuru wa Vyombo vya Habari?,”alihoji Balile.

Balile amesema kuwa kuna haja ya kurejea kwenye utaratibu wa awali ambapo gazeti lilikuwa linajiendesha bila kuwapo kwa utaratibu wa kufutwa baada ya kusajili.

“Je, kwa nini tusirudi katika utaratibu wa zamani ambapo gazeti lilikuwa linasajiliwa na kujiendesha bila kufutwa kama ilivyo sasa? mazingira yakiwa vizuri, sheria zikawa nzuri, matangazo yakatolewa kwa bei stahiki badala ya sasa ambapo wanashusha bei watakavyo, mapato ya vyombo vya habari yataongezeka,” amesema Balile.

Balile amesema kuwa idara ya Habari Maelezo inapewa madaraka na Sheria hii kifungu cha 5 (l) kuratibu matangazo yote ya Serikali na kwamba serikali haioni kuwa kifungu hicho kitapunguza ufanisi wa kutoa na kusambaza matangazo nchi nzima ikiwemo kuweka mazingira ya rushwa.