Bonnah kuja na mashindano ya soka kwa watu wenye ulemavu

Mtanzania
Published: Nov 29, 2022 19:02:36 EAT   |  Sports

Na Norah Damian, Mtanzania Digital Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, anatarajia kuandaa mashindano ya soka yatakayohusisha watu wenye ulemavu kwa lengo la kutafuta na kukuza vipaji mbalimbali kwa jamii hiyo. Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka ujao baada ya kumalizika mashindano yaliyoandaliwa na mbunge huyo yanayohusisha watu wasio na ulemavu. Akizungumza na […]

Na Norah Damian, Mtanzania Digital

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, anatarajia kuandaa mashindano ya soka yatakayohusisha watu wenye ulemavu kwa lengo la kutafuta na kukuza vipaji mbalimbali kwa jamii hiyo.

Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka ujao baada ya kumalizika mashindano yaliyoandaliwa na mbunge huyo yanayohusisha watu wasio na ulemavu.

Akizungumza na Mtanzania Digital, Bonnah amesema amekuwa na programu mbalimbali za kusaidia watu wenye ulemavu lakini hakuwahi kuandaa mashindano ya aina hiyo.

“Natambua kwenye jimbo langu wako watu wenye ulemavu na tumekuwa na programu mbalimbali za kuwasaidia, wako ambao tumewagusa mmoja mmoja, kwenye vikundi na hata kupitia mfuko wa jimbo, kwa sababu binadamu wote ni sawa.

“Naamini kupitia mashindano tutakayoyaandaa tutaibua na kukuza vipaji vya ndugu zetu wenye ulemavu, tunatambua michezo ni afya na michezo pia ni ajira hivyo, wanaweza kupata fursa mbalimbali,” amesema Bonnah.

Naye Ofisa Elimu Maalumu katika Halamashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Msechu, amesema wanazo programu mbalimbali za kuibua vipaji vya watu wenye ulemavu hivyo, mashindano hayo yakifanyika ni fursa nyingine ya kuibua vipaji.