Ziara Ababu FIFA imetiki

Mwanaspoti
Published: Nov 29, 2022 09:14:53 EAT   |  Sports

KUMBE zile picha zilizokuwa zinazagaa kwenye mtandao wa kijamii zikimuonyesha Waziri wa Michezo, Ababu Namwamba, akiwa na Rais wa FIFA, Gianni Infantino, hazikuwa za PR maze na wala Waziri hakwenda Qatar kushangaa Kombe la Dunia. Mpango mzima ni huu, ahadi aliyotoa Namwamba hatimaye ameitekeleza baada ya jana barua ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) iliyotiwa saini na Katibu Mkuu, Fatma Samoura, ilidhibitisha kuiondoa kibano ambacho Kenya imekuwa ikiitumikia tangu Februari 24 mwaka huu. Hii sasa inamaanisha Kenya ipo huru kushiriki michuano za kimataifa zinazosimamiwa na FIFA pamoja na washirika wake kama vile Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki n Kati (CECAFA). Katika barua ambayo FIFA imemuandikia Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu, Barry Otieno, tarehe ikiwa ni Novemba 28 mwaka huu, ilisema Baraza la FIFA ilipewa taarifa ya hali ilivyo FKF Novemba 25 mwaka huu ili watoe uamuzi. Awali Barry alikuwa ameandikia FIFA Novemba 4 mwaka huu akidhibitisha Serikali ya Kenya ikiwakilishwa na Waziri mpya wa Michezo Namwamba ilirudisha uongozini Kamati Utendaji FKF na kuzifungulia ofisi za shirikisho hilo. “Ujumbe kutoka FIFA-CAF utatumwa Nairobi kueleza hatua ambazo FKF zitafuata na pia kukutana na Waziri Mteule wa Michezo,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo ya Fatma.