Yacouba: Nimetoka Yanga ila sitaisahau

Mwanaspoti
Published: Feb 01, 2023 12:10:43 EAT   |  Sports

ULIPOFUNGWA usajili wa dirisha dogo moja ya majina makubwa lililoshtua lilipotajwa kutua Ihefu ni mshambuliaji Yacouba Songne, raia wa Burkina Faso. Yacouba alifikia uamuzi huo baada ya kuachwa na Yanga katika dakika za mwisho kufuatia klabu hiyo kukosa nafasi katika wachezaji ambao waliwasajili msimu huu kisha jamaa kudakwa na matajiri wa Mbarali kule Mbeya. Baada ya usajili huo Mwanaspoti lilimtafuta Yacouba na kupiga naye stori tukianza na maisha yake Yanga yalivyokuwa na kutua kwake Ihefu. MAISHA YANGA Yacouba anaeleza jinsi alivyoanza mwaka wa kwanza ndani ya Yanga kabla ya kuingia katika changamoto ya majeraha ule mwaka wa pili wa maisha yake ndani ya timu hiyo. “Mwaka wa kwanza nilianza vizuri, ingawa tulikuwa na timu inayoanza kujengeka lakini tulipambana kulinda hadhi ya klabu kubwa kama Yanga. Nafikiri nilikuwa mfungaji bora katika msimu huo kwa klabu ingawa hatukupata mafanikio makubwa kama ambavyo tulijipangia kabla kwa malengo yetu,” anaeleza Yacouba. “Mwaka wa pili nao tulianza vizuri timu ikiwa imeongezewa watu wengine bora ambao walitukuta, lakini bahati mbaya sana nikaumia na ndipo kila kitu kiliishia hapo na kuanza kujiuguza. “Kitu ambacho namshukuru Mungu ni jinsi klabu ilivyochukua hatua za kunitibia majeraha yangu na kupona kabisa na sasa niko tayari kuichezea klabu yoyote na kuendelea na maisha yangu kama ilivyokuwa kabla. “Hakuna mchezaji anayependa kupata majeraha makubwa kama ambavyo mimi niliumia goti. Unafika salama, lakini baadaye unapata tukio la namna ile kiukweli liliniumiza sana lakini kila kitu kinapangwa na Mungu ndiyo maana sasa nimerudi katika afya yangu na kuendelea na kazi. “Ukiacha viongozi wa Yanga hasa rais wa klabu Hersi (Said) na mfadhili GSM (Ghalib Said) ambao walihakikisha napona, lakini pia niwashukuru kocha Nabi (Nasreddine) na daktari Yousef (Mohamed) ambao ndio walikuwa na mawasiliano na kumtafuta daktari yule bingwa wa kule Tunisia ambaye alinitibu na kupona, ila mwisho kabisa nimshukuru kocha wa mazoezi ya viungo Helmy (Gueldich) kwa kazi kubwa ya kunirudisha katika ubora kupitia mazoezi yake. Alinihudumia hata nje ya muda wake wa kazi ili anione narejea.” MAISHA YALIBADILIKA KIFEDHA Nyota huyo baada ya tukio hilo matarajio yake ya kiuchumi pia yaliathirika, akisema: “Kiukweli niliumia wakati mbaya mkataba wangu ulikuwa unaelekea mwisho, lakini naishukuru klabu kwa kunitunza kwa matibabu lakini pia maisha yangu kifedha yalibadilika kwa kuwa sikuwa na mkataba. Kwa hiyo sikuwa nalipwa kama mshahara, walikuwa wananikumbuka wakati mambo yalipokuwa sawa na kuna wakati nakosa, maisha yalikuwa hivyo lakini kitu nachoshukuru ni kutibiwa na sasa nimerudi uwanjani maisha yataendelea,” anasema. AAMBIWA HAKUNA MKATABA Kuna nyakati ngumu ambazo humpata mtu na hasa kama ametoke kujiuguza. “Nakumbuka niliitwa ofisi ya mtendaji mkuu (wa klabu, Andre Mtine) tulikaa naye na akaniambia klabu ilikuwa inanihitaji, lakini kwa sasa wasingeweza kunisajili kutokana na ufinyu wa nafasi za wachezaji wa kigeni. Aliniambia kuna wachezaji wanaletwa na nafasi yangu haitaweza kupatikana. “Ile taarifa iliniumiza sana kwa sura mbili. Kwanza nilishajipanga vizuri kuja kuisaidia zaidi Yanga kwa kuwa awali sikumalizia mkataba wangu wa kwanza vizuri, lakini pili niliwahi kuongea na kocha (Nabi) akaniambia ananihitaji ila uamuzi ulikuja wakati ambao si mzuri dirisha likikaribia kufungwa,” anasema. “Niliwaza nitapataje timu haraka ukizingatia nilikuwa nje bila kucheza muda mrefu. Hilo ndilo lilinisumbua. Kama wangefanya uamuzi wao ndani ya muda mzuri kwangu nisingeumia kama ambavyo ilitokea. Hilo sikulifurahia sana, lakini ndio maisha.” YANGA ANAYOIACHA Mchezaji huyo licha ya kuondoka Jangwani lakini ana jambo lake kwa waajiri hao wa zamani. “Yanga ni timu nzuri na imesajili vizuri. Nadhani wataendelea kupata mafanikio zaidi. Nadhani kuanzia mwezi Februari watakuwa na majukumu mengi hasa kutokana na mechi za CAF. Kama makocha hawatafanya mzunguko mzuri wa wachezaji kucheza wanaweza kupata majeruhi wengi lakini nawaamini makocha waliopo wanalijua hilo,” anasema. MAYELE KUWABEBA JANGWANI Moto wa straika wa Yanga, Fiston Mayele unamkosha kila mtu na Yacouba anasema: “Kitu nachofurahia nikiwaona washambuliaji wa Yanga ni kwamba ni wazuri. Jambo bora kuliko yote eneo hilo ni uwepo wa mshambuliaji ambaye ni ngumu kupitisha mechi mbili bila kufunga Fiston (Mayele). Huyu ni roho ya Yanga katika timu yao hasa safu yao ya ushambuliaji. “Mayele ataibeba pia Yanga kwenye mechi za hatua ya makundi kitu ambacho wanatakiwa kufanya ni kushinda mechi tatu za nyumbani na timu ya kupata matokeo hayo wanayo itategemea mipango ya kiuongozi na maandalizi ya makocha. Viongozi wa Yanga wanatakiwa kumsikiliza kocha kwa kuwa makocha wanajua pia nini kifanyike ili kushinda kwa kuwa wao wanaishi na wachezaji kila siku.” ANAIONAJE LIGI BARA? Licha ya kucheza Ligi Kuu Bara kwa muda mfupi akiwa Yanga, nyota huyu anasema imekamilika na ina ushindani mkubwa. “Ligi ya hapa inapanda. Ni ligi ngumu ambayo ina wachezaji wengi wa kimataifa wakitoka mataifa mbalimbali. Ukiangalia ligi ya hapa ukilinganisha na Ghana au Ivory Coast utaona hapa ni kubwa na ngumu. Jambo zuri zaidi mashabiki hapa wanapenda mpira na klabu zao,” anasema Hata hivyo, pamoja na hayo, soka la Tanzania lina presha na linawalazimu wachezaji kujipanga kwelikweli. “Kitu ambacho huwa kinawaumiza wachezaji ni presha kubwa ya mashabiki. Nimecheza Yanga, lakini mashabiki wao wanataka kuona timu inashinda kila mchezo. Hawajui timu kufungwa wala mchezaji kukosea, wanakuwa wakali na kusahau haraka mazuri uliyofanya. Hapa kama akija mchezaji mwenye roho rahisi anaweza kukimbia, lakini kitu bora ni pale wakishinda nao wanafurahi na kusahau yote. “Mashabiki wa Yanga mbali na yote nawapenda sana ni watu wakarimu kama ambavyo nilisema awali hasa ukiwa unafanya kazi vizuri. Sikuwahi kugombana nao wala kuwachukia. Nilipokuwa nacheza walikuwa na mimi na hata nilipoumia walikuwa karibu nami, wananitumia ujumbe kuna baadhi walisikia naondoka walionyesha kuumia sana lakini niwaambie maisha kuna wakati mtatakiwa kuachana kama hivi huwezi jua kesho kipi kitatokea.” AZIZ KI MBONA MTAMWELEWA Yacouba na nyota mpya wa Yanga, Aziz KI wanatoka nchi moja na Yacouba anamjua vilivyo kiungo huyo wa Yanga. “Aziz KI ni mchezaji mpya ambaye kaja Tanzania amekutana na soka la aina tofauti anahitaji kuzoea mazingira kidogo. Nilikwambia ligi ya hapa ni ngumu kuliko maeneo mengi niliyowahi kupita. Anahitaji kuzoeana na wenzake ili ajue jinsi ya kucheza nao kwa ushirikiano,” anasema. “Namuona anaendelea vizuri lakini bado sijamuona Aziz KI ninayemjua na naamini kama wakimpa muda zaidi kujuana na wenzake zaidi watu watafurahia sana kumuona. Ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa. Sisemi haya kwa kuwa labda natoka naye taifa moja hapana, huyu ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa. YANGA NI BINGWA Akizungumzia uwezekano wa timu ipi itaweza kuchukua ubingwa Yacouba anasema ingawa ligi ni ngumu kuamua moja kwa moja nani anaweza kuwa bingwa, lakini anaipa nafasi kubwa Yanga. “Ukitazama ligi kuna mechi nyingi lolote linaweza kutokea. Timu inayoongoza imeizidi ya pili kwa pointi sita, hiyo ni sawa na timu inayoongoza ipoteze mechi mbili lakini binafsi naiona Yanga itachukua tena ubingwa sababu zangu ni mbili kwanza wameizidi Simba kwa pointi sita lakini kubwa zaidi ni ubora wa kikosi na makocha wao,” anasema. AWAGUSIA KANOUTE NA OKRAH Kama ulikuwa hujui Yacouba aliwahi kucheza na viungo wawili wa Simba, Sadio Kanoute na Agustine Okrah na hapa anazungumzia viwango vyao vya sasa ndani ya Wekundu hao. “Kanoute namjua sana ni rafiki yangu. Niliwahi kucheza naye hata Okrah. Kanoute bado yuko kwenye ubora ninavyomuona anavyocheza akiwa na Simba. Ni kiungo mpiganaji hasa. Kwa Okrah alianza vyema kama ambavyo namjua lakini hapa kati nimeona ameshuka sijajua kuna matatizo gani yamemkumba.” OKRAH ANA MKWANJA MREFU Yacouba anafichua kwamba katika kikosi cha Simba cha sasa Okrah anaweza kuwa mchezaji namba moja kwa mkwanja mrefu au wa pili. “Okrah ana pesa sana sio mchezaji ambaye anaanza kuzitafuta sasa. Alishacheza soka sehemu mbalimbali nadhani fedha nyingi alizipata alipokuwa Sudan. Kule alikuwa mchezaji anayelipwa sana kwa hiyo ukiacha fedha anazopata sasa ni kama zinakwenda kumuongezea tu. KWANINI IHEFU? Yacouba pia alizungumzia sababu zake za kutua Ihefu badala ya timu nyingine nchini. “Niliamua kwenda Ihefu kutokana na heshima ambayo viongozi walinipa waliposikia Yanga wameniacha. Nafikiri kidogo ofa yao ilikuwa na utofauti na timu zingine ambazo zilinihitaji, haikuwa kubwa lakini pia heshima ambayo walinipa,” anasema. “Jambo lingine ni heshima ambayo kocha (Zuberi Katwila) alinipa mara baada ya kufika. Alinipokea kama mchezaji mkubwa, tuliongea na aliniambia anachotaka kutoka kwangu hii ilikuwa kubwa zaidi. “Uwepo wa wachezaji wengi wa kigeni pia niliamini haitakuwa kitu kigumu kwangu kuweza kuishi hapo. Nachotaka ni kupata muda wa kutosha wa kucheza ndio maana nimesaini mkataba mfupi kwa kuwa nina malengo makubwa.” IHEFU HAISHUKI Yacouba anasema licha ya timu hiyo kupambana kutoshuka daraja, anadai hilo la kushuka halitawezekana kwao na itabaki Ligi Kuu.