Wadau wakubali... Simba, Yanga ni bab'kubwa!

Mwanaspoti
Published: Mar 24, 2023 12:52:50 EAT   |  Sports

ZIMETUHESHIMISHA. Ni baadhi ya kauli za wadau wa soka nchini walioshiriki mjadala maalumu kutokana na Simba na Yanga kutinga robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, huku ikielezwa zimebebwa kiuchumi kulinganisha na miaka ya nyuma. Mjadala huo wa Twitter Space uliandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) na ulianza kati ya saa 2:00-4:00 usiku ukihusisha wadau mbalimbali, akiwamo viongozi wa klabu hizo, huku wachangiaji wakuu wakiwa Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, maofisa habari wa Simba na Yanga, Ahmed Ally na Ally Kamwe na wa Bodi ya Ligi (TPLB), Karim Boimanda. Wengine walioshiriki ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka (TFF), Angetile Osiah na Mwandishi Mwandamizi wa magazeti yanayozalishwa na MCL, Charles Abel sambamba na wadau wengine waliokuwa wasikilizaji wa mjadala huo uliosisimua. Akichangia mjadala huo, Arafat alisema kukua kiuchumi kwa klabu za Simba na Yanga ni sababu kubwa iliyozibeba timu hiyo kufika hatua hiyo na kuna maana kwenye soka la Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki. Arafat alifungua mjadala huo kwa nondo zake akianza kwa kuipongeza MCL kwa kuandaa jukwaa hilo lililowakutanisha wadau wa Simba na Yanga kisha kuweka mawazo yao pamoja kwa ajili ya maendeleo ya soka la Tanzania. "Ligi yetu imekuwa kwa hatua ambayo timu zetu zimefika, tunao wadau wengi nje ya Afrika wanafuatilia timu zetu hizi, chagizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kutoa zawadi ya Sh 5 milioni kwa kila bao nalo limekuwa chachu na kufanikiwa," alisema Arafat na kuongeza; "Mafanikio haya maana yake ni nini? Simba na Yanga kuingia robo fainali imeihakikishia nchi nafasi ya kuingiza timu nne kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao, kama tunapata nafasi hizi natamani kuona timu zote nne ziingie makundi na hata kutinga hatua ya robo fainali na isiwe kwa Simba na Yanga." KILICHOZIBEBA Makamu huyo wa Rais wa Yanga, anaendelea kuongea kwa kusema; "Nini kimezibeba Simba na Yanga, wadau wamekuwa na mchango kwa maana ya kuingia kama wabia, tumeona Yanga wameenda kwa Sportpesa na Simba kwa M-Bet huku wakiwemo wengine." "Hii ni faida ambayo naamini imechangia kwa timu hizi kufika mbali, mpira wa Afrika kuendesha ni gharama kubwa sana, ili uendelee kuwa imara inahitaji kuwa sawa kiuchumi...Timu zetu zimeenda mbali kwa kuwa na mabenchi mapana kwa kuwa na kila mtu na eneo lake tofauti na zamani ambapo mtu mmoja alikuwa akifanya vitu vingi," alisema Arafat na kuongeza; "Zamani tulikuwa tukiona DR Congo ikifanya vizuri lakini kwa sasa imekuwa tofauti inamaana ya kuwa nguvu ya timu zetu kiuchumi zimekua." LIGI KUWA MAARUFU Kitendo cha klabu za Simba na Yanga kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa kimeelezwa kuwa kinaongeza umaarufu wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Hilo limeelezwa na Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi, Boimanda wakati akichangia mjadala huo,"Tumekuwa tukikusanya watu wengi viwanjani lakini hawasikilizani lakini hapa watu wanasikilizana kwa hiyo niwapongeze sana. Timu zinapofuzu kwenda robo kwanza tunaongeza umaarufu wa ligi yetu, inavutia madhamini kutoka ndani na nje ya nchi, wadhamini wanaleta fedha ambazo zinasaidia timu kuwa sawa kiasi cha kuweza kusajili wachezaji bora kutoka ndani na nje ya nchi," alisema "Baada ya klabu kupata nguvu zinaenda kufanya vizuri kwenye mashindano, klabu ikiwa sawa ndio inapata nguvu pia ya hata kuendesha soka la vijana," aliongeza Boimanda. Boimanda anatamani kuona timu za Ligi Kuu Bara zikiendelea kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa ili kuendelea kuipa umaarufu ligi ya ndani. ZISHIKILIE BOMBA Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally, alisema itakuwa na maana kubwa sana kwa nchi kama klabu za Tanzania zikiwemo Simba na Yanga zitaendelea kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa. Ahmed ambaye alikuwa mmoja kati ya wachangiaji kwa upande wa Simba. "Mpira wa nchi hii umepiga hatua kubwa kwa timu za Simba na Yanga kufuzu robo fainali kwa mara ya kwanza zikiwa pamoja, pia kuna nchi utaona ina timu moja tu kwenye hii hatua sasa hili ni jukumu letu kubwa la kuhakikisha tunaendelea kushikilia hapa tulipo," alisema Ahmed na kuongeza; "Hii ina maana kuna kazi kubwa imefanyika kuanzia kwenye klabu, wasimamizi na serikali ingekuwa timu moja pekee, tungesema ni juhudi za Simba pekee mathalani zipo timu mbili basi kuna nguvu kubwa, kwenye 50 akifaulu mmoja ni juhudi za mtu binafsi wakifaulu zaidi lazima useme kuhusu mwalimu." "Robo fainali mbili ni ishara tosha kuwa mpira wetu unapiga hatua huku tukiangalia changamoto zilizopo ili kutatua, niwapongeze Yanga kwa uimara, waliamini mafanikio ni kuifunga Simba lakini kwa sasa wameonyesha walilala kwa miaka mingi na sasa wameamka," alisema Ahmed. MAFANIKIO YA BODI Naye Angetile, mmoja ya waandishi na wahariri wazoefu nchini na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa TFF enzi za utawala wa Rais Leodegar Tenga kwa upande wake alisema; "Kitendo cha Simba na Yanga kuingia hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika ni mafanikio makubwa kwa upande wa Bodi ya Ligi (TPLB), kutokana na wao kuitangaza vyema ligi yetu." "Mafanikio ya Simba na Yanga kimataifa yana maana kubwa kwenye ranking (viwango) lakini haina maana kwa timu zetu za taifa kwa sababu hata wachezaji wengi wanaofanya vizuri ni wa nje kuliko wa hapa kwetu." FURSA KWA WAZAWA Mwandishi Mwandamizi na mchambuzi wa soka wa gazeti hili, Charles Abel naye alichangia kwa kusema kitendo cha timu za Simba na Yanga kufuzu hatua ya robo fainali za mashindano ya Afrika kuna faida kubwa kwa sababu inatoa fursa kwa wachezaji wengi wazawa kuonekana kimataifa. "Wachezaji wetu wanakutana na watu tofauti ambao mataifa yao yameendelea, hivyo kuwaongezea ujuzi na hata pia kwa makocha wa timu hizo kwa maana wanapata mbinu mbalimbali za kiufundi," alisema Abel. Simba iliyotinga hatua ya robo kwa mara ya tatu katika misimu mitano ya Ligi ya Mabingwa ilikuwa Kundi C imefikisha pointi tisa baada ya mechi tano na itakamilisha ratiba kwa kuifuata Raja Casablanca ya Morocco inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi 13. Mechi hiyo itapigwa Aprili Mosi jijini Casablanca. Kwa upande wa Yanga wao ndio vinara wa Kundi D wa Kombe la Shirikisho ikiwa na pointi 10 kama US Monastir ya Tunisia ili zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa na itamalizia mechi ugenini kwa kuifuata TP Mazembe ya DR Congo mechi itakayopigwa Aprili 2, jijini Lubumbashi.