SPOTI DOKTA: Theluji inavyoweza kuathiri kiwango cha soka

Mwanaspoti
Published: Mar 24, 2023 12:40:31 EAT   |  Sports

KATIKA mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa kati klabu ya Yanga na US Monastir ya Tunisia mvua ilinyesha kuanzia alfajiri hadi mchana. Mechi hiyo ilichezwa mvua ikiwa imekata ilisababisha sehemu chache za uwanja kuwa na vijidimbwi vilivyopunguza kasi ya mpira na huku wachezaji wakitumia nguvu kuukwamua mpira uliokwama. Wakati hapa Bongo hali ya mvua isiyo na baridi ikitokea kule nchini Uingereza katika ligi ya EPL ilishuhudiwa mvua iliyoambatana na theluji ikiendelea kudondoka ikiwamo katika baadhi ya nchi zingine za Ulaya. Katika mchezo mkali wa robo fainali ligi ya Europa kati ya Arsenal dhidi ya Sporting Lisbon uliochezwa Alhamisi iliyopita jijini London dimba la Emirates iliwalazimu watazamaji kuachia siti kutokana na maji ya mvua yakiwa na theluji kuwamwagikia kutoka juu ya paa la uwanja. Maji ya mvua iliyonyesha Bongo yako tofauti katika jotoridi kwani yale ya mvua ya Uingereza ambayo ilikuwa inamwagika na theluji yenye jotoridi la sentigrade chini ya -1. Hapo unapata picha namna wachezaji wa Ulaya walivyokutana na hali ngumu ya hewa hewa ukilinganisha na wale wa mechi ya Yanga na ambao kipindi mechi inaanza mvua tayari imekata. Yanga alishinda 2-1 katika mazingira ya mvua ya baridi ya kawaida wakati kule Ulaya Arsenal akatolewa kwa mikwaju ya penati 5-4 ya penati kwenye mvua theluji yenye baridi kali. Utabiri wa hali ya hewa wiki hii baadhi ya mechi za soka hapa bongo zikachezwa na mvua na kule Ulaya mvua yenye theluji au theluji pekee. Ulaya majira ya baridi kali ikiwa na theluji huanzia mwezi Desemba na kuendelea katika miezi ya Januari mpaka Aprili mwaka unaofuata. Enzi za Arsene Wenger Arsenal iliwahi kuonekana wachovu kipindi cha majira ya baridi hatimaye kupoteza michezo yake kirahisi pamoja ya kuwa walikuwa na mastaa wakali. Hata hivyo hali hiyo iliendelea kuwepo hata katika mchezo wao ligi wa siku ya jumapili walioshinda 4-1 Crystal Palace lakini angalau hali hiyo haikuwa kama ya siku ya alhamisi katika ligi ya Europa. Je kuna ukweli wowote wa hali kama ya baridi kali kuwa kikwazo cha mchezaji kucheza kwa kiwango? Hebu leo tupate ufahamu wa jambo hili. BARIDI KALI INAATHIRI KIWANGO KAMA HIVI Joto la kawaida la mwili wa mwanadamu huwa ni nyuzi joto 36.9 C ambalo halitakiwi kushuka sana wala kupanda sana hivyo mwili hujilinda jambo hili lisitokee. Udhibiti wa joto la mwili katika mazingira ya baridi kali ni jambo ambalo linaweza kuleta athari katika kiwango cha mchezaji anayecheza katika mazingira hayo. Katika mazingira ya joto au baridi mwili hujaribu kulinda mazingira ya ndani ya mwili yawe sawa katika kiwango chake inachohitajika kwa ajili ya shughuli zake. Katika kipindi cha baridi mwili hulazimika kujibadili kiutendaji katika kazi za mwili ikiwamo kutetemeka ili kuupasha mwili moto. Kwa kawaida misuli hai ya mwanasoka huwa na uhitaji wa damu kwa wingi ili kuweza kucheza kwa kiwango, lakini katika baridi utiririkaji wa damu huwa ni tofauti. Wakati wa baridi damu hupungua kutiririka juu ya ngozi kwa sababu Mishipa ya damu iliyopo juu ya ngozi husinyaa na kujificha ndani ya ngozi lengo ni kulinda joto la ndani ya mwili lisishuke. Hali ya damu kupungua kutirika katoka katika ngozi na kuelekea kwa wingi ndani ya mwili ni jambo muhimu kufanyika pale kunapokuwa na ongezeko la uhitaji wa nguvu. Mwili hufanya hivi ili kujaribu kuendelea kulinda joto la mwili na wakati huo huo kutengeneza nguvu zaidi itakayotumika na misuli kwa ajili ya mazoezi au kucheza. Shuguli zingine za mwilini za kuufanya mwili kuwa na maji mengi huathirika wakati wa ikiwamo upoteaji wa maji kwa jasho hupungua na huku upoteaji wa maji kwa njia ya kupumua hewa huongezeka Wanasoka wanakuwa katika hatari ya upungufu wa maji mwilini kwani kiu huwa inapotea katika mazingira ya baridi. Hivyo kuwafanya kutokunywa maji yakutosha wakati wanapoteza maji mwilini kwa njia ya kupumua kuliko kutoka jasho. Maji ni kitu muhimu kwa mwili katika kudhibiti mazingira ya ndani, upungufu wa maji ni kihatarishi cha kupoteza joto la ndani ya mwili katika mazingira ya baridi. Mwili unapokuwa na maji ya kutosha husaidia ujazo wa damu mzungukoni kuwa mzuri. Hata ukitoka jasho na kupoteza joto bado mwili huweza kulinda kiwango cha utendaji wa misuli ya mwili. Lakini hali hii inakuwa tofauti kucheza katika baridi kali kwani mwili unakuwa katika mazingira ambayo hupata shinikizo kubwa na kuathirika katika njia nyingi. Kiujumla misuli iliyopata baridi huwa ni dhaifu kiutendaji, utendaji katika miitikio ya kimwili huwa ni ya taratibu na dhaifu. Mipitisho ya fahamu inayotumwa na mishipa ya fahamu kwenda katika ubongo kupata tafsiri, kutolewa maamuzi na kurudishwa na maelekezo katika maeneo ya mwili huwa ni taratibu. Hali hii inapokuwepo ina maana maamuzi ya kimwili yanakuwa ya taratibu katika baridi. Katika baridi Misuli ya mwili inakuwa mkakamao, inashindwa kunyumbulika kwa wepesi na kufanya vitendo kwa haraka na kwa wakati. Inapotokea misuli ya mwili haipati damu na virutubisho kwa wingi na kwa haraka na kwa wakati husababisha kukosa nguvu zakutosha kutenda mambo mbalimbali kwa ufanisi. Mfano wa matendo hayo ni kama vile kujikunja na kukunjua kwa misuli ili kuweza kukimbia, kutembea, kupiga mpira au kuruka. Vile vile misuli iliyo na baridi na mkazo huwa haifanyi kazi kwa kiwango, hali hii ndiyo inayochangia kupata majeraha kirahisi ukilinganisha na misuli iliyopo katika mazingira ya joto. Kiwango cha mchezaji huathirika na kushuka kiutendaji kutokana pia mwili kufanya kazi kubwa na kutumia nguvu nyingi katika shughuli za ndani na huku moyo hufanya kazi ya ziada katika mazingira ya baridi. Mwili huweza kujibadili haraka na kukabiliana na mazingira magumu ya joto kali, lakini kujibadili katika mazingira magumu ya baridi kali huwa ni taratibu sana na dhaifu. CHUKUA HII Ni dhahiri mchezaji kucheza katika mvua inayoambatana na theluji yenye baridi kali inaweza kuathiri afya ya mchezaji na kiwango cha chake. Wakati wa baridi kali au theluji wachezaji waliopo benchi wajifunike na mablanketi na makoti ili wanapoingia misuli yao iwe imechangamka tayari na huku pia kupasha mwili moto na mazoezi lainishi ya viungo. Bongo soka na mvua, ulaya soka na theluji. Ukiona mwanasoka ana upiga mwingi katika mazingira ya baridi kali ujue ana utimamu wa nguvu kustahimili baridi kali.