Singida BS yasuka mbinu kuiua Simba

Mwanaspoti
Published: Feb 01, 2023 15:42:36 EAT   |  Sports

MASTAA wa SINGIDA Big Stars wametumia saa mbili kujifua tayari kwa ajili ya kuikabili Simba Ijumaa hii kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao dakika 90 zitaamua ubora wa timu zote mbili. Mchezo wa kwanza Singida BS ikiwa nyumbani ililazimishwa sare ya bao 1-1 mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida. Timu hiyo ikiwa chini ya kocha mkuu, Hans Van Pluijm ilianza mazoezi saa 3:15 asubuhi wakianza na kupasha viungo huku wakigawanyika kwa nafasi za viungo, mabeki na makipa. Baada ya mazoezi ya kupasha mwili misuli Hans aligawa timu mbili akitumia zaidi mawinga kutengeneza nafasi za kufunga zoezi ambalo lilitumia nusu saa na kupumzisha wachezaji kupata nafasi ya kunywa maji. Mastaa hao walirudi tena kuendelea na zoezi la kutengeneza mabao zaidi kwa kupitia mawinga na mabeki wa pembeni ambao walikuwa wanapanda na kushuka. Safu ya ushambuliaji upande mmoja ilikuwa na Amis Tambwe, Meddie Kagere, Ibrahim Ajib na Francy Kazad ambao walionekana kutumia maarifa zaidi kwa kucheza mipira ya kupasiana pasi fupifupi na kufunga. Huku upande wa pili kukiwa na Bruno Gomes, Nicholas Gyan, Saadun, Nickson Kibabage ambao walikuwa wanatumia mfumo wa kupiga krosi za juu washambuliaji wafunge kwa vichwa. Baada ya saa moja kukamilika walijumuika pamoja na kunyoosha misuli ya viungo na kufanya sala ya pamoja kwaajili ya kumaliza jukumu na kumsikiliza kocha ambaye alitumia robo saa kuzungumza nao