Singida Big Stars sasa ruksa kusajili

Mwanaspoti
Published: Nov 29, 2022 17:17:14 EAT   |  Sports

KAMATI ya Sheria na hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania (TFF) imeiondolea klabu ya Singida Big Stars (SBS) adhabu ya kufungiwa kusajili. Uamuzi huo umefanywa leo na kamati hiyo baada ya kupitia hoja za timu hiyo katika maombi yao ya marejeo (review) kuhusu uamuzi wa awali wa kufungiwa kusajili. Ikumbukwe kuwa Oktoba 7, 2022 kamati hiyo ya TFF iliifungia Singida Big Stars na Tanzania Prisons kusajili kwa dirisha moja la usajili baada ya kufanya kosa la kusajili wachezaji wenye mikataba na klabu zingine. Ambapo Singida Big Stars ilimsajili Kipa Metacha Mnata huku akiwa na mkataba na klabu ya Polisi Tanzania huku Prisons ikimsajili kipa Mussa Mbisa aliyekuwa na mkataba na Coastal Union ya Tanga. Badala ya kuondolewa kifungo hicho, Singida Big Stars imepigwa faini ya Sh 1 milioni ambayo inatakiwa kulipwa kabla ya dirisha dogo la usajili linalofunguliwa Desemba 15. Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari ambayo imetolewa leo Novemba 29, 2022, kamati hiyo imesema iwapo Singida Big Stars haitalipa faini hiyo ndani ya muda uliowekwa, adhabu ya kufungiwa kusajili itabaki palepale.