Simba Queens yatibua jambo Nyamagana, Shikangwa atupia manne

Mwanaspoti
Published: Feb 01, 2023 16:15:35 EAT   |  Sports

Mwanza. MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, Simba Queens imeibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Alliance Girls leo katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza mchezo ambao umepigwa kuanzia saa 10 jioni. Ushindi huo ni wa sita mfululizo kwa Simba Queens katika michezo saba ya ligi tangu ilipopoteza kwa mabao 2-1 mbele ya JKT Queens katika mchezo wake wa kwanza msimu huu, huku ikiwa ni dozi ya pili mfululizo nzito kwa timu hiyo kuigawa baada ya kuichapa Amani Queens mabao 7-0 mchezo uliopita. Mabao yote ya Simba Queens yamefungwa na mshambuliaji, Jentrix Shikangwa raia wa Kenya akifunga katika dakika ya sita, 23, 42 na 65, ambapo amefikisha mabao sita katika mechi saba alizocheza huku akifunga mfululizo baada ya mchezo uliopita kutupia mawili dhidi ya Amani Queens. Shikangwa ni mchezaji wa pili msimu huuu kufunga mabao matatu katika mchezo mmoja (Hattrick), akitanguliwa na straika wa Alliance Girls, Winfrida Charles aliyefunga dhidi ya Mkwawa Queens, huku Hattrick zote zikipatikana katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza. Baada ya kichapo hicho, Alliance Girls imetibuliwa rekodi yake ya kutopoteza mechi msimu huu ama kuruhusu bao katika uwanja wake wa nyumbani, Nyamagana. Simba Queens imepaa hadi nafasi ya kwanza kwa kufikisha pointi 16 huku Alliance ikisalia nafasi ya tano na pointi zao 10. Katika mchezo huo, nyota mpya wa Simba, Asha Rashid ‘Mwalala’ aliyesajiliwa dirisha dogo amecheza mchezo wake wa kwanza akiingia kipindi cha pili mnamo dakika ya 77 akichukua nafasi ya Mwanahamisi Omari. Michezo mingine ya ligi hiyo raundi ya saba imepigwa katika viwanja mbalimbali, ambapo vinara JKT Queens wamelazimishwa suluhu na Yanga Princess (0-0), Baobab Queens imeshinda mabao 3-0 ugenini mbele ya Mkwawa Queens, Fountain Gate Princess imebanwa mbavu na Ceassia Queens na kutoka suluhu (0-0) na Tigers Queens imepata ushindi wa kwanza wa mabao 3-0 dhidi ya Amani Queens.