Simba kubeba kiungo Geita Gold

Mwanaspoti
Published: Nov 30, 2022 08:30:15 EAT   |  Sports

DIRISHA dogo la usajili litafunguliwa Disemba 15 mwaka huu huku timu mbalimbali zikijipanga kufanya maboresho kwenye vikosi vyao hasa baada ya kuona matokeo ya mechi zao kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara. Hata hivyo, miongoni mwa timu ambazo zinaweza kufanya usajili mkubwa ni Simba kutokana na namna inavyoonekana kushindwa kuwa na matokeo mazuri mfululizo na tayari imeanza kupiga hesabu kali za kunasa baadhi ya wachezaji nyota wakianza na wazawa. Kutokana na mahitaji na mapendekezo ya benchi la ufundi Simba ikishirikiana na uongozi wa timu hiyo watasajili si chini ya wachezaji wanne, nafasi ya straika ambao huenda wakawa wawili, kiungo wa ukabaji na beki mwenye uwezo wa kucheza kushoto na kulia. Taarifa kutoka kwenye vikao vya ndani vya Simba, zinaeleza kuwa mabosi wa Simba wametua Geita Gold kwa kiungo wa ukabaji, Kelvin Nashon anayeonekana kufanya kazi nzuri kwenye kikosi hicho tangu msimu uliopita ikimsajili kutoka JKT Tanzania. Baadhi ya mabosi wa Simba wanaoingia kwenye vikao hivyo vya usajili vilivyokuwa na usiri mkubwa ndani yake inaelezwa wamekuwa wakimjadili, Nashon katika nyakati tofauti kama watakubaliana kumfuata na kuongea nae huenda akawa mchezaji mzawa atakayesajiliwa na mzunguko wa pili akajiunga na kikosi hicho. Simba inahitaji kiungo mkabaji mwingine na atasajili kwenye dirisha dogo kutokana na Mzamiri Yassin na Sadio Kanoute kucheza mara kwa mara. Hata hivyo Mzamiru na Kanoute wameonekana kuwa kwenye ubora utakaompa wakati mgumu Nashon kuaminika kikosi cha kwanza. Wachezaji wanaocheza kama mbadala ni Jonas Mkude aliyepoteza nafasi kikosi cha kwanza, Erasto Nyoni anayeishia benchi mara kwa mara na Victor Akpan aliyesajiliwa msimu huu na ameshindwa kuonyesha makali yake kama ilivyokuwa msimu uliopita wakati anacheza Coastal Union hadi kuwavutia Simba na kumsajili. Simba kama ikikubaliana kumsajili Nashon kama mawazo yao yalivyo inamuona kama mbadala sahihi wa Mzamiru na Kanoute kutokana na umri wake kuwa mdogo na kiwango chake kuwa bora kwa sasa kwenye michezo wa ligi. Wakati huo huo inaelezwa mabosi hao wa Simba wamekuwa wakimjadili kiungo mwingine wa ukabaji, Mudathir Yahya pamoja na Kelvin Kijili wa KMC. Kijili anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaojalidiwa kwenye usajili wa dirisha dogo ili kusaidiana na Shomary Kapombe pamoja na Israel Mwenda ambaye kwasasa ni majeruhi na inasemekana atakuwa nje kwa muda mrefu. Kwa upande wa Mudathir ambaye pia anatajwa kuwaniwa na Singida Big Stars pamoja na kurudi Azam FC kama atatua Simba basi watafaidika naye kwasababu anacheza nafasi mbili kiungo wa chini na juu. Dirisha kubwa la usajili mabosi wa Simba walihitaji huduma ya Mudathir lakini ilishindikana ambapo alidai anahitaji kupumzika baada ya kumaliza mkataba na Azam. Hivi sasa Mudathir anafanya mazoezi na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), KMKM ili kujiweka fiti ambapo amedai amepokea ofa nyingi ila hakuziweka wazi.