Rage: Kwa Yanga hii mjipange

Mwanaspoti
Published: Nov 29, 2022 07:38:01 EAT   |  Sports

MWENYEKITI wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage ametoboa siri ya Yanga kuendeleza rekodi ya kutokufungwa. Yanga juzi ilifikisha michezo 49 ya Ligi Kuu Bara bila ya kufungwa tangu ilipofungwa na Azam FC Aprili 25 mwaka jana jambo ambalo limemfanya kiongozi huyo kueleza kinachowabeba. Rage alisema ni ngumu sana kucheza na Yanga kwa sasa kutokana na morali iliyopo kutoka kwa viongozi, benchi la ufundi na wachezaji wenyewe wanaojitoa. “Wanastahili hiki kinachoendelea kwa sababu wana viongozi wa mpira, umoja baina yao kwa wao kitu ambacho sio rahisi kukiona kwenye klabu nyingine sasa,” alisema Rage na kuongeza; “Unapokosea ndio njia sahihi ya kujirekebisha, Yanga ilipitia misukosuko ila iilichukulia kama fursa ya kuwajenga na kutatua pale walipokosea ndio maana tunaona leo wamefanikiwa.” Kuhusu mbio za ubingwa Rage alisema licha ya kasi ya Yanga ila bado ni mapema kuzungumzia hilo. “Ukiwangaalia na washindani wao unaona wametulia zaidi kwa mfano ukiangalia Simba kitu ambacho kinawaangusha ni majeruhi jambo linaloweza kuwanufanisha Yanga,” alisema. Kitendo cha Yanga kufikisha michezo 49 bila ya kufungwa ni rasmi klabu hiyo imeifikia rekodi ya Arsenal ya England iliyoiweka msimu wa 2003/2004 kuanzia Mei 7, 2003 hadi Oktoba 16, 2004.