Pablo karudi, aeleza sababu kuwa Dar

Mwanaspoti
Published: Nov 29, 2022 07:30:12 EAT   |  Sports

SIMBA juzi Jumapili ilikuwa Kilimanjaro dhidi ya wenyeji wake, Polisi Tanzania lakini habari ikufikie kocha wa zamani, Pablo Franco yuko nchini akitua kimyakimya. Ujio wa Pablo unaleta maswali mengi hasa wakati huu Simba ikitafuta kocha mkuu atakayekuja kuungana na Juma Mgunda ambaye Mwanaspoti linafahamu mzawa huyo mkataba wake unaonyesha atakuwa kwa wekundu hao kama kocha msaidizi. Ingawa Pablo alikuwa mgumu kuthibitisha amekuja nchini kwa hesabu za Simba lakini Mwanaspoti linafahamu kocha huyo amekutana na mmoja wa watu wazito wa wekundu hao kisha wakakubaliana kutatafutana kwa kuzungumza zaidi. Itakumbukwa wakati Pablo akiwa Simba aliiacha timu hiyo kwa heshima akiifikisha hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini ikitolewa na Orlando Pirates kwa matuta. Kwenye hatua hiyo Simba chini ya Pablo mechi ya kwanza ilishinda bao 1-0, lililofungwa na Shomary Kapombena ile ya marudiano Afrika Kusini Orlando ilishinda 1-0, mechi ilikwenda kwenye penalti Simba ilifungwa 4-3. Msimu huo, Pablo alichukua taji la Mapinduzi huku mataji mengine yakichukuliwa na Yanga huku kocha huyo raia wa Hispania akikabiliwa na majeruhi wengi katika kikosi chake. Januari 13, Simba chini ya Pablo ilichukua ubingwa huo baada ya mchezo wa fainali kushinda bao 1-0 dhidi ya Azam, lililofungwa na Meddie Kagere. Akizungumza na Mwanaspoti jana, Pablo alisema amerejea nchini kwa mambo yake binafsi na wala hakuja kwa ajili ya mwaliko wa waajiri wake wa zamani Simba. “Nipo hapa kwa mambo yangu binafsi, sina mwaliko wowote na Simba, siwezi kukwambia ni mambo gani yamenileta hapa nchini, nikimaliza mambo yangu nitakwambia naondoka lini rafiki yangu,” alisema Pablo huku akicheka na kuondoka. Jana kocha huyo alikuwa Mlimani City akiwatazama Yanga wakiumana dhidi ya Mbeya City mabingwa hao wakishinda 2-0 akiwa na mmoja wa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba (jina tunalo) ambaye pia amekuwa akisimamia masuala ya kisheria ya wekundu hao. Mapema Simba ilikuwa katika mazungumzo na makocha mbalimbali wakisaka kocha mpya ambapo hivi karibuni Mwanaspoti linafahamu kuwa mazungumzo yao na kocha mmoja raia wa Ureno yalikwenda vizuri na kazi ya kumtoa kwao na kumleta nchini kumtambulisha kisha kuanza kazi ya kukinoa kikosi cha Simba. Mabosi wa Simba walikuwa wanatafuta (connection) ya ndege kutoka Ureno ili kufika Tanzania kwani mazungumzo na kocha huyo yalikuwa yamekamilika ila katiuka hali isiyojulikana hadi sasa suala hilo limekwama hapohapo. Novemba 7, 2021, Simba ilimtambulisha Pablo kuwa kocha mpya wa kikosi hicho akichukua mikoba ya Didier Gomes na hukudumu kwenye kikosi hicho kwani Machi 31, 2022 Simba iliachana na Mhispania huyo na nafasi yake kuchukuliwa na Zoran Maki aliyedumu kwa siku 70 tu, kabla ya nafasi hiyo kukaimiwa na Juma Mgunda. Simba inatafuta kocha kwa ajili ya kukijenga kikosi chake kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara na vilevile kujipanga kwa ajili ya kujipanga na Ligi ya Mabingwa Afrika itakayoanza Februari.