Mwamuzi achezea kichapo Dodoma, akimbia

Mwanaspoti
Published: Feb 01, 2023 15:45:54 EAT   |  Sports

Dodoma. Mwamuzi Halima Ally wa mkoani Manyara amechezea kichapo kutoka kwa mashabiki na wachezaji wa timu ya Fountain Gate katika mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) uliomalizika jioni ya leo katika uwanja wa Jamhuri Jijini hapa. Mchezo huo ulikuwa dhidi ya Ceasiaa Queens ya mkoani Iringa na ulimalizika kwa timu hizo kutoka sare ya kutofungana. Mara baada ya kumalizika mchezo huo baadhi ya wachezaji wa Fountain walianza kumzonga huku wakitaka kumpiga. Kuona anazidi kuzongwa mwamuzi huyo ilibidi atimue mbio hadi jukwaa ambapo alipokelewa na mashabiki wa Fountain waliokuwa na hasira. Wakati akiingia katika vyumba vya kubadilishia nguo mashabiki wa timu hiyo walimfuata na kuanza kumpa kichapo ambapo baadhi ya waamuzi ambao hawakuwa na jezi waliokuwepo jukwaa Kuu ilibidi waingilie kumwokoa mwamuzi mwenzao. Ilibidi mwamuzi huyo aingie katika chumba cha waandishi wa habari badala ya cha kubadilishia nguo kutokana na mashabiki hao kumrushia chupa pamoja na kumpiga. Baadhi ya wachezaji waliungana na mashabiki hao na kumpa kichapo mwamuzi huyo huku baadhi wakimwagia maji Baada ya dakika kadhaa mwamuzi huyo aliingia katika vyumba vya kubadilishia nguo huku waamuzi wenzake ambao hawakuwa na jezi wakimkinga asipigwe na mashabiki na wachezaji wa Fountain. Hata hivyo mashabiki wa Fountain waliendelea kusubiria jukwaa Kuu wakitaka mwamuzi huyo atoke waendelee kumpa kichapo.