Mechi ya Yanga yamliza Asukile

Mwanaspoti
Published: Nov 30, 2022 12:54:45 EAT   |  Sports

WAKATI mwingine kazi inaweza ikamtambulisha tofauti mtu. Ndivyo pia ilivyo kwa nahodha wa Tanzania Prisons, Benjamin Asukile anayeonekana anatumia ubabe akiwa uwanjani kutimiza majukumu, ilhali nje ya soka ana maisha tofauti kabisa. Mwanaspoti limegundua hilo baada ya kufanya mahojiano na mchezaji huyo ambaye ni askari wa Jeshi la Magereza na kubaini nyuma yake ni mkarimu, mnyenyekevu, mcheshi na sura yake inabadilika kulingana na mazungumzo yanavyofanyika. Kama mazungumzo yanakuwa ya kuchekesha muda wote utamuona ni mwenye sura ya furaha, ilhali kama yatabadilika na kuhusu huzuni ni rahisi kuona macho yakimbubujika, hivyo sura inatoa taswira ya mazungumzo husika. Katika mahojiano yaliyofanyika eneo la Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam, Asukile amefunguka mambo aliyojifunza na anayoendelea kujifunza kwenye soka la Tanzania. UBORA NA UDHAIFU LIGI KUU Asukile anasema udhaifu uliopo kwenye ligi ni mabadiliko ya kila wakati ya ratiba na pia baadhi ya timu zimekuwa zikipewa kipaumbele hasa katika suala la muda wa mechi. “Kwenye ligi hatujawahi kufuata ratiba kama ilivyopangwa hadi mwisho, lazima kutatokea viporo. Sijui kwa nini, (lakini) umekuwa kama ugonjwa wetu. “Kama tungekuwa tunafuata ratiba vizuri ligi yetu ingekuwa bora kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati au Afrika nzima,” anasema Asukile. “Najiuliza kama ratiba inapangwa kulingana na ratiba za CAF au Fifa sasa kwa nini unakuta baadaye inapanguliwa panguliwa? Shida ni nini na kama ipo mbona hawaitafutiwi tiba.” Kinachomshangaza zaidi nyota huyo ni kwamba, licha ya uwepo wa kanuni, lakini kunakuwepo kuahirisha kwa mechi na sababu inakuwa ni wachezaji watatu au wanne kuitwa Taifa ‘Stars’. “Timu inasajili wachezaji 30 au 25 wachezaji watatu wakikosekana kwenye hiyo timu unasema tunaahairisha mechi? Dah! mpira wa Tanzania kazi sana huwa naumia sana kuona kwa nini hatubadiliki,” anasema Asukile. “Unajiuliza ina maana wachezaji wawili au watatu watazuia timu fulani isicheze mechi kisa wameenda timu ya Taifa na mwisho mnatengeneza viporo kwenye ligi visivyokuwa na maana yoyote. “Halafu hilo jambo linaweza kuwaathiri hata kisaokolojia wachezaji wengine wa hiyo timu kwani kila mtu ana mtazamo wake. Mtu anaweza akahoji ina maana wachezaji wawili au watatu ndio wanaibeba timu nzima, hapo ndipo yanapoanzia matabaka. “Mfano wachezaji watatu wameumwa je timu haitaenda kucheza na mtatoa taarifa kuwa haiendi kucheza kisa hao watatu wanaumwa. Ifikie hatua lazima ratiba ipewe heshima yake ndipo tutakapofikia malengo tunayoyata kila siku.” Asukile anashangazwa kwa nini timu kongwe hazipangwi kucheza mechi za mchana (saa 8:00) badala yake ratiba ya muda huo inakuwa kwa timu ndogo. “Iweje baadhi ya timu hasa hizi ndogo ndio zicheze mchana na hizo zingine zinazoitwa kongwe hazijawahi hata mara moja kucheza muda huo. “Hata huko Ulaya kuna muda Manchester United au Real Madrid zinacheza wakati wa jua kali na wakati mwingine usiku, lakini hapa kwetu lini umewahi kusikia Simba na Yanga zinacheza mchana? Je wenyewe wanacheza ligi gani? Ina maana ligi wanayocheza ni tofauti na yetu. “Wasiangalie wingi wa mashabiki au huyu anasema nini wafuate haki kama wanapanga huyu anaweza kucheza mchana, basi na mwingine yeyote acheze mchana kwa sababu wote tunashiriki ligi moja.” Nyota huyo anasema kama mamlaka za soka nchini zitaweza kuondoa udhaifu, anaamini soka la Tanzania litapiga hatua akisisitiza kwamba wapo mashabiki wa Simba na Yanga wanaopenda mpira wa ushindani, lakini hawapendi timu ndogo zionewe. UDHAMINI LIGI KUU Nje na kutaja upungufu uliopo kwenye ligi akivitaka vyombo husika kutafuta tiba, pia anasema TFF na Bodi ya Ligi wamejitahidi kusaka wadhimini na kuondoa adha kwa baadhi ya timu ambazo zilikuwa zinakwama kusafiri kwenda vituo vya mechi. “Yapo mambo ambayo TFF na Bodi ya Ligi wanastahili pongezi, naamini wataongeza (wadhamini) wengine ili kuzifanya ligi za madaraja yote kuwa na ushindani utakaofanya timu za taifa ziwe na wachezaji wa viwango vikubwa. “Udhamini wa Azam, NBC umesaidia timu kupata urahisi wa kufanya mipango kama maandalizi, kusafiri na pia kufunga taa kwenye baadhi ya viwanja, ili mechi ziweze kuchezwa usiku,” anasema Asukile WA KIGENI LIGI KUU Asukile hapingani na uwepo wa wachezaji wa kigeni katika Ligi Kuu isipokuwa jicho lake linatazama namna Taifa Stars inavyoathirika akitoa sababu ya kauli yake. “Asilimia 90 wachezaji wanaotegemewa kuunda timu yetu ya Taifa ni kutoka Yanga, Simba na kidogo Azam FC. Ndani ya vikosi hivyo wachezaji wanaocheza kikosi cha kwanza ni wageni, je pindi yanapokuja majukumu ya taifa na wazawa wengi wanakaa benchi ushindani wanaupataje?” anahoji. “Endapo (wazawa) kama watakuwa wanapata nafasi ya kucheza vikosi vyao vya kwanza na wakapata uzoefu wa michuano ya kimataifa, basi Stars yetu itakuwa imara zaidi na yenye matokeo chanya.” MECHI NA YANGA BALAA Mechi dhidi ya Yanga, Asukile analilazimika kusimulia baada ya kuulizwa ilikuwaje alilalama sana mechi dhidi ya wababe hao wa Jangwani walipofungwa bao 1-0 mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) uliofanyika April 30, mwaka jana kwenye Uwanja wa Nelson Mande Sumbawanga. Baada ya mchezo Asukile alikuwa na hasira na alifanya mahojiano na kituo cha runinga cha Azam na kutoa tuhuma nzito. “Huwa nikikaa nikifikiria ile mechi nabaki naumia tu kwani tulikuwa na uhakika ilikuwa ndani ya uwezo wetu kushinda ila ndio hivyo labda Mungu hakupanga,” anaanza kwa kusema. “Kuna vitu nilivyoongea baada ya ile mechi lakini siwezi kuvizungumzia tena kwa sababu vilishapita, ila soka la bongo lina mambo mengi sana. Mungu atusaidie tu.” Asukile anasema haogopi kusema ukweli wa anachoamini na hahofii kuchukiwa kwani hawezi kukaa na kitu moyoni ambacho kinamuumiza. “Baada ya ile mechi na kufanya yale mahojiano nilikuwa na siku mbaya sana na nilipigiwa simu nyingi mno hadi nikaamua kuzima maana niliona nijiepushe nisije nikayazua mengine na hata kuwajibu watu vibaya. “Nakumbuka baada ya kufika kwenye vyumba vya kubadilishia nguo nililia sana, kwani ni mechi ambayo iliniuma kwa sababu ilikuwa ndani ya uwezo wetu kushinda. Niliwaza mambo mengi mpaka nilifikia kuacha mpira wenyewe. “Kwa sababu unatumia nguvu kubwa uwanjani halafu kuna mtu anakuja kukufanyia mambo ya ajabu ambayo hayatakiwi kwenye mpira. Yaani niliwaza kuwa kuna siku nitakuja kustaafu na mtu kwenye huu mpira,” anasema. Asukile anasema siku ya pili baada ya mchezo alitakiwa kwenda Dar es Salaam kujiunga na kambi ya soka la ufukweni jambo ambalo alilifanya na anamshukuru kocha wa timu hiyo, Boniface Pawasa ambaye alikaa naye muda mwingi kumjenga kisaikolojia. “Pawasa namshukuru sana kwani tuliongea vitu vingi na ukizingatia yeye amecheza soka muda mrefu na amepitia mengi, hivyo alinituliza na alinifundisha. Ni kama alichukua nafasi sio tu kama kocha, bali kama kaka na baba pia. Kiukweli mambo tuliyoongea yalinisaidia sana na nikawa sawa,” anasema. NI KWELI MBABE? Asukile anasema yeye si mbabe kama watu wanavyohisi au kudai, bali ni asili yake kutokubali kushindwa jambo kwa urahisi. “Mbona mimi naona nacheza kawaida tu na wala sina ubabe wowote, ila nakuwa mbishi kwa sababu sipendi kushindwa kirahisi na hii roho ya kutokubali kushindwa nilijengwa na baba yangu,” anasema mkongwe huyo. “Halafu watu lazima wajue mpira wakati mwingine kuwe na ubabe kidogo uwanjani. Sasa utachezaje hata hamgusani kwani muziki huo na hata falsafa ya Prisons ni soka la kibabe. msimu huu ndio tunacheza mpira mlaini sana. Hata tulivyochukua timu yenye nidhamu msimu uliopita nilikwazika sana nikajisemea Prisons imefikia hatua ya kuchukua timu yenye nidhamu? Nikajisemea kweli siku hizi hatuchezi pira gwaride.” TIMU LIGI KUU, APATA AJIRA Unaweza usiamini kwani watu wengi walikuwa wakifikiria Asukile ni askari Magereza muda mrefu, kumbe ilikuwa sivyo kwani mwenyewe anafichua kuwa ajira amepata mwaka huu. Asukile aliisaidia Tanzania Prisons kubaki Ligi Kuu msimu huu baada ya kufunga bao la kusawazisha katika mchezo wa mtoano dhidi ya JKT Tanzania uliofanyika Julai 13, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya na matokeo kuwa bao 1-1. Aliingia uwanjani dakika ya 49 na katika mchezo huo alitumia dakika 20 tu kufunga bao la kusawazisha ingawa hata hivyo hakumaliza mechi baada ya dakika ya 90+4 kuonyeshwa kadi nyekundu pamoja na beki mwingine wa kikosi hicho, Jumanne Elifadhili. “Baada ya ile mechi kila mtu alifurahi. Kuanzia familia, mashabiki, askari Magereza yaani ndipo niligundua hii timu yetu inapendwa bwana, maana maaskari waliunda makundi na kunichangia pesa. “Nashukuru pia baada ya muda mrefu nilipata na ajira ya kudumu, kwani nilikuwa si askari na wengi waliamini kuwa mimi ni mjeda muda mrefu kwa jinsi ninavyojitolea uwanjani na nilivyokuwa na uchungu na timu, lakini haikuwa hivyo kwani kuna baadhi ya vitu vilikuwa havijakamilika. Lakini nashukuru mwaka huu nikapata ajira,” anasema. SALUTI YA BOCCO Asukile anasema straika wake bora wa muda wote Bongo ni John Bocco ‘Adebayor’ wa Simba huku akiwataka mashabiki na viongozi kumpa heshima yake mchezaji huyo. “Bocco amejitahidi sana kuwa kwenye kiwango bora kwa muda mrefu na amefanya vizuri. Hata kipindi fulani mashabiki wa Simba wakati wanamuandama eti ni mzee aachwe ilikuwa inaniuma. “Hebu wajaribu kumpa heshima yake jamani, waangalie ni mazuri mangapi aliyowafanyia kwani kila kitu kina wakati wake. Hauwezi kuwa bora kwa muda wote. Lakini walijiulize je wakati ule alitufanyia kitu gani. Alikuwa na mazuri gani. Aliipambania timu hadi inachukua ubingwa mara nne mfululizo leo mnamdharau, ahaa! Jamani wampe heshima basi japo kidogo. Sasa hivi ameshuka kiwango kidogo tu wanaanza kumponda mara mzee. Sasa wanataka asizeeke halafu kwenye mpira hakuna mzee bali kuna mzoefu au mkongwe,” anasema. NJE YA SOKA Asukile anasema nje ya soka ni mpole na mcheshi ingawa wengi wanajua na hawataamini hilo. “Mimi ni mpole sana ila watu wengi wananichukulia yale (nayofanya) ya uwanjani basi nje ya uwanja niko hivyo hivyo ni tofauti na mawazo yao. “Napenda kucheka, sipendi ugomvi wala mivutano na mtu. Mambo yangu ya uwanjani yanaishia uwanjani, nikitoka tu nakuwa mtu tofauti. “Huwezi kuona nimeenda klabu au kwenye sehemu ya vilevi na sina rafiki wa karibu kwani kila mtu ni rafiki yangu,” anasema Asukile ambaye anapenda vyakula vya asili. FAIDA NA HASARA ZA KAMBI Asukile anasema haoni faida ya kukaa muda mrefu kambini kwani mpira wa sasa umebadilika na mchezaji mwenye akili anajitunza mwenyewe. “Mnaweza mkakaa kambini muda wote, lakini ukampa nafasi ndogo tu mchezaji humohumo kambini akaharibu. Ndio maana nasema binadamu anajichunga mwenyewe muhimu atambue wajibu wake,” anasema. “Pia kukaa kambini muda mrefu ni hasara upande mwingine kwa sababu kuna maisha mengine nje ya mpira mchezaji anatakiwa kufanya ikiwemo kufuatilia madili zikiwemo biashara ambazo zitamsaidia pindi akiachana na soka.” ALIPOANZIA SOKA Asukile alianza soka la ushindani katika timu ya Tanzania Prisons msimu wa 2009/2010 na baada ya msimu mmoja akajiunga na Kagera Sugar aliyoichezea hadi 2015 na kurejea Prisons alipo hadi sasa. “Unajua nafasi ya kwanza kucheza ilikuwa kipa wakati huo nikiwa timu za madaraja ya chini huko Tukuyu, hivyo hata likitokea lolote Prisons mfano kipa kapewa kadi nyekundu na hakuna mwingine nakaa golini nadaka. Ni kama ilivyo kwa Jumanne Elifadhili ambaye naye alivyokuja Prisons alikuwa kipa, ila baadaye ndio akabadilishwa na kucheza ndani. Akizungumzia pesa ya kwanza kuishika akiwa mchezaji, Asekile anasema: “Ilikuwa 300,000 nilitumia kununua redio kwa sabau napenda sana muziki hasa ile ya zamani. Hii ya kizazi kipya inategemea na upi naukubali ingawa zamani Diamond alikuwa anaimba sana, ila siku hizi nyimbo zake zimekaa kiujana sana kuna sehemu huwezi kusikiliza na watoto au wazee,” anasema Asukile ambaye anasema alivutiwa kuingia kwenye soka na beki wa zamani wa Yanga, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’ na Hayati Godfrey Bonny ‘Ndanje’. HII SASA NDO PRISONS Asukile anasema inawezekana Prisons ilikuwa timu bora tangu miaka ya nyuma, lakini kuna kikosi alikishuhudia 2008/2009 kilikuwa hatari na kilicheza ‘pira gwaride’ ambalo hadi leo halijawahi kutokea.