Mbaraka, Mhilu wapishana Kagera Sugar

Mwanaspoti
Published: Nov 28, 2022 11:51:54 EAT   |  Sports

BAADA ya kuanza katika mechi 13 za Kagera Sugar msimu huu, mshambuliaji wa timu hiyo, Mbaraka Yusuph leo amepumzishwa huku nafasi yake ikichukuliwa na Yusuph Mhilu ambaye hajaanza katika mechi mbili zilizopita. Kagera Sugar itashuka uwanjani muda mfupi ujao kuivaa Mtibwa Sugar katika dabi ya Wakata miwa inayopigwa kuanzia saa 8 mchana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Wenyeji wanaingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kuvuna alama nne ugenini kwenye michezo miwili iliyopita dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons huku wakikumbuka kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga mara ya mwisho walipocheza Kirumba. Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime ambaye leo ni mchezo wake wa tano tangu akabidhiwe jukumu la kuinoa timu hiyo amefanya mabadiliko hayo ya mchezaji mmoja baada ya kuanza na kikosi kile kile kwenye michezo miwili iliyopita dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons. Katika mchezo wa leo Maxime anasaka ushindi wa tatu ambapo ameanza na kipa, Said Kipao, mabeki wa pembeni Dickson Mhilu na David Luhende huku mabeki wa kati wakiwa Laurent Alfred na Abdallah Mfuko. Viungo ni Abdallah Seseme, Ally Ufudu na Ally Ramadhan 'Kagawa' huku mawinga wakiwa ni Yusuph Mhilu na Meshack Mwamita na mshambuliaji wa kati ni Anuary Jabir mwenye mabao manne. Kikosi cha akiba ni Ramadhan Chalamanda, Deus Bukenya, Datius Peter, Appolinaire Ngueko, Yusuph Dunia, Erick Mwijage, Mbaraka Yusuph, Hamis Kiiza na William Edgar.