Mbabe wa Simba aanza kazi Prisons

Mwanaspoti
Published: Feb 01, 2023 10:28:52 EAT   |  Sports

Mbeya. Baada ya kuwasili kikosini, hatimaye Abdalah Mohamed 'Bares' ameanza kazi rasmi leo, Februari Mosi kuitumikia Tanzania Prisons akisimamia matizi ya nyota wake katika uwanja wa Magereza jijini hapa. Bares ametua kikosini humo kuchukua nafasi ya mtangulizi wake, Patrick Odhiambo raia wa Kenya ambaye alitemwa kutokana na matokeo kutokuwa mazuri baada ya mkataba wake kumalizika Januari 14. Bares amesaini kandarasi ya miezi sita japokuwa katika mkataba wake kipo kipengele cha kuongeza iwapo timu hiyo itafanikiwa kubaki ligi kuu msimu ujao. Kocha huyo aliyewahi kuhudumu kwa Wajelajela hao msimu wa 2019/20 kabla ya kuondoka katikati ya 2020/21 anarejea tena huku akitarajia kuanza na mchezo ujao dhidi ya Mtibwa Sugar, Ijumaa ya wiki hii. Mzanzibar huyo anarejea tena Bara akiwa na kumbukumbu ya kufanya vizuri katika michuano ya kombe la Mapinduzi alipoipa ubingwa Mlandege FC huku akiwavua taji waliokuwa bingwa mtetezi, Simba. Hadi sasa Prisons ipo nafasi ya 12 kwa pointi 21 baada ya mechi 22 na sasa Kocha huyo atakuwa na kibarua kizito kuhakikisha timu hiyo inabaki ligi kuu msimu ujao.