Mayele afichua siri kambini

Mwanaspoti
Published: May 25, 2023 12:16:26 EAT   |  Sports

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Fiston Mayele ameelezea namna wachezaji wa timu hiyo waliopo kambini wanavyotamani kuchukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kwenye fainali dhidi ya USM Algers. Yanga imetinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho ikiwa ni mara yao ya kwanza kufikia hatua hiyo kubwa kwenye michuano ya Afrika. Akizungumza na Mwanaspoti Jijini Dar es Salaam,Mayele ambaye ni raia wa DR Congo, alisema kila mchezaji kambini anasubiri kwa hamu kuona timu hiyo inatwaa ubingwa mwezi ujao na kila hatua wanazungumzia hilo. Staa huyo anaongoza kwa kufunga mabao kwenye Kombe la Shirikisho akiwa ameshafunga sita, lakini pia anaongoza kwenye Ligi Kuu Bara akiwa amepachika mabao 16 hadi sasa zikiwa zimebaki mechi mbili ligi imalizike. “Akili zetu zote zipo katika mchezo muhimu unaowakilisha Taifa na nguvu zetu tumeweka huko ili kuhakikisha tunafanya vizuri, kambini kwetu kwa sasa kila mmoja anatamani kuona tunatwaa ubingwa na hayo ndiyo mazungumzo ambayo yamekuwa yakitawala, lakini wakati mwingine tukipeana mbinu za hapa na pale kuhakikisha tunapata ushindi kwenye mchezo wa fainali, kila mmoja amekuwa akimhimiza mwenzake kuhakikisha anafanya vizuri.” “Fainali yoyote siyo ya kuupuuzwa kwetu ndio maana tunafanya maandalizi makubwa ili kuhakikisha tunafanya vizuri na kurudisha heshima kikosini kwetu,” alisema Mayele raia wa DR Congo. Yanga wanatakiwa kuutumia vema uwanja wake wa nyumbani Jumapili kabla haijaenda kumaliza kazi nchini Algeria Juni 3, mwaka huu. Hii siyo mara ya kwanza kwa Yanga kukutana Algier kwani waliwahi kuvaana kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2018.