Mastaa Azam kutibiwa Aga Khan

Mwanaspoti
Published: Feb 01, 2023 10:14:07 EAT   |  Sports

TAASISI ya Utoaji wa Huduma za Afya ya Aga Khan, Tanzania (AKHST) imeingia makubaliano ya kutoa huduma za matibabu, mafunzo na uchunguzi wa afya kwa ujumla na klabu ya Azam kwa kipindi cha miaka miwili. Makubaliano hayo yamefikiwa Leo, Februari mosi, 2023 kwenye moja ya kumbi za mikutano za Hospitali hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam ikiwahusisha Watendaji wakuu (CEO’s) wa taasisi zote mbili, Sisawo Konteh wa AKHST na Abdul Kareem ‘Popat’ wa Azam sambamba na viongozi wengine. Mkataba huo unalenga kuimarisha uhusiano kati ya AKHST na Azam Fc, ukijikita zaidi kwenye kutoa huduma mbalimbali za matibabu katika vituo vyote vya AKHST vilivyopo nchini ikiwemo upimaji wa afya, upatikanaji wa huduma za maabara na miyonzi, mafunzo, ukarabati na huduma za uchunguzi, uhamasishaji wa habari za afya na Elimu, na mashauriano zaidi ya kitaalamu kwa wachezaji, benchi la ufundi na wafanyakazi wanaotambulika wa klabu hiyo. Ofisa Mtendaji mkuu wa AKHST, Konteh amesema wamefurahi na kujivunia kushirikiana na Azam ikiwa ni moja ya klabu za soka zinazofanya vizuri zaidi Tanzania. “AKHST imejitolea sana kutoa huduma za matibabu za kiwango cha kimataifa katika Hospitali na Kliniki zetu huku tukiifikia jamii kwa namna mbalimbali ikiwemo kupitia michezo na afya njema. “Ni maoni yetu tunaenda kuwa kiongozi wa Kikanda katika dawa na tiba ya michezo.” Alisema Konteh. Kwa upande wa Azam, Popat alisema; “Siku zote tunachunguza namna tunavyoweza kuimarisha afya na uchezaji wa wachezaji wetu ili kuhakikisha wanatambua uwezo wao wakiwa salama uwanjani na ushirikiano huu utatusaidia kuongeza utimamu wa mwili na afya njema kwa timu zote, Wafanyakazi na benchi la ufundi,” alisema Popat na kuongeza; “Nilichoona katika Hospitali hii, (AKHST) katika suala la vifaa na utoaji wa huduma ya matibabu imekuwa ya kushangaza sana, tumejifunza na tutaendelea kujifunza mambo mengi kutoka hapa na tutaimarisha ushirikiano wetu.” Aidha kusainiwa kwa mkataba huo, Azam itanufaika katika maeneo mengine, kujenga uwezo juu ya mafunzo maalumu yanayohitajika na mamlaka za soka, kuinua viwango vya huduma za dharura, kuendelea na uchunguzi wa kimatibabu kwa wachezaji wapya waliosajiliwa kila msimu, usaidizi wa mipango ya pamoja ya jamii na kukuza elimu ya afya na uhamasishaji.