Kipa wa vijana amrithi Parapanda Singida

Mwanaspoti
Published: Apr 02, 2024 15:03:53 EAT   |  Sports

UONGOZI wa Singida Fountain Gate umempandisha kipa, Aziz Said Mohammed kutoka timu ya vijana kuziba pengo la Ibrahim Rashid 'Parapanda' aliyeenda kwenye kozi ya jeshi Zanzibar. Parapanda ambaye alikuwa kipa namba mbili wa Singida Fountain Gate ametimka ndani ya kikosi hicho na anatarajia kurejea mwishoni mwa msimu huu. Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari ya Singida Fountain Gate, Hussein Massanza amesema wamemruhusu kipa huyo kwenda kozi na kufanya jitihada za kumpandisha mwingine kutoka timu ya vijana ili kukamilisha idadi ya makipa watatu. "Parapanda ameshaondoka na tayari tumempandisha Aziz kwaajili ya kuungana na nahodha Kakolanya na Benedict Haule ambao watamalizia mechi za msimu huu," amesema. "Wanatambua umuhimu wa nafasi aliyoipata kipa huyo na tunaamini itakuwa na faida kwa mchezaji miaka ijayo huku tukitengeneza kipa mwingine ambaye atapata ujuzi kutoka kwa walio mtangulia." Akizungumzia kupandishwa kwa Aziz amesema ni faida kwa mchezaji na klabu kwa ujumla kwani kupandishwa kwa kiwango atakachoonyesha ana uwezo wa kupata nafasi ya kukaa langoni. "Hivyo endapo atapata nafasi hiyo ni faida kwake kujijengea kujiamini na kujipa nafasi ya kuonekana zaidi kwa timu nyingine lakini pia atapata mafunzo kutoka kwa kaka zake kina Kakolanya na Haule," amesema.