HISIA ZANGU: Manzoki na kumfunga mtani vilipogeuzwa ajenda ya uchaguzi

Mwanaspoti
Published: Feb 01, 2023 12:19:55 EAT   |  Sports

MPAKA leo ni nani ambaye anaweza kuelewa mshambuliaji wa Mkongomani, Cesor Manzoki alikuja kufanya nini katika mkutano mkuu wa Simba? Ni ngumu kujua. Ni mshambuliaji ambaye Simba ilimkosa katika dirisha kubwa lililopita kwa sababu aliuzwa kwenda China. Aliibuka katika ukumbi wa uchaguzi wa Simba na kuwasalimia wana Simba ambao akili zao zilikuwa wamezielekeza katika uchaguzi. Baada ya hapo akawapiga kijembe watani wa Simba, Yanga. Nadhani alipewa maelekezo hayo. Habari yake ilikuwa tofauti kidogo na watani zao ambao msimu uliopita katika mkutano wao walimtambulisha kiungo mpya wa kimataifa wa Burundi, Gael Bigirimana. Tofauti ni kwamba Yanga ilikuwa inamtambulisha mchezaji. Simba ilikuwa imemuita ukumbini mchezaji ambaye sio wao na hatarajii kuwa wao siku za karibuni. Pande zote mbili zimekosea lakini Simba imekosea zaidi. Kwa Yanga nadhani ilikuwa mara ya pili kumtambulisha mchezaji katika ukumbi wa mikutano. Mchezaji wa kwanza alikuwa Juma Balinya. Alitambulishwa pale Diamond Jubilee. Huyu Bigirimana ni wa pili. Wachezaji wana mahala pao pa kutambulishwa. Wachezaji hawatambulishwi katika majumba ya mikutano. Wanatambulishwa mbele ya waandishi wa habari na watendaji wa timu. Kule katika majumba ya mikutano ni habari za kisiasa tu. Mchezaji anaweza kutambulishwa na kocha au mtendaji mkuu wa klabu huku akiwa ameshikilia jezi. Habari inaishia hapo. Zile picha za koti jeupe pale GSM huwa zinatosha sana. Wakati mwingine tusipofanya mambo ya kisasa Mungu huwa anakuja kutuumbua mbele ya safari. Balinya na Bigirimana wote wamefeli vibaya Yanga. Halafu kuna hawa rafiki zangu Simba ndio wamechemsha zaidi kwa kumuingiza mchezaji ambaye sio wao katika siasa za klabu. Kuna namna fulani ilitumika kuwafanya wanachama wa Simba kama vile ni watu wajinga kitu ambacho sio sahihi. Nashukuru hata wengine wengi kati yao wamepinga. Huyu ni mchezaji ambaye Simba ilimhitaji msimu uliopita. Ikadanganywa kwamba anaweza kuja katika dirisha la Januari kwa sababu mbalimbali. Wakati huo alikuwa amekwenda kucheza soka la kulipwa China ambako analipwa kiasi kikubwa cha pesa ambacho sisi hatuwezi kumlipa. Aliletwa nchini kwa mpango mahususi wa kuwatia tamaa wana Simba kwamba anaweza kuja muda wowote kuanzia sasa. Hii ilikuwa maalumu kwa ajili ya kumpa nguvu mgombea wa nafasi ya uenyekiti. Kwamba kambi yake ilitaka kuwaonyesha wapigakura kwamba wao hawana ahadi feki. Kwamba walizungumza suala la Manzoki na kweli mpaka sasa Manzoki yupo katika rada zao na anaweza kutua Simba. Siwezi kumlaumu Manzoki kwa sababu alikatiwa tiketi ya ndege bure, akaenda kulala katika hoteli ya kifahari bure, na inawezekana kwamba alipewa kiasi fulani cha pesa kwa ajili ya kuifanya kazi hiyo. Nani angekataa? Tatizo nimeiona athari katika suala zima la ujio wake. Kwanza ni namna ambavyo mpinzani wa mgombea wake amepata kura nyingi. Lakini pia kuna hatari kubwa kuwahusisha wachezaji hawa na siasa za uchaguzi. Vipi kama angeshinda mgombea mpinzani? Nafasi ya Manzoki kuchezea Simba siku za usoni ingekuwa wapi? Lakini kwa kiasi fulani ni suala ambalo linashusha morali kwa wachezaji waliopo ambao wanaendelea kuitumikia Simba kwa sasa. Wanapoona mchezaji mmoja anapewa promo kubwa wakati havai jezi yao kuna athari kwamba siku akija kuvaa wanaweza kumtenga kwa sababu tayari uongozi umewapa ishara kwamba ni mchezaji muhimu zaidi. Tukiacha na hilo la Manzoki, liliibuka jambo ambalo lilinichekesha zaidi katika kampeni hizi za Simba. Mgombea aliyeshinda alikuwa amebanwa kuhusu suala la kutomfunga mtani wa jadi katika utawala wake. Ameshinda mechi moja tu kule Kigoma katika Kombe Shirikisho la Azam. Watu wamemjia juu kuhusu ukame wa kutomfunga mtani ambaye amekuwa akitawala mechi zao. Na yeye ametoa ahadi ya kumfunga mtani. Wakati mwingine unaweza kudhani sasa hivi tupo mwaka 1823. Mpaka leo tunawaza namna ya kumfunga mtani na kuona ni moja kati ya mafanikio maku bwa klabuni. Wanachama wanaowaza hivyo wanaishi katika zama za mawe. Mgombea anayetoa ahadi hiyo pia anaishi katika zama za mawe. Huu ni wakati ambapo Simba na watu wake wanapaswa kuwaza mambo makubwa zaidi klabuni. Wanapaswa kuwaza kufikia maendeleo halisi ya klabu ya soka kama vile ongezeko la mapato, kuimarisha huduma mbalimbali za klabu, miundombinu ya klabu, kutwaa mataji barani Afrika na mengineyo. Simba na Yanga huwa zina mechi mbili za msingi kwa msimu lakini zina mambo mengi ya kufanya nje ya kufungana. Hata kocha mkuu au nahodha wa timu hapaswi kutoa ahadi ya kumfunga mtani. Katika pambano la soka jambo lolote linaweza kutokea. Kitu cha msingi ni kuangalia namna msimu mzima ulivyokwenda na kipi ambacho klabu imevuna. Zamani kulikuwa na watu ambao wanaamini ukimfunga mtani mara mbili katika ligi halafu mtani akatwaa ubingwa, basi msimu huo umekuwa wenye mafanikio kwa sababu mtani atafunga mdomo. Nilidhani watu wa namna hiyo wameondoka lakini kumbe bado wanaishi. Na mbaya zaidi wanapewa dhamana kubwa ya kuongoza soka. Hapa katikati Simba ilikuwa inafanya vizuri katika michuano ya kimataifa halafu ikafungwa na Bernard Morrison na Zawadi Mauya katika za ligi. Baadhi ya watu wa Yanga walianza kuchoshwa na tabia za kumfunga mtani, huku wakiwa hawatwai mataji wala kushiriki vyema katika michuano ya kimataifa. Ule ulikuwa mwelekeo sahihi zaidi wa mabadiliko ya kihisia. Lakini kwa hiki ambacho kimeibuliwa tena majuzi katika uchaguzi wa Simba inaonekana safari yetu bado ni ndefu. Nilidhani ulikuwa wakati wa kujikita kuangalia namna gani Simba itashiriki vyema katika hatua ya makundi, lakini kumbe hadithi imekuwa tofauti.