Bruno, Mangalo kuiwahi Namungo

Mwanaspoti
Published: Nov 29, 2022 08:44:59 EAT   |  Sports

NYOTA wa Singida Big Stars, Bruno Gomes na Abdulmajid Mangalo huenda wakawa fiti kwenye mchezo unaofuata wa timu hiyo wakati kikosi hicho kitakapocheza na Namungo Disemba 2. Mastaa hao wawili walikosekana juzi kwenye mchezo walioibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting. Akizungumza na Mwanaspoti daktari wa timu hiyo, Shaban Shija alisema maendelezo yao sio mabaya na kuanzia wiki inayofuata watakuwa fiti kucheza hivyo mashabiki wasiwe na hofu. “Baada ya mchezo wetu na Yanga, Bruno alipatwa na tatizo kidogo kwenye mapafu huku Mangalo yeye ana shida kwenye misuli ya goti ingawa afya zao zinazidi kuimarika,” alisema Shija. Shija aliongeza kuwa hadi kufikia mchezo wao dhidi ya Namungo utakaochezwa nyumbani kwao kwenye Uwanja wa Liti, Singida huenda mastaa hao wakawa fiti kwa asilimia 100 kucheza na kuisaidia timu. Kwa upande wa kocha msaidizi wa timu hiyo, Mathias Lule alisema kwa jinsi ambavyo ligi hii imekuwa ngumu na yenye ushindani mkubwa unapomkosa hata mchezaji wako mmoja inakuwa ni pigo kubwa. Bruno ambaye ni raia wa Brazil anayeichezea Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu ambapo hadi sasa amefunga mabao matatu huku akiwa mchezaji muhimu katika kikosi cha kocha Van der Pluijm.