Beki la mabao latajwa Yanga

Mwanaspoti
Published: May 25, 2023 09:53:33 EAT   |  Sports

YANGA tayari imetangazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu inayofikia tamati Juni 9 huku ikiwa ndio timu iliyoruhusu mabao machache kama ilivyo kwa Simba zilizofungwa mabao 15, huku Nickson Kibabage akiwa ndiye beki aliyefunga mabao mengi. Simba ndiyo timu inayoongoza kwa kufunga mabao mengi hadi sasa ikiwa imetupia kambani mabao 66, huku Yanga ikifunga mabao 56 na kati ya hayo, Fiston Mayele akifunga mabao 16. Hata hivyo, Mtibwa Sugar ndio timu iliyoruhusu mabao mengi zaidi ikifungwan 44 na kichapo kikali zaidi kukipata kilikuwa dhidi ya Simba mabao 5-0, Uwanja wa Mkapa Oktoba 30. Michezo ambayo Mtibwa imefunga mabao mengi ni ule dhidi ya Azam Novemba 12 wakati timu hiyo ikifungwa mabao 4-3 katika Uwanja wa Manungu. Timu nyingine iliyoruhusu mabao mengi ni Polisi Tanzania iliyofungwa mabao 40, sawa na Mbeya City ambayo yenyewe imefunga mabao 24 huku, Sixtus Sabilo ndiye kinara wa mabao akiwa amefunga tisa. Ruvu Shooting inafuata kwa kuruhusu mabao mengi msimu huu ikifungwa 39, ambapo tayari imeshashuka daraja kwa kuburuza mkia kwa alama zake 20 katika michezo 28 iliyocheza. Geita Gold, ambayo msimu uliopita ilishiriki kimataifa katika Kombe la Shirikisho imekuwa timu ya tano kwa kufungwa mabao mengi ambayo ni 38 huku ikifunga mabao 33 tofauti ya mabao matano tu. Ruvu Shooting inayonolewa na kocha Mbwana Makata licha ya kuwa timu ya kwanza kushuka daraja ndio timu iliyofunga mabao machache zaidi hadi sasa ikifunga mabao 18. Mshambuliaji mwenye mabao mengi kwenye kikosi hicho ni Abalkassim Suleman mwenye mabao manne ambayo aliyafunga kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, Polisi Tanzania, Geita Gold na Tanzania Prisons kwa mkwaju wa penalti. Wakati Abalkassim akiwa mshambuliaji mwenye mabao mengi kwenye kikosi cha Ruvu Shooting kwa mabao hayo manne, Nickson Kibabage wa Singida Big Stars ndiye beki mwenye mabao mengi kwenye ligi akiwa na mabao manne. Makata alisema kuna vitu vingi vimechangia timu kufika hapo ilipo hasa kutokana na uwepo kwa madhaifu mengi ambayo muda wa kuyarekebisha ulishapita, sababu ili timu ifanye vizuri lazima ifunge na kuzuia vizuri.