Beki aliyepiga division one ataja siri

Mwanaspoti
Published: Feb 01, 2023 11:50:48 EAT   |  Sports

BAADA ya kupata matokeo mazuri ya kidato cha nne, beki wa Fountain Gate Princess, Ester Mabanza amesema msingi mzuri aliojijengea kwenye suala la elimu ndio siri ya ufaulu alioupata. Beki huyo ambaye amehitimu elimu ya kidato cha nne katika Shule ya Fountain Gate Secondary School amepata ufaulu wa daraja la kwanza (division 1.16). Akizungumza na Mwanaspoti, Mabanza alisema alikuwa na muda mwingi wa kusoma tofauti na mambo ya mpira ni kutokana na kuipa kipaumbele elimu kwenye maisha yake. “Muda wa kusoma ulikuwepo nikiwa kwenye mambo ya mpira akili yangu ilikuwa inazingatia suala hilo na nikiingia kwenye maisha ya shule, basi nitahakikisha sitoki bila kitu kwa kufuatilia masomo na kuzingatia kile ninachokiamini,” alisema na kuongeza; “Mpira ulikuwa na muda wake hakukuwa na nafasi kubwa ya kunizuia kusoma nafikiri hilo ndilo limeweza kunipa mwanga mzuri wa kutenga muda wa kusoma na kuzingatia mambo muhimu ambayo yamenipa matokeo.” Alisema anapenda mpira na kusoma ndio maana kila kitu anakifanya kwa ubora kutokana na muda husika huku akisisitiza kuwa kila mmoja akiamua kufanya jambo au mambo kwa usahihi inawezekana. “Hakuna kisichowezekana kama mtu utaamua kuukikiwekea maanani, binafsi ninapenda kusoma na msingi wangu wa elimu umeanzia chini yaani tangu naanza kusoma na kuingia katika masuala ya mpira ni kitu ambacho nakipenda ndio maana nimevitengea muda nikiwa nafanya soka akili yote inakuwa hapo pia kwenye shule ni hivyo hivyo.”