Arafat: Yanga Princess kuna changamoto

Mwanaspoti
Published: Mar 24, 2023 12:25:10 EAT   |  Sports

Jana tuliona sehemu ambayo makamu mwenyekiti wa Yanga, Arafat akiwa anazungumza kuhusu usajili pamoja na mafanikio ya timu hiyo kwenye michuano ya kimataifa, alieleza kuwa baada ya kufanikiwa kufika hatua ya robo fainali sasa wanawaza hatua ya nusu fainali na kueleza mikakati ambayo wameiweka. Pia alizungumza mambo mengi yakiwemo mafanikio ya timu hiyo kwenye michuano mingine na jinsi walivyopambana kwa kipindi cha miezi tisa klabu hapo, sasa endelea na sehemu hii ya mwisho ya makala hii ambapo anaanza kwa kueleza kuhusu changamoto zilizopo kwenye timu ya wanawake, Yanga Princes. YANGA PRINCESS HALI IKOJE? Moja ya ahadi ambayo utawala wao uliiweka mbele ni kuijenga timu yao ya wanawake imara yaani Yanga Princess hapa anaeleza tathimini yao. "Binafsi naridhishwa na maendeleo yao lakini nikiri kuna changamoto bado timu haijatulia kwa namna ambavyo tunataka wananchi, niseme jambo moja kuunda timu sio kitu cha usiku mmoja, sote tunajua jinsi tulivyounda hii timu yetu kubwa ambayo sasa tunajivunia. "Mtaona jinsi tulivyoanza kwa kufanya usajili mkubwa kwa kuleta wachezaji wenye uzoefu na wanaochezea mataifa yao, lakini la pili tukalazimika kufanya mabadiliko ya benchi la ufundi kwa kuleta kocha mwingine, hizi zote ni hatua za kujenga kitu kilichoimara, sasa tupo katika kuwachia makocha wafanye kazi zao lakini pia wachezaji kuzoea mazingira. "Ukitazama ligi utaona hatujaachana sana na wanaongoza msimamo wa ligi, ukiniuliza nafasi ya ubingwa tutakubaliana kwamba bado ipo lakini tumewaachia makocha wetu kazi ya kuhakikisha klabu inafikia malengo yao wakati huu utawala nao tukitimiza wajibu wetu. ISHU YA FEISAL NI VIPI? "Nadhani kauli ya uongozi ilishatolewa na mimi sitakuwa na cha kubadili kutokea hapo ni jambo ambalo tumeliweka wazi kwa maeneo matatu kwa kuwa TFF imetoa msimamo kwamba yule ni mchezaji wetu basi arudi kutekeleza mkataba wake na Yanga hatutasita kumpokea kwa mikono miwili, pili atakaporejea kama ataona anahitaji kubaki hapa tuko tayari kuangalia maboresho yake ya mkataba kama ambavyo sera ya klabu inafanya na mwisho kama kuna klabu inamtaka basi ailete mezani hatutasita kumuuza kwa maslahi ya kipaji chake na maslahi ya klabu, tumeuza wengi yeye sio wa kwanza. "Mimi nina ushauri kwa Feisal, wachezaji na hata TFF nadhani kupitia sakata hili tunaweza kupata picha nzuri ya jinsi gani watu ambao wako nyuma ya wachezaji wetu baadhi yao au wengi wao sio watu sahihi kuwaongoza. "Kwanza niwapongeze TFF kupitia kamati yao ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ambayo imesimama imara kutoa majibu yaliyosahihi katika sakata hili, haya hayakuwa maamuzi ya kumkandamiza Feisal, yalikuwa ni maamuzi ya haki imeonekana kutendeka katika sura nyingine uamuzi huu ni uamuzi ambao umekwenda kutunza hadhi ya mpira wetu kwa wadau kuheshimu mikataba kama kungekuwa na kuyumba hapa watu wengi wangewalaumu TFF lakini walisimamia haki, tunatakiwa kuwapongeza kwa hili wameutendea haki mpira. "Kama kuna mtu ambaye yuko nyuma ya Feisal huyu ndio mtu wa kwanza ambaye hautendei haki mpira wa nchi hii lakini pia hamtendei haki mchezaji mwenyewe, watu wa namna hii tunatakiwa kushirikiana kuwafichua na kumuondoa katika mpira wetu nadhani TFF itakapoona kuna haja basi ziandaliwe semina za kutosha katika kuwapa elimu wachezaji wetu juu ya mikataba yao na hata kutafuta watu muafaka wa kuwasimamia. AHADI YA UJENZI WA UWANJA "Niwatoe hofu wananchi viongozi bado tupo katika njia kuu kutimiza ahadi ambazo tulizitoa wakati tunaingia madarakani, zipo ambazo tumeshazitekeleza, zingine zinaendelea katika kufanyiwa kazi, zoezi limeanza la ujenzi kwa hatua zote za awali, tumeshatambua mipaka ya eneo letu pale Jangwani, bahati mbaya ni kwamba baada ya kupimwa eneo tuligundua eneo letu limepungua kwa kiwango kikubwa sana. "Eneo hili lilivamiwa na eneo lililopo wataalam wetu walitushauri kwamba halitatosha kulingana na ramani ambayo tunataka kujenga uwanja pale wenye uwezo wa kuchukua watazamaji elfu ishirini, tumeshawasilina na serikali kuomba watuongezee eneo hilo na tuko pazuri katika mazungumzo yetu, tunafahamu kuwa kuna mipango ya kiserikali katika eneo lile hasa kutokana na mafuriko yanayoletwa na mto Msimbazi, tunaimani watatusikia na kutupa tunachihitaji.