Wanafunzi Sekondari 7,457, Msingi 1,554 wapata ujauzito

Milard Ayo
Published: Feb 01, 2023 09:00:40 EAT   |  News

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imelieleza Bunge kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 na 2022 wanafunzi 1,554 wa shule za msingi na 7,457 wa sekondari walipata ujauzito. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema takwimu hizo ni kubwa. Akaitaka hiyo wizara kuandaa takwimu kuhusu idadi ya wanaume walioshitakiwa na kupatikana na hatia ya kuwapa […]

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imelieleza Bunge kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 na 2022 wanafunzi 1,554 wa shule za msingi na 7,457 wa sekondari walipata ujauzito.

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema takwimu hizo ni kubwa. Akaitaka hiyo wizara kuandaa takwimu kuhusu idadi ya wanaume walioshitakiwa na kupatikana na hatia ya kuwapa ujauzito wanafunzi.

Dk Tulia alisema takwimu kuhusu wanaume wenye hatia ni muhimu ili kuona kama sheria ya kuwalinda watoto dhidi ya vitendo viovu inafanya kazi.

Awali wakati akijibu swali la wali la Mbunge wa Viti  Maalumu, Hawa Chakoma (CCM), Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga alisema bungeni Dodoma kuwa, wanafunzi 1,692 wa shule za sekondari wamerejeshwa shuleni baada ya kukatiza masomo kwa sababu ya ujauzito. Mbunge huyo aliuliza ni wanafunzi wangapi waliokuwa wajawa zito na wangapi wamerejeshwa shuleni baada ya agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuwataka wanafunzi wote waliopata ujauzito wakiwa shuleni warejeshwe.

Kipanga alisema idadi hiyo ni waliorudi shuleni hadi kufikia Januari mwaka huu na akasema wanaendelea kukusanya takwimu za shule za msingi.

Alisema ili kumaliza tatizo hilo serikali imeweka mikakati minne ukiwemo wa Rais Samia kuridhia kujengwa shule 26 za sekondari za wasichana moja kila mkoa.

Kipanga alisema pia mkakati wa serikali ni kuhakikisha kwamba ujenzi wa hosteli unaendelea kwenye maeneo yenye umuhimu wa kuwa na mabweni.

Aliwaeleza wabunge kuwa mkakati mwingine wa serikali ni kuanzisha vitengo vya elimu ya unasihi na ushauri katika shule mbalimbali ili kuhakikisha vitendo vya unyanyasaji havijitokezi. Pia mkakati mwingine ni kuchukua hatua kwa wale wote wanaohusika katika vitendo vya kunyanyasa wanafunzi ili wachukuliwe hatua za kinidhamu.

Kuhusu kutunga sheria, Kipanga alisema, ni kweli kuna waraka namba 2 wa 2021 wa urejeshaji wanafunzi na ni mwaka mmoja tangu umetoka hivyo wanaendelea kufanya tathmini ya utekelezaji wake na changamoto na mafanikio yaliyopo.